Ruka hadi kwenye maudhui
Sura ya 4 · Aya ya 102

An-Nisaa 4:102

النساء

وَإِذَا كُنتَ فِيهِمْ فَأَقَمْتَ لَهُمُ ٱلصَّلَوٰةَ فَلْتَقُمْ طَآئِفَةٌ مِّنْهُم مَّعَكَ وَلْيَأْخُذُوٓا۟ أَسْلِحَتَهُمْ فَإِذَا سَجَدُوا۟ فَلْيَكُونُوا۟ مِن وَرَآئِكُمْ وَلْتَأْتِ طَآئِفَةٌ أُخْرَىٰ لَمْ يُصَلُّوا۟ فَلْيُصَلُّوا۟ مَعَكَ وَلْيَأْخُذُوا۟ حِذْرَهُمْ وَأَسْلِحَتَهُمْ ۗ وَدَّ ٱلَّذِينَ كَفَرُوا۟ لَوْ تَغْفُلُونَ عَنْ أَسْلِحَتِكُمْ وَأَمْتِعَتِكُمْ فَيَمِيلُونَ عَلَيْكُم مَّيْلَةً وَٰحِدَةً ۚ وَلَا جُنَاحَ عَلَيْكُمْ إِن كَانَ بِكُمْ أَذًى مِّن مَّطَرٍ أَوْ كُنتُم مَّرْضَىٰٓ أَن تَضَعُوٓا۟ أَسْلِحَتَكُمْ ۖ وَخُذُوا۟ حِذْرَكُمْ ۗ إِنَّ ٱللَّهَ أَعَدَّ لِلْكَـٰفِرِينَ عَذَابًا مُّهِينًا

Maana

Na unapokuwa miongoni mwao, na ukawasimamishia Swala, basi kundi moja miongoni mwao lisimame pamoja nawe, na wachukue silaha zao. Na watakapomaliza kusujudu, basi na wawe nyuma yenu, na lije kundi lingine ambalo halijaswali, na waswali pamoja nawe, nao wachukue hadhari yao na silaha zao. Walipenda wale waliokufuru lau mghafilike mbali na silaha zenu na mizigo yenu ili wawavamie mvamio wa mara moja. Wala hakuna ubaya juu yenu ikiwa mnaona udhia kwa sababu ya mvua au mkawa wagonjwa, mkaziweka silaha zenu. Na chukueni hadhari yenu. Hakika, Mwenyezi Mungu amewaandalia makafiri adhabu ya kudunisha.

Maana: Swahili Translation - Rowad Translation Center. Issued by the Islamic Content Service Association in Languages Toleo 1.0.5, 2025-12-17. QuranEnc.com

Maana

Na unapo kuwa pamoja nao, ukawasalisha, basi kundi moja miongoni mwao wasimame pamoja nawe na wachukue silaha zao. Na watakapo maliza sijida zao, basi nawende nyuma yenu, na lije kundi jingine ambalo halijasali, lisali pamoja nawe. Nao wachukue hadhari yao na silaha zao. Walio kufuru wanapenda mghafilike na silaha zenu na vifaa vyenu ili wakuvamieni mvamio wa mara moja. Wala si vibaya kwenu ikiwa mnaona udhia kwa sababu ya mvua au mkawa wagonjwa, mkaziweka silaha zenu. Na chukueni hadhari yenu. Hakika Mwenyezi Mungu amewaandalia makafiri adhabu ya kudhalilisha. [102]

[102] Ewe Nabii Muaminifu, ukiwa nao na Swala ya Jamaa inasaliwa, msisahau kutahadhari na maadui. Na hayo ni kuwagawa Waislamu makundi mawili. Moja lianze kuswali kwa kukufuata wewe, na wakati huo la pili lisimame kwa hadhari na silaha likilinda vifaa. Ukisha nusu ya Swala, kundi lilio sali nawe lende nyuma yako, na lije jengine lisali nawe Swala iliyo bakia. Kisha litimize sehemu waliyo ikosa. Na lile la kwanza lisali baki ya Swala. Na hii huitwa "Laahiqah", yaani iliyo kutwa na nyengine inaitwa "Masbuuqah", yaani iliyo tanguliwa ,kwa kuwa inasaliwa mwanzo wa Swala ya Jamaa; na "Laahiqah" inasaliwa mwisho wa Swala ya Jamaa. Mpango huu ni kwa sababu isikosekane Swala, na kutahadhari na makafiri ambao wanapenda mghafilike na silaha zenu na vifaa vyenu wapate kukuvamieni kwa ghafla, na wakumalizeni nanyi mmo katika Swala. Vita na washirikina ni waajibu, na havina ukomo. Lakini hapana dhambi juu yenu kusita kwa ajili ya udhuru kama mvua au maradhi, juu ya kuwa lazima muwe na hadhari ya kudumu. Na hii ni adhabu ya Mwenyezi Mungu kwa makafiri hapa duniani, na Akhera amewaandalia adhabu ya fedheha na udhalili. "Laahiq" ni anaye swali na Imam mwanzo wa Swala na akalazimika kusali iliyo baki peke yake, na "Masbuuq" anaye iwahi sehemu ya mwisho ya Swala ya Jamaa, kisha akatimiza sehemu aliyo ikosa peke yake.

Maana: Swahili Translation - Ali Mohsin Al-Barwani. Translated by Ali Mohsen Al-Barwani Toleo 1.0.1, 2025-06-25. QuranEnc.com

Maana

Na ukiwa, ewe Nabii, kwenye kiwanja cha vita na ukataka kuswalisha, basi kundi moja lisimame nawe ili kuswali, huku wakiwa wameshika silaha zao. Watu wa kundi hili wakiwa kwenye sijda, basi lije kundi lingine liwe nyuma yenu likiwa limeelekea upande wa adui wenu. Watu wa kundi la kwanza watimize rakaa ya pili na kutoa salamu. Kisha watu wa kundi lingine, ambalo bado halijaanza kuswali, waje kukufuata katika rakaa yao ya kwanza, kisha wamalize wenyewe rakaa yao ya pili. Na wajihadhari na adui wao na washike silaha zao. Kwani wenye kukanusha dini ya Allah Mtukufu wanatamani mughafilike na silaha zenu na vyombo vyenu wapate kuwashambulia kwa mara moja na kuwaua. Na hamuna makosa, kukiwa na mvua yenye kuwasumbua au mkawa wagonjwa, kuacha silaha zenu pamoja na kuwa na hadhari. Hakika Allah Mtukufu, Amewaandalia wenye kuikanusha dini Yake adhabu ya kuwatweza na kuwadhalilisha.

Maana: Swahili Translation - Abdullah Muhammad and Nasser Khamis. Translated by Dr. Abdullah Muhammad Abu Bakr & Shaykh Nasser Khamis Toleo 1.0.1, 2026-03-12. QuranEnc.com

An-Nisaa

Kiarabu ni maandishi ya Tanzil, bila kubadilishwa. Maana ni matoleo ya wachapishaji wake, bila kubadilishwa; wahakiki wa Sabīl wenyewe bado hawajazikagua. Kiarabu: maandishi ya Uthmani ya Tanzil, toleo la 1.1. Chanzo: tanzil.net