An-Nisaa 4:11
النساءيُوصِيكُمُ ٱللَّهُ فِىٓ أَوْلَـٰدِكُمْ ۖ لِلذَّكَرِ مِثْلُ حَظِّ ٱلْأُنثَيَيْنِ ۚ فَإِن كُنَّ نِسَآءً فَوْقَ ٱثْنَتَيْنِ فَلَهُنَّ ثُلُثَا مَا تَرَكَ ۖ وَإِن كَانَتْ وَٰحِدَةً فَلَهَا ٱلنِّصْفُ ۚ وَلِأَبَوَيْهِ لِكُلِّ وَٰحِدٍ مِّنْهُمَا ٱلسُّدُسُ مِمَّا تَرَكَ إِن كَانَ لَهُۥ وَلَدٌ ۚ فَإِن لَّمْ يَكُن لَّهُۥ وَلَدٌ وَوَرِثَهُۥٓ أَبَوَاهُ فَلِأُمِّهِ ٱلثُّلُثُ ۚ فَإِن كَانَ لَهُۥٓ إِخْوَةٌ فَلِأُمِّهِ ٱلسُّدُسُ ۚ مِنۢ بَعْدِ وَصِيَّةٍ يُوصِى بِهَآ أَوْ دَيْنٍ ۗ ءَابَآؤُكُمْ وَأَبْنَآؤُكُمْ لَا تَدْرُونَ أَيُّهُمْ أَقْرَبُ لَكُمْ نَفْعًا ۚ فَرِيضَةً مِّنَ ٱللَّهِ ۗ إِنَّ ٱللَّهَ كَانَ عَلِيمًا حَكِيمًا
Mwenyezi Mungu anawausia juu ya watoto wenu: Fungu la mwanamume ni kama fungu la wanawake wawili. Na wakiwa ni wanawake zaidi ya wawili, basi wana theluthi mbili za alichokiacha maiti. Lakini akiwa mtoto mwanamke ni mmoja, basi fungu lake ni nusu. Na kwa wazazi wake wawili, kila mmoja wao apate sudusi moja katika kile alichokiacha, ikiwa ana mtoto. Na ikiwa hana mtoto, na wazazi wake wawili wakawa wanamrithi, basi mama yake atapata theluthi moja. Na ikiwa ana ndugu, basi mama yake atapata sudusi. Haya ni baada ya kutolewa alichousia au kulipa deni. Baba zenu na watoto wenu, nyinyi hamjui ni nani kati yao aliyekaribu zaidi kwenu kwa manufaa. Hiyo ni sheria iliyotoka kwa Mwenyezi Mungu. Bila ya shaka, Mwenyezi Mungu ni Mwenye kujua, Mwenye hekima.
Maana: Swahili Translation - Rowad Translation Center. Issued by the Islamic Content Service Association in Languages Toleo 1.0.5, 2025-12-17. QuranEnc.com
Mwenyezi Mungu anakuusieni juu ya watoto wenu: Fungu la mwanamume ni kama fungu la wanawake wawili. Na ikiwa wanawake zaidi ya wawili, basi watapata thuluthi mbili za alicho kiacha maiti. Lakini akiwa mtoto mwanamke ni mmoja, basi fungu lake ni nusu. Na wazazi wake wawili, kila mmoja wao apate sudusi ya alicho kiacha, ikiwa anaye mtoto. Akiwa hana mtoto, na wazazi wake wawili wamekuwa ndio warithi wake, basi mama yake atapata thuluthi moja. Na akiwa anao ndugu, basi mama yake atapata sudusi. Haya ni baada ya kutolewa alicho usia au kulipa deni. Baba zenu na watoto wenu, nyinyi hamjui ni nani baina yao aliye karibia zaidi kwenu kwa manufaa. Hiyo ni Sharia iliyo toka kwa Mwenyezi Mungu. Bila ya shaka Mwenyezi Mungu ni Mjuzi na Mwenye hikima. [11]
[11] Mwenyezi Mungu anakuamrisheni katika mambo ya kuwarithisha watoto wenu na wazazi wenu, pindi mtakapo kufa, kwa njia inayo leta uadilifu na maslaha. Nayo ni kuwa sehemu ya mwanamume ni sawa na sehemu ya wanawake wawili, ikiwa watoto wanao rithi ni wanaume na wanawake. Ikiwa watoto wote ni wanawake watupu, na idadi yao imezidi wawili, basi sehemu yao ni thuluthi mbili za tirka, yaani mali yaliyo achwa na maiti. Inafahamika katika madhumuni ya Aya kuwa fungu la binti wawili ni kama fungu la walio zidi hapo. Na akiwa mtu amemuacha binti mmoja