An-Nisaa 4:12
النساءوَلَكُمْ نِصْفُ مَا تَرَكَ أَزْوَٰجُكُمْ إِن لَّمْ يَكُن لَّهُنَّ وَلَدٌ ۚ فَإِن كَانَ لَهُنَّ وَلَدٌ فَلَكُمُ ٱلرُّبُعُ مِمَّا تَرَكْنَ ۚ مِنۢ بَعْدِ وَصِيَّةٍ يُوصِينَ بِهَآ أَوْ دَيْنٍ ۚ وَلَهُنَّ ٱلرُّبُعُ مِمَّا تَرَكْتُمْ إِن لَّمْ يَكُن لَّكُمْ وَلَدٌ ۚ فَإِن كَانَ لَكُمْ وَلَدٌ فَلَهُنَّ ٱلثُّمُنُ مِمَّا تَرَكْتُم ۚ مِّنۢ بَعْدِ وَصِيَّةٍ تُوصُونَ بِهَآ أَوْ دَيْنٍ ۗ وَإِن كَانَ رَجُلٌ يُورَثُ كَلَـٰلَةً أَوِ ٱمْرَأَةٌ وَلَهُۥٓ أَخٌ أَوْ أُخْتٌ فَلِكُلِّ وَٰحِدٍ مِّنْهُمَا ٱلسُّدُسُ ۚ فَإِن كَانُوٓا۟ أَكْثَرَ مِن ذَٰلِكَ فَهُمْ شُرَكَآءُ فِى ٱلثُّلُثِ ۚ مِنۢ بَعْدِ وَصِيَّةٍ يُوصَىٰ بِهَآ أَوْ دَيْنٍ غَيْرَ مُضَآرٍّ ۚ وَصِيَّةً مِّنَ ٱللَّهِ ۗ وَٱللَّهُ عَلِيمٌ حَلِيمٌ
Nanyi mna nusu ya walichoacha wake zenu ikiwa hawana mtoto. Lakini ikiwa wana mtoto, basi mna robo katika kile walichokiacha, baada ya wasia waliyousia au kulipa deni. Na wake zenu wana robo katika kile mlichokiacha, ikiwa hamna mtoto. Lakini ikiwa mna mtoto, basi wana thumuni katika kile mlichokiacha, baada ya wasia mliousia au kulipa deni. Na ikiwa mwanamume au mwanamke anayerithiwa hana mtoto wala wazazi, lakini anaye kaka au dada, basi kila mmoja wao ana sudusi. Na wakiwa zaidi kuliko hivyo, basi watashirikiana katika theluthi, baada ya wasia iliyousiwa au kulipa deni, pasi na kuleta madhara. Huu ndio wasia uliotoka kwa Mwenyezi Mungu. Na Mwenyezi Mungu ni Mwenye kujua, Mstahamilivu.
Maana: Swahili Translation - Rowad Translation Center. Issued by the Islamic Content Service Association in Languages Toleo 1.0.5, 2025-12-17. QuranEnc.com
Na fungu lenu ni nusu walicho acha wake zenu ikiwa hawana mtoto. Wakiwa na mtoto basi fungu lenu ni robo ya walicho acha, baada ya wasia waliyo usia au kulipa deni. Na wake zenu watapata robo mlicho kiacha, ikiwa hamna mtoto. Mkiwa mna mtoto basi sehemu yao ni thumni ya mlicho kiacha, baada ya wasia mlio usia au kulipa deni. Na ikiwa mwanamume au mwanamke anaye rithiwa hana mtoto wala wazazi, lakini anaye ndugu mume au ndugu mke, basi kila mmoja katika hawa atapata sudusi. Na wakiwa zaidi kuliko hivyo basi watashirikiana katika thuluthi, baada ya wasia ulio usiwa au kulipa deni, pasio kuleta dhara. Huu ndio wasia ulio toka kwa Mwenyezi Mungu. Na Mwenyezi Mungu ni Mjuzi na Mpole. [12]
[12] Fungu la mume ni nusu ya alicho acha mke ikiwa huyo mke hakuacha mtoto kutokana na mume huyo au mwenginewe. Akiwa huyo mke ana mtoto, basi mumewe atapata robo baada ya kutolewa wasia aliye uusia huyo mwanamke au kulipwa deni lake. Na fungu la mke au wake ni robo ya alicho acha mume ikiwa hakuacha mtoto kwa wake hao au wenginewe. Akiwa anaye mwana kutokana na hao au wake wenginewe basi mke huyu au wake hawa watapata thumni ya tirka baada ya wasia alio usia au deni. Na mwana wa mwana, yaani