Al-Ahzaab 33:53
الأحزابيَـٰٓأَيُّهَا ٱلَّذِينَ ءَامَنُوا۟ لَا تَدْخُلُوا۟ بُيُوتَ ٱلنَّبِىِّ إِلَّآ أَن يُؤْذَنَ لَكُمْ إِلَىٰ طَعَامٍ غَيْرَ نَـٰظِرِينَ إِنَىٰهُ وَلَـٰكِنْ إِذَا دُعِيتُمْ فَٱدْخُلُوا۟ فَإِذَا طَعِمْتُمْ فَٱنتَشِرُوا۟ وَلَا مُسْتَـْٔنِسِينَ لِحَدِيثٍ ۚ إِنَّ ذَٰلِكُمْ كَانَ يُؤْذِى ٱلنَّبِىَّ فَيَسْتَحْىِۦ مِنكُمْ ۖ وَٱللَّهُ لَا يَسْتَحْىِۦ مِنَ ٱلْحَقِّ ۚ وَإِذَا سَأَلْتُمُوهُنَّ مَتَـٰعًا فَسْـَٔلُوهُنَّ مِن وَرَآءِ حِجَابٍ ۚ ذَٰلِكُمْ أَطْهَرُ لِقُلُوبِكُمْ وَقُلُوبِهِنَّ ۚ وَمَا كَانَ لَكُمْ أَن تُؤْذُوا۟ رَسُولَ ٱللَّهِ وَلَآ أَن تَنكِحُوٓا۟ أَزْوَٰجَهُۥ مِنۢ بَعْدِهِۦٓ أَبَدًا ۚ إِنَّ ذَٰلِكُمْ كَانَ عِندَ ٱللَّهِ عَظِيمًا
Enyi mlioamini, msiingie katika nyumba za Nabii isipokuwa mpewe ruhusa kwenda kula chakula, siyo kungojea kiive. Lakini mtakapoitwa, basi ingieni, na mkishakula, tawanyikeni, wala msiweke hapo mazungumzo. Hakika hayo yanamuudhi Nabii, naye anawastahi, lakini Mwenyezi Mungu hastahi kwa jambo la haki. Na mnapowauliza wakeze haja, waulizeni kwa nyuma ya mapazia. Hivyo ndivyo usafi zaidi kwa nyoyo zenu na nyoyo zao. Wala haikufailiini kumuudhi Mtume wa Mwenyezi Mungu, wala kuwaoa wake zake baada yake kabisa. Hakika jambo hilo ni kubwa mbele ya Mwenyezi Mungu.
Maana: Swahili Translation - Rowad Translation Center. Issued by the Islamic Content Service Association in Languages Toleo 1.0.5, 2025-12-17. QuranEnc.com
Enyi mlio amini! Msiingie nyumba za Nabii ila mpewe ruhusa kwenda kula, sio kungojea kiwive. Lakini mtakapo itwa basi ingieni, na mkisha kula tawanyikeni, wala msiweke mazungumzo. Hakika hayo yanamuudhi Nabii naye anakustahini, lakini Mwenyezi Mungu hastahi kwa jambo la haki. Na mnapo wauliza wakeze haja waulizeni nyuma ya mapazia. Hivyo ndio usafi zaidi kwa nyoyo zenu na nyoyo zao. Wala haikufalieni kumuudhi Mtume wa Mwenyezi Mungu, wala kuwaoa wake zake baada yake kabisa. Hakika jambo hilo ni kubwa mbele ya Mwenyezi Mungu. [53]
[53] Enyi mlio amini! Msiingie nyumba za Nabii ila kwa idhini yake kwa ajili ya kwenda kula chakula, bila ya kwenda kungoja wakati mpaka kitapo kuwa tayari. Lakini Mtume akikuiteni, basi ingieni. Na mkisha kula ondokeni. Wala msikae baada yake mkijizoeza mazungumzo nyinyi kwa nyinyi. Kwani hakika kuingia bila ya idhini yake, na kukaa muda mrefu baada ya kwisha kula, kunamuudhi Nabii, naye anakustahini hawezi kukutakeni mtoke. Lakini Mwenyezi Mungu Mtukufu hana la kumzuia asiitangaze haki kama wanavyo zuilikana viumbe. Na mtakapo wauliza wake za Nabii s.a.w. haja yoyote, basi waulizeni nyuma ya mapazia. Hivyo ni usafi bora kwa nyoyo zenu na nyoyo zao zisiingiwe na uchochezi wa Shetani. Na haikufaliini nyinyi kumuudhi Mtume wa Mwenyezi Mungu, wala kuwaoa wake zake baada yake milele, kwa sababu ya hishima yake na yao. Hakika jambo hilo ni dhambi kubwa kwa Mwenyezi Mungu. Yanarejea maelezo ya ki-ilimu juu ya Aya mbili 58, na 59 za Surat An-nur, katika yaliyo khusu adabu za kuzuru.
Maana: Swahili Translation - Ali Mohsin Al-Barwani. Translated by Ali Mohsen Al-Barwani Toleo 1.0.1, 2025-06-25. QuranEnc.com
Enyi mliomuamini Allah Mtukufu na Mtume Wake na mkazifuata Sheria Zake kivitendo, msiingie nyumba za Mtume, isipokuwa kwa ruhusa yake, kwa kula chakula bila ya kungoja kuiva kwake. Lakini mkiitwa ingieni, na mkimaliza kula ondokeni, bila ya kujipumbaza kwa mazungumzo baina yenu. Kwani kule kungoja kwenu na kujipumbaza kwenu kunamkera Nabii, naye anawaonea haya kuwatoa kwenye hizo nyumba pamoja na kuwa hiyo ni haki yake, na Allah Mtukufu Haoni haya kuieleza haki na kuidhihirisha. Na mkiwaomba wake za Mtume, (rehema za Allah Mtukufu na amani zimshukie), wawapatie kitu chochote mnachokihitajia katika vyombo vya nyumbani na mfano wake, basi waombeni mkiwa nyuma ya pazia. Kufanya kwenu hivyo kunatakasa zaidi nyoyo zenu na nyoyo zao na kuziepusha na mawazo ambayo yanawapitia wanaume kuhusu mambo ya wanawake na wanawake kuhusu mambo ya wanaume, kwani kuona ndio sababu ya kufitinika. Na haifai kwenu kumkera Mtume wa Allah Mtukufu wala kuwaoa wake zake baada ya kufa kwake kabisa, kwa kuwa wao ni mama zenu, na haifai mtu kumuoa mama yake. Hakika kumkera kwenu Mtume wa Allah Mtukufu, (rehema za Allah Mtukufu na amani zimshukie), na kuwaoa wake zake baada yake ni dhambi kubwa kwa Allah Mtukufu. Ummah huu ulitekeleza amri hii na ulijiepusha na kile Allah Mtukufu Aliukataza nacho.
Maana: Swahili Translation - Abdullah Muhammad and Nasser Khamis. Translated by Dr. Abdullah Muhammad Abu Bakr & Shaykh Nasser Khamis Toleo 1.0.1, 2026-03-12. QuranEnc.com
Kiarabu ni maandishi ya Tanzil, bila kubadilishwa. Maana ni matoleo ya wachapishaji wake, bila kubadilishwa; wahakiki wa Sabīl wenyewe bado hawajazikagua. Kiarabu: maandishi ya Uthmani ya Tanzil, toleo la 1.1. Chanzo: tanzil.net