tu, basi fungu lake ni nusu ya alicho kiacha. Na akiwa mtu amemuacha baba na mama, basi kila mmojapo kati ya hao atapata sudusi, yaani sehemu moja katika sita, ikiwa huyo maiti alikuwa na mtoto mmoja - mwanamume au mwanamke - pamoja na hao wazazi wake. Akiwa hana mtoto na wakamrithi wazazi wake tu, basi mama sehemu yake ni thuluthi, na kilicho baki ni cha baba. Na ikiwa huyo maiti alikuwa na ndugu, basi mama yake atapata sudusi na kilicho baki ni cha baba, na wale ndugu hawapati chochote. Mafungu hayo hupewa wanao stahiki baada ya kwisha lipwa deni lilio kuwa juu ya maiti, na kutimiza yale aliyo yausia katika mipaka aliyo ruhusu Mwenyezi Mungu. Hii ni hukumu ya Mwenyezi Mungu. Na huu ndio uadilifu na ndio hikima. Na nyinyi hamjui ni nani kwenu mwenye manufaa zaidi kwenu, baina ya wazazi na wana. Na kheri khasa ni aliyo yaamrisha Mwenyezi Mungu, kwani Yeye ndiye Mwenye kuyajua maslaha yenu, na ndiye Mwenye hikima katika yale aliyo kulazimisheni.
Maana: Swahili Translation - Ali Mohsin Al-Barwani. Translated by Ali Mohsen Al-Barwani Toleo 1.0.1, 2025-06-25. QuranEnc.com
Allah Mtukufu Anawausia na kuwaamrisha, kuhusu wana wenu atakapokufa mmoja wenu na akaacha watoto wa kiume na wa kike, kwamba urithi wote ni wao: mtoto wa kiume atapata mfano wa fungu la watoto wawili wa kike, iwapo itakuwa hakuna mawarithi wengine isipokuwa ni wao tu. Iwapo atawaacha watoto wa kike peke yao, basi watoto wa kike wawili au zaidi watapata theluthi mbili ya alichokiacha. Na iwapo mrithi ni binti mmoja, basi atapata nusu ya mali, na wazazi wawili wa maiti, kila mmoja atapata sudusi. Hii ni iwapo maiti ana mtoto wa kiume au wa kike, mmoja au zaidi. Iwapo maiti hana mwana, na wakawa mawarithi wake ni wazazi wake wawili, basi mamake atapata theluthi na babake atapata kilichosalia. Na iwapo maiti ana ndugu, wawili au zaidi, wawe ni wanawake au ni wanaume, basi mamake atapata sudusi, baba atapata kilichosalia na ndugu hawatapata kitu. Mgawanyo huu wa mali yalioachwa hufanyika baada ya kutoa wasia aliousia maiti katika kiwango cha theluthi, au baada ya kutoa deni adaiwalo. Baba zenu na watoto wenu ambao wamepangiwa kurithi, hamjui ni yupi katika wao mwenye manufaaa ya ukaribu zaidi na nyinyi katika dunia yenu na Akhera yenu. Kwa hivyo, msimfanye mmoja kati yao ni bora kuliko mwengine. Hili mliousiwa nalo limefaradhiwa kwenu na Allah Mtukufu. Hakika Allah Mtukufu ni Mjuzi wa viumbe Wake, ni Mwenye hekima katika Sheria Alizowaekea.
Maana: Swahili Translation - Abdullah Muhammad and Nasser Khamis. Translated by Dr. Abdullah Muhammad Abu Bakr & Shaykh Nasser Khamis Toleo 1.0.1, 2026-03-12. QuranEnc.com
Kiarabu ni maandishi ya Tanzil, bila kubadilishwa. Maana ni matoleo ya wachapishaji wake, bila kubadilishwa; wahakiki wa Sabīl wenyewe bado hawajazikagua. Kiarabu: maandishi ya Uthmani ya Tanzil, toleo la 1.1. Chanzo: tanzil.net