An-Nisaa 4:176
النساءيَسْتَفْتُونَكَ قُلِ ٱللَّهُ يُفْتِيكُمْ فِى ٱلْكَلَـٰلَةِ ۚ إِنِ ٱمْرُؤٌا۟ هَلَكَ لَيْسَ لَهُۥ وَلَدٌ وَلَهُۥٓ أُخْتٌ فَلَهَا نِصْفُ مَا تَرَكَ ۚ وَهُوَ يَرِثُهَآ إِن لَّمْ يَكُن لَّهَا وَلَدٌ ۚ فَإِن كَانَتَا ٱثْنَتَيْنِ فَلَهُمَا ٱلثُّلُثَانِ مِمَّا تَرَكَ ۚ وَإِن كَانُوٓا۟ إِخْوَةً رِّجَالًا وَنِسَآءً فَلِلذَّكَرِ مِثْلُ حَظِّ ٱلْأُنثَيَيْنِ ۗ يُبَيِّنُ ٱللَّهُ لَكُمْ أَن تَضِلُّوا۟ ۗ وَٱللَّهُ بِكُلِّ شَىْءٍ عَلِيمٌۢ
Wanakuuliza hukumu ya kisheria, sema: Mwenyezi Mungu anawapa hukumu ya kisheria juu ya kalala (mtu aliyekufa bila ya kuacha mzazi wala mwana). Ikiwa mtu amekufa, naye hana mwana, lakini anaye dada, basi huyo atapata nusu ya alichokiacha. Naye (mwanamume) atamrithi (dada yake) ikiwa hana mwana. Na ikiwa wao ni madada wawili, basi watapata theluthi mbili za alichokiacha. Na wakiwa ndugu wanaume na wanawake, basi wa kiume atapata sehemu iliyo sawa na ya wa kike wawili. Mwenyezi Mungu anawabainishia ili msipotee. Na Mwenyezi Mungu ni Mwenye kujua kila kitu.
Maana: Swahili Translation - Rowad Translation Center. Issued by the Islamic Content Service Association in Languages Toleo 1.0.5, 2025-12-17. QuranEnc.com
Wanakuomba uhukumu, sema: Mwenyezi Mungu anakupeni hukumu juu ya mkiwa. Ikiwa mtu amekufa, naye hana mtoto, lakini anaye ndugu wa kike, basi huyo atapata nusu alicho acha maiti. Na mwanamume atamrithi ndugu wa kike ikiwa hana mwana. Na ikiwa wao ni ndugu wa kike wawili, basi watapata thuluthi mbili za alicho acha maiti. Na wakiwa ndugu wanaume na wanawake, basi mwanamume atapata sehemu iliyo sawa na ya wanawake wawili. Mwenyezi Mungu anakubainishieni ili msipotee; na Mwenyezi Mungu ni Mjuzi wa kila kitu. [176]
[176] Ewe Nabii! Wanakuuliza vipi atarithiwa aliye kufa naye akawa hana mwana, wala mzazi. Sema: Hakika hukumu ya Mwenyezi Mungu katika urithi wa hawa ni kuwa, akiwa maiti ana ndugu wa kike basi atapata nusu ya tirka. Na akiwa maiti ni mwanamke naye ana ndugu wa kiume basi atarithi mali yote. Na ikiwa ameacha ndugu wawili wa kike, basi watapata hao thuluthi mbili ya urithi. Na ikiwa hao ndugu ni mchanganyiko wanaume na wanawake, basi fungu la mwanamume ni sawa na mafungu mawili ya wanawake. Mwenyezi Mungu anakubainishieni haya msije mkapotea katika kugawa mafungu ya urithi. Na Mwenyezi Mungu ni Mkamilifu wa ujuzi wa a'mali zenu na vitendo vyenu vyote. Na atakulipeni kwavyo. (Angalia: Urithi wa ndugu katika Aya hii ni wa ndugu khalisa, yaani ndugu kwa baba na mama, au ndugu kwa baba. Ama urithi wa ndugu kwa mama tu umekwisha tajwa katika Aya 12 ya Sura hii ya Annisaa.) Na Sunna (Mafunzo ya Mtume) imebainisha kuwa wakizidi kuliko ndugu wa kike wawili, pamoja na Aya ya mirathi iliyo tajwa, kuwa wakizidi kuliko binti wawili, watachukua thuluthi mbili. Ni bora kuwa zaidi kuliko ndugu wawili wa kike, kwa sababu mabinti ni karibu zaidi kwa maiti. Tuzingatie kuwa kwa mujibu wa kanuni za Kizungu za kurithi, ambazo zimetokana na kanuni ya Kirumi, ndugu wanaume wala wa kike wala watoto wao hawarithi. Na juu ya hivyo mwenye mali anayo ruhusa kumkata yeyote asipate urithi wake. Uislamu umekataza haya. Warithi lazima wapate urithi wao, ila mtu anayo haki ya kuandika wasia kujihukumia kisicho zidi thuluthi moja ya mali yake.(W.H. Ingrams katika kitabu chake Zanzibar Its History and Its People ameandika: "Hakika Sharia Takatifu yaonekana kuwa ni ya haki zaidi sana kuliko hata mpango wa Kiingereza wa kugawanya mali. Katika Zanzibar [na bila ya shaka katika Waislamu wote] hapana mwendo wa kuwa mtu "kukatwa urithi akabakishwa na shilingi moja tu"; vyo vyote vile, ni sehemu ndogo tu ndiyo inaweza kuandikiwa wasia, na yaliyo baki lazima yagawiwe kwa warithi kwa mujibu wa kiwango maalumu.")
Maana: Swahili Translation - Ali Mohsin Al-Barwani. Translated by Ali Mohsen Al-Barwani Toleo 1.0.1, 2025-06-25. QuranEnc.com
Wanakuuliza, ewe Nabii, kuhusu hukumu ya urithi wa kalãlah, naye ni aliyekufa akiwa hana mwana wala mzazi. Sema, Allah Mtukufu Anawafafanulia hukumu yake, kwamba yoyote atakayefariki na akawa hana mwana wala mzazi, na akawa ana dada yake wa kwa baba na mama au wa kwa baba tu. Basi dada huyo atapata nusu ya mali yaliyoachwa na aliyefariki. Na iwapo aliyefariki ni huyo dada, na akawa hana mwana wala mzazi, basi kaka yake, wa kwa baba na mama au wa kwa baba, atarithi mali yote. Na iwapo yule aliyefariki, bila ya kuacha mwana wala mzazi, ana dada zake wawili, basi wao watapata theluthi mbili ya mali aliyoyaacha. Na watakapokusanyika pamoja kwenye urithi ndugu wa kiume na wa kike wasiokuwa wa kwa mama, basi kila mmoja, katika ndugu wa kiume, atapata mfano wa mafungu mawili ya mwanamke. Allah Mtukufu Anawafafanulia namna ya kugawanya urithi na hukumu ya aliyefariki bila ya kuacha mwana wala mzazi, ili msije mkapotea kwenye njia ya haki kuhusu hukumu ya mambo ya urithi. Na Allah Mtukufu ni Mjuzu wa mwisho wa mambo na yaliyo na heri kwa waja Wake.
Maana: Swahili Translation - Abdullah Muhammad and Nasser Khamis. Translated by Dr. Abdullah Muhammad Abu Bakr & Shaykh Nasser Khamis Toleo 1.0.1, 2026-03-12. QuranEnc.com
Kiarabu ni maandishi ya Tanzil, bila kubadilishwa. Maana ni matoleo ya wachapishaji wake, bila kubadilishwa; wahakiki wa Sabīl wenyewe bado hawajazikagua. Kiarabu: maandishi ya Uthmani ya Tanzil, toleo la 1.1. Chanzo: tanzil.net