An-Nisaa 4:16
النساءوَٱلَّذَانِ يَأْتِيَـٰنِهَا مِنكُمْ فَـَٔاذُوهُمَا ۖ فَإِن تَابَا وَأَصْلَحَا فَأَعْرِضُوا۟ عَنْهُمَآ ۗ إِنَّ ٱللَّهَ كَانَ تَوَّابًا رَّحِيمًا
Na wawili kati yenu wafanyao hayo miongoni mwenu, waudhini. Na wakitubia wakatengenea, basi waacheni. Hakika, Mwenyezi Mungu ni Mwingi wa kupokea toba, Mwenye kurehemu.
Maana: Swahili Translation - Rowad Translation Center. Issued by the Islamic Content Service Association in Languages Toleo 1.0.5, 2025-12-17. QuranEnc.com
Na wawili kati yenu wafanyao hayo waadhibuni. Na wakitubia wakatengenea basi waacheni. Hakika Mwenyezi Mungu ni Mwingi wa kupokea toba, Mwenye kurehemu. [16]
[16] Mwanamume na mwanamke walio zini, nao hawajaoa (au kuolewa), wapewe adhabu maalumu, pindi ikithibiti hiyo zina kwa mashahidi wane waadilifu. Wakitubu baada ya kupewa adhabu, basi msiwatajie hayo maasi waliyo yatenda, wala msiwaaziri. Hakika Mwenyezi Mungu kwa rehema yake anakubali toba ya wenye kutubu.
Maana: Swahili Translation - Ali Mohsin Al-Barwani. Translated by Ali Mohsen Al-Barwani Toleo 1.0.1, 2025-06-25. QuranEnc.com
Na wawili wenye kujiingiza kwenye kitendo cha uzinifu basi waudhini kwa kuwapiga, kuwahama na kuwaaibisha. Wakitubia na kitendo walichokifanya na wakajirekebisha kwa kufanya mambo mema, wasameheni na kuacha kuwaudhi. Faida inayotokana na aya hii na ile kabla yake ni kwamba wanaume wakifanya kitendo cha uzinifu wataudhiwa., ama wanawake watafungwa na kuudhiwa. Kifungo, kikomo chake ni kifo. Na udhia, kikomo chake ni toba na kutengea. Hii ilikuwako mwanzo wa Uislamu, kisha ikaondolewa kwa Sheria iliowekwa na Allah Mtukufu na Mtume wake, nayo ni kupigwa mawe mpaka kufa, kwa yule ambaye ashaoa au ashaolewa, wakiwa wote wawili ni watu huru, waliobaleghe, wenye akili na ambao wameingilia au kuingiliwa katika ndoa sahihi. Ama wasiokuwa hao, adhabu yao ni kupigwa fimbo mia na kuhamishwa mwaka mzima. Hakika Allah Mtukufu ni Mwenye kuzikubali toba za waja Wake wanaotubia, ni Mwenye huruma kwao.
Maana: Swahili Translation - Abdullah Muhammad and Nasser Khamis. Translated by Dr. Abdullah Muhammad Abu Bakr & Shaykh Nasser Khamis Toleo 1.0.1, 2026-03-12. QuranEnc.com
Kiarabu ni maandishi ya Tanzil, bila kubadilishwa. Maana ni matoleo ya wachapishaji wake, bila kubadilishwa; wahakiki wa Sabīl wenyewe bado hawajazikagua. Kiarabu: maandishi ya Uthmani ya Tanzil, toleo la 1.1. Chanzo: tanzil.net