Al-Ahzaab 33:50
الأحزابيَـٰٓأَيُّهَا ٱلنَّبِىُّ إِنَّآ أَحْلَلْنَا لَكَ أَزْوَٰجَكَ ٱلَّـٰتِىٓ ءَاتَيْتَ أُجُورَهُنَّ وَمَا مَلَكَتْ يَمِينُكَ مِمَّآ أَفَآءَ ٱللَّهُ عَلَيْكَ وَبَنَاتِ عَمِّكَ وَبَنَاتِ عَمَّـٰتِكَ وَبَنَاتِ خَالِكَ وَبَنَاتِ خَـٰلَـٰتِكَ ٱلَّـٰتِى هَاجَرْنَ مَعَكَ وَٱمْرَأَةً مُّؤْمِنَةً إِن وَهَبَتْ نَفْسَهَا لِلنَّبِىِّ إِنْ أَرَادَ ٱلنَّبِىُّ أَن يَسْتَنكِحَهَا خَالِصَةً لَّكَ مِن دُونِ ٱلْمُؤْمِنِينَ ۗ قَدْ عَلِمْنَا مَا فَرَضْنَا عَلَيْهِمْ فِىٓ أَزْوَٰجِهِمْ وَمَا مَلَكَتْ أَيْمَـٰنُهُمْ لِكَيْلَا يَكُونَ عَلَيْكَ حَرَجٌ ۗ وَكَانَ ٱللَّهُ غَفُورًا رَّحِيمًا
Ewe Nabii, tumekuhalalishia wake zako uliowapa mahari yao, na uliowamiliki kwa mkono wako wa kulia katika wale aliokupa Mwenyezi Mungu, na mabinti wa ami zako, na mabinti wa shangazi zako, na mabinti wