Ruka hadi kwenye maudhui
Sura ya 4 · Aya ya 46

An-Nisaa 4:46

النساء

مِّنَ ٱلَّذِينَ هَادُوا۟ يُحَرِّفُونَ ٱلْكَلِمَ عَن مَّوَاضِعِهِۦ وَيَقُولُونَ سَمِعْنَا وَعَصَيْنَا وَٱسْمَعْ غَيْرَ مُسْمَعٍ وَرَٰعِنَا لَيًّۢا بِأَلْسِنَتِهِمْ وَطَعْنًا فِى ٱلدِّينِ ۚ وَلَوْ أَنَّهُمْ قَالُوا۟ سَمِعْنَا وَأَطَعْنَا وَٱسْمَعْ وَٱنظُرْنَا لَكَانَ خَيْرًا لَّهُمْ وَأَقْوَمَ وَلَـٰكِن لَّعَنَهُمُ ٱللَّهُ بِكُفْرِهِمْ فَلَا يُؤْمِنُونَ إِلَّا قَلِيلًا

Maana

Miongoni mwa Mayahudi wamo wanaopotosha maneno kuyatoa pahali pake, na husema: 'Tumesikia na tumeasi, na sikia bila ya kusikizishwa.' Na husema: "Raai'naa", kwa kuzipotoa ndimi zao na kuitukana Dini. Na lau kama wangelisema: "Tumesikia na tumetii, na usikie na "Undhurna (utuangalie)," ingelikuwa heri kwao na ya unyoofu zaidi. Lakini Mwenyezi Mungu aliwalaani kwa kufuru yao; basi hawaamini isipokuwa wachache tu.

Maana: Swahili Translation - Rowad Translation Center. Issued by the Islamic Content Service Association in Languages Toleo 1.0.5, 2025-12-17. QuranEnc.com

Maana

Miongoni mwa Mayahudi wamo ambao hubadilisha maneno kuyatoa mahala pake, na husema: Tumesikia na tumeasi, na sikia bila ya kusikilizwa. Na husema: "Raai'naa", kwa kuzipotoa ndimi zao ili kuitukana Dini. Na lau kama wangeli sema: Tumesikia na tumet'ii, na usikie na "Undhurna" (Utuangalie), ingeli kuwa ni kheri kwao na sawa zaidi. Lakini Mwenyezi Mungu amewalaani kwa kufuru yao; basi hawaamini ila wachache tu. [46]

[46] Miongoni mwa Mayahudi kipo kikundi kazi yao kugeuza geuza maana ya maneno. Wao husema kimoyomoyo kumwambia Mtume s.a.w.: Tumesikia hayo maneno, na hatuifati hiyo amri. Na pia husema: Sikia maneno yetu - hukusikia wito. Wakikusudia kwa hayo kumuapiza Mtume. Na husema: Sikia bila ya kusikilizwa. Tamko hilo wanalipindua maana. Muradi wao ni kumuapiza, na wanajidai kuwa muradi wao ni kumwombea dua. Na husema: "Raai'na", wakipindua ndimi zao wakijitia kuwa wanakusudia "Undhurna" yaani "Tuangalie". Wanaonyesha kuwa wanataka uangalizi wake, na kumbe wanakusudia neno la Kiyahudi lenye maana ya "Mpumbavu" ili kuibeza Dini ya Kiislamu. Na lau kuwa wangeli nyooka sawa wakasema: "Tumesikia na tumet'ii" badala ya hiyo kauli yao ya "Tumesikia na tumeasi", na wakasema: "Sikia" na wasiseme "Bila ya kusikilizwa", na wakasema :"Undhurna" yaani "Tuangalie", badala ya "Raa'ina", ingeli kuwa bora kwao kuliko hayo wayasemayo, na ingeli kuwa ndiyo njia ya uadilifu zaidi. Lakini Mwenyezi Mungu amewatoa katika rehema yake kwa ule upinzani wao. Kwa hivyo huwaoni miongoni mwao wanao mwitikia mwenye kuwaitia Imani ila wachache tu.

Maana: Swahili Translation - Ali Mohsin Al-Barwani. Translated by Ali Mohsen Al-Barwani Toleo 1.0.1, 2025-06-25. QuranEnc.com

Maana

Miongoni mwa Mayahudi kuna kundi lililozoea kuyabadilisha maneno ya Allah Mtukufu na kuyageuza kinyume cha vile yalivyo kwa kumzulia Allah Mtukufu urongo na kusema kumwambia Mtume, rehema za Allah Mtukufu na amani zimshukiye, «Tumesikia neno lako na tumeasi amri yako, na sikia kutoka kwetu mwana kutosikia,» na wanasema, «tupe masikizi yako,» yaani, tuelewe na utufahamishe, huku wakizipotoa ndimi zao kwa hilo wakikusudia kumnasibisha na upumbavu, kulingana na lugha yao, na kuitukana dini ya Uislamu. Na lau wao wangesema, «Sami‛nã wa aṭa‛nã» (tumesikia na tumetii),» badala ya kusema «‛Aṣaynã» (tumeasi), na wangesema «Isma‛» (sikia) bila kuongeza «Ghayra musma‛» (mwana kutosikia) na wangesema, «Unẓurnã» (tuangalie na utuchunge) badala ya kusema,»Rã‛inã», ingalikuwa ni bora kwao mbele ya Allah Mtukufu na lingalikuwa ni neno la uadilifu zaidi. Lakini Allah Mtukufu Aliwatoa kwenye rehema Yake kwa sababu ya ukafiri wao na kukanusha kwao unabii wa Muhammad, rehema za Allah Mtukufu na amani zimshukiye, kwa kuwa hawaamini isipokuwa Imani chache isiyowanufaisha.

Maana: Swahili Translation - Abdullah Muhammad and Nasser Khamis. Translated by Dr. Abdullah Muhammad Abu Bakr & Shaykh Nasser Khamis Toleo 1.0.1, 2026-03-12. QuranEnc.com

An-Nisaa

Kiarabu ni maandishi ya Tanzil, bila kubadilishwa. Maana ni matoleo ya wachapishaji wake, bila kubadilishwa; wahakiki wa Sabīl wenyewe bado hawajazikagua. Kiarabu: maandishi ya Uthmani ya Tanzil, toleo la 1.1. Chanzo: tanzil.net