mjukuu, ni kama mwana katika haya yaliyo tangulia. Na akiwa maiti ni mwanamume au mwanamke, naye hana mwana wala mzazi, na kamwacha ndugu mume kwa mama, au ndugu wawili wa kike kwa mama, basi kila mmoja wao atapata sudusi, yaani sehemu moja katika sita. Na wakiwa wengi kuliko hivyo watashirikiana katika thuluthi, watagawana sawa sawa wanaume na wanawake kwa mujibu wa ushirika, baada ya kulipa madeni yaliyo kuwa juu yake, na kutimiza wasia ambao haudhuru urithi, nao ni wasia usio pindukia thuluthi iliyo baki baada ya kulipa madeni. Basi, enyi Waumini! Jilazimisheni kufuata aliyo kuusieni Mwenyezi Mungu; kwani Yeye hakika ni Mwenye kujua vyema nani miongoni mwenu anaye dhulumu na nani anaye fanya uadilifu, Yeye ni Mpole hafanyi haraka kutoa adhabu.
Maana: Swahili Translation - Ali Mohsin Al-Barwani. Translated by Ali Mohsen Al-Barwani Toleo 1.0.1, 2025-06-25. QuranEnc.com
Na nyinyi, enyi wanaume, muna nusu ya kilioachwa na wake zenu baada ya kufa kwao, iwapo hawana watoto wa kiume au wa kike, na ikiwa wana watoto, basi mtapata robo ya walichokiacha ambacho mtakirithi baada ya kutekeleza wasia wao unaofaa au baada ya kulipa deni lao kwa wastahiki. Na wake zenu, enyi waume, watapata robo ya mlichokiacha iwapo hamuna mwana wa kiume au wa kike kutoka kwao, hao wake zenu, au wengineo mliokuwa mumewaoa. Na iwapo mtakuwa na mwana wa kiume au wa kike, basi hao wake zenu watapata thumni ya mlichokiacha. Hiyo robo au thumni itagawanywa kati yao; na iwapo ni mke mmoja, basi hiyo robo au thumni itakuwa ndio fungu lake. Hii ni baada ya kutekeleza kile mlichousia kitekelezwe katika nyasia zifaazo, au kulipa deni lenu. Na iwapo mwanamume au mwanamke atakufa, na akawa hana mwana wala mzazi, na akawa na ndugu mmoja wa kwa mama, wa kiume au wa kike, basi kila mmoja kati yao wawili atapata sudusi; wakiwa ni zaidi ya mmoja watashirikiana katika theluthi itakayogawanywa baina yao kwa usawa bila kutafautisha baina ya mwanamume na mwanamke. Hili ndilo fungu Alilowaekea Allah Mtukufu ndugu wa kwa mama, wa kiume na wa kike, likiwa ni urithi wao, baada ya kutekeleza wasia wa aliyekufa iwapo aliusia chochote ambacho hakina madhara kwa mawarithi au baada ya kulipa madeni yake. Kwa hili Amewausia Mola wenu, wasia wenye manufaa kwenu. Na Allah Mtukufu ni Mjuzi mno kwa yanayowafaa viumbe Wake, ni Mpole, Hana haraka ya kuwaadhibu.
Maana: Swahili Translation - Abdullah Muhammad and Nasser Khamis. Translated by Dr. Abdullah Muhammad Abu Bakr & Shaykh Nasser Khamis Toleo 1.0.1, 2026-03-12. QuranEnc.com
Kiarabu ni maandishi ya Tanzil, bila kubadilishwa. Maana ni matoleo ya wachapishaji wake, bila kubadilishwa; wahakiki wa Sabīl wenyewe bado hawajazikagua. Kiarabu: maandishi ya Uthmani ya Tanzil, toleo la 1.1. Chanzo: tanzil.net