An-Nisaa 4:171
النساءيَـٰٓأَهْلَ ٱلْكِتَـٰبِ لَا تَغْلُوا۟ فِى دِينِكُمْ وَلَا تَقُولُوا۟ عَلَى ٱللَّهِ إِلَّا ٱلْحَقَّ ۚ إِنَّمَا ٱلْمَسِيحُ عِيسَى ٱبْنُ مَرْيَمَ رَسُولُ ٱللَّهِ وَكَلِمَتُهُۥٓ أَلْقَىٰهَآ إِلَىٰ مَرْيَمَ وَرُوحٌ مِّنْهُ ۖ فَـَٔامِنُوا۟ بِٱللَّهِ وَرُسُلِهِۦ ۖ وَلَا تَقُولُوا۟ ثَلَـٰثَةٌ ۚ ٱنتَهُوا۟ خَيْرًا لَّكُمْ ۚ إِنَّمَا ٱللَّهُ إِلَـٰهٌ وَٰحِدٌ ۖ سُبْحَـٰنَهُۥٓ أَن يَكُونَ لَهُۥ وَلَدٌ ۘ لَّهُۥ مَا فِى ٱلسَّمَـٰوَٰتِ وَمَا فِى ٱلْأَرْضِ ۗ وَكَفَىٰ بِٱللَّهِ وَكِيلًا
Enyi Watu wa Kitabu! Msipite kiasi katika dini yenu, wala msiseme juu ya Mwenyezi Mungu isipokuwa haki tu. Hakika, Masihi Isa mwana wa Maryam ni Mtume wa Mwenyezi Mungu, na neno lake tu alilomfikishia Maryam, na ni roho iliyotoka kwake. Basi Muaminini Mwenyezi Mungu na Mitume wake. Wala msiseme: 'Utatu.' Komekeni! Itakuwa heri kwenu. Hakika, Mwenyezi Mungu ni Mungu mmoja tu. Ametakasika Yeye na kuwa na mwana. Ni vyake Yeye vyote vilivyo katika mbingu na vilivyo katika ardhi. Na Mwenyezi Mungu anatosha kuwa Mtegemewa.
Maana: Swahili Translation - Rowad Translation Center. Issued by the Islamic Content Service Association in Languages Toleo 1.0.5, 2025-12-17. QuranEnc.com
Enyi Watu wa Kitabu! Msipite kiasi katika dini yenu, wala msimseme Mwenyezi Mungu ila kwa lilio kweli. Hakika Masihi Isa mwana wa Maryamu ni Mtume wa Mwenyezi Mungu, na neno lake tu alilo mpelekea Maryamu, na ni roho iliyo toka kwake. Basi Muaminini Mwenyezi Mungu na Mitume wake. Wala msiseme: Utatu. Komeni! Itakuwa kheri kwenu. Hakika Mwenyezi Mungu ni Mungu mmoja tu. Ametukuka Yeye na kuwa na mwana. Ni vyake Yeye vyote viliomo katika mbingu na katika ardhi. Na Mwenyezi Mungu ni Mtegemewa wa kutosha. [171]
[171] Enyi Watu wa Kitabu! Msipindukie haki, mkazidisha kupita kiasi katika dini yenu, wala msimzulie uwongo Mwenyezi Mungu, mkaukanya utume wa Isa, au mkamfanya kuwa ni Mungu pamoja na Mwenyezi Mungu. Kwani Masihi ni Mtume kama walivyo Mitume wengine. Mwenyezi Mungu amemuumba kwa uwezo wake na neno lake alilo mbashiria kwalo, na Jibrili akampulizia Maryamu roho ya Mwenyezi Mungu. Hii ni siri katika siri za uwezo wake Mwenyezi Mungu. Basi muaminini Mwenyezi Mungu na Mitume wake wote imani ya kweli. Wala msidai kuwa katika Ungu kuna Utatu!! Tokeni katika upotovu huu, itakuwa kheri kwenu. Hakika Mwenyezi Mungu ni Mungu mmoja tu, wala hana mshirika wake. Naye ametakasika na kuwa na mwana! Na kila kilioko katika mbingu na ardhi ni chake. Na Yeye Mwenyewe anajitosha peke yake kuwa ni Mwendeshaji wa Ufalme wake. (Kuitwa Nabii Isa Neno au Roho iliyo toka kwa Mungu, hakumpi Ungu. Yeye ni neno kwa kuumbwa kwa amri ya "Kun", "Kuwa" akawa. Haya ni kuwapinga Mayahudi walio dai kuwa yeye ni mwanaharamu. Basi wanaambiwa kuwa ameumbwa kama vilivyo umbwa vitu vyote, kwa amri ya Mwenyezi Mungu. Naye ni Roho iliyo toka kwa Mwenyezi Mungu kama walivyo pewa Waumini wote (58.22) na alivyo puliziwa Adam (15.29) na kwa hivyo wanaadamu wote (32.7-9). Hapana hata pahala pamoja katika Injili ziliomo katika Biblia ambapo Yesu (Nabii Isa a.s.) alijiita mwenyewe Mwana wa Mungu. Kila mara akijiita Mwana wa Adamu. Na alipo mwita Mungu Baba, alikusudia ni Baba wa watu wote, kama alipo sema: "Ninapaa kwenda kwa Baba yangu naye ni Baba yenu, kwa Mungu wangu naye ni Mungu wenu." Injili ya Yohana 10.33-36.)
Maana: Swahili Translation - Ali Mohsin Al-Barwani. Translated by Ali Mohsen Al-Barwani Toleo 1.0.1, 2025-06-25. QuranEnc.com
Enyi watu wa Injili! Msiikiuke itikadi ya haki katika dini yenu mkachupa mipaka na msiseme kuhusu Allah Mtukufu isipokuwa haki. Hivyo basi, msimfanye kuwa Ana mke wala msimfanye kuwa ana mwana; hakika Al-Masîḥ ‘Ǐsâ, mwana wa Maryam, ni mjumbe wa Allah Mtukufu, Allah Mtukufu amemtuma kwa haki na Amemuumba kwa neno ambalo Amemtuma nalo Jibrili alipeleke kwa Maryam, nalo ni neno Lake, «Kuwa!» na ikawa. Nalo ni mvivio kutoka kwa Allah Mtukufu, Aliyetukuka, aliouvivia Jibrili kwa amri ya Mola Wake. Kwa hivyo, aminini kwamba Allah Mtukufu ni Mmoja na mjisalimishe Kwake na muwaamini Mitume Wake katika yale waliowaletea kutoka kwa Allah Mtukufu na myafuate kivitendo. Wala msimfanye ‘Ǐsâ na mamake kuwa ni washirika wa Allah Mtukufu. Komeni na matamshi hayo! Itakuwa bora kwenu kuliko hayo mliyonayo. Hakika Allah Mtukufu ni Mola Mmoja, kutakasika na sifa za upungufu ni Kwake. Vilivyoko mbinguni na ardhini ni milki Yake. Basi vipi Atakuwa na mke au mtoto kati ya hivyo? Inatosha kuwa Allah Mtukufu Ndiye Msimamizi wa kupanga mambo ya viumbe Wake na kuendesha maisha yao. Hivyo basi, mtegemeeni, Yeye Peke Yake, kwani Yeye Ndiye Mwenye kuwatosha.
Maana: Swahili Translation - Abdullah Muhammad and Nasser Khamis. Translated by Dr. Abdullah Muhammad Abu Bakr & Shaykh Nasser Khamis Toleo 1.0.1, 2026-03-12. QuranEnc.com
Kiarabu ni maandishi ya Tanzil, bila kubadilishwa. Maana ni matoleo ya wachapishaji wake, bila kubadilishwa; wahakiki wa Sabīl wenyewe bado hawajazikagua. Kiarabu: maandishi ya Uthmani ya Tanzil, toleo la 1.1. Chanzo: tanzil.net