An-Nisaa 4:119
النساءوَلَأُضِلَّنَّهُمْ وَلَأُمَنِّيَنَّهُمْ وَلَـَٔامُرَنَّهُمْ فَلَيُبَتِّكُنَّ ءَاذَانَ ٱلْأَنْعَـٰمِ وَلَـَٔامُرَنَّهُمْ فَلَيُغَيِّرُنَّ خَلْقَ ٱللَّهِ ۚ وَمَن يَتَّخِذِ ٱلشَّيْطَـٰنَ وَلِيًّا مِّن دُونِ ٱللَّهِ فَقَدْ خَسِرَ خُسْرَانًا مُّبِينًا
Na hakika nitawapoteza, na nitawatia matamanio, na nitawaamrisha, basi hakika watakata masikio ya wanyama, na nitawaamrisha, basi hakika watabadili aliyoumba Mwenyezi Mungu. Na mwenye kumfanya Shetani kuwa ni rafiki mwandani badala ya Mwenyezi Mungu, basi hakika amehasiri hasara ya dhahiri.
Maana: Swahili Translation - Rowad Translation Center. Issued by the Islamic Content Service Association in Languages Toleo 1.0.5, 2025-12-17. QuranEnc.com
Na hakika nitawapoteza na nitawatia matamanio, na nitawaamrisha, basi watakata masikio ya wanyama, na nitawaamrisha, basi watabadili aliyo umba Mwenyezi Mungu. Na mwenye kumfanya Shet'ani kuwa ni mlinzi wake badala ya Mwenyezi Mungu, basi huyo amekhasiri khasara ya dhaahiri. [119]
[119] Hakika kiapo chake Shetani ni kuwa atawapoteza wale anao wapumbaza kwa kuwatenga mbali na Haki, na kuchochea pumbao lao na matamanio yao, mpaka wakawa wamepotea wanatanga tanga katika mawazo na tamaa za uwongo. Wakisha kuwa katika kuzainiwa huku na tamaa hizo chini ya utawala wake Shetani, tena huwatokomeza kwenye mambo yasiyo ingia akilini, na huwapelekea hao wafikiri kufanya hayo ni ibada. Na ilhali haya yote ni mawazo ya uwongo tu. Basi huwatia wasiwasi wakatenda mambo, kama kwa mfano kuwakata masikio baadhi ya ngamia wao, wageuze khulka aliyo iumba Mwenyezi Mungu. Wakafanya kuwa ngamia aliye katwa masikio yake hachinjwi, wala hafanyishwi kazi, wala hazuiliwi kwenda machungani atakavyo. Yote haya ni kwa amri yake Shetani kuwazaini. Tena huwatia wasiwasi mpaka wakaona kuwa hayo ni katika dini. Na hakika wao inakuwa wanamfuata yeye Shetani, na wanamfanya yeye ndiye wa kuwanusuru, na ndiye wa kumfuata badala ya Mwenyezi Mungu. Na mwenye kumfanya Shetani ndiye msaidizi wake wa kumfuata, basi amekhasiri khasara kubwa iliyo wazi. Kwani hapo anakuwa amepotea njia ya Haki, na ameipumbaza akili yake, na utampata ufisadi duniani, na adhabu Akhera.
Maana: Swahili Translation - Ali Mohsin Al-Barwani. Translated by Ali Mohsen Al-Barwani Toleo 1.0.1, 2025-06-25. QuranEnc.com
«Na nitawaepusha na haki wenye kunifuata, nitawaahidi kwa urongo mambo wanayoyatamani, nitawaita wayakate na kuyapasua masikio ya wanyama hoa kwa kuwapambia walifanye jambo hili la ubatili na nitawalingania wageuze umbo la Allah Mtukufu Alilowaumbia nalo katika tabia za kimaumbile na hali ya viumbe vile walivyo.» Na mwenye kukubali mwito wa Shetani na kumfanya yeye ndiye muokozi wake badala ya Allah Mtukufu, ameangamia maangamivu yaliyo wazi.
Maana: Swahili Translation - Abdullah Muhammad and Nasser Khamis. Translated by Dr. Abdullah Muhammad Abu Bakr & Shaykh Nasser Khamis Toleo 1.0.1, 2026-03-12. QuranEnc.com
Kiarabu ni maandishi ya Tanzil, bila kubadilishwa. Maana ni matoleo ya wachapishaji wake, bila kubadilishwa; wahakiki wa Sabīl wenyewe bado hawajazikagua. Kiarabu: maandishi ya Uthmani ya Tanzil, toleo la 1.1. Chanzo: tanzil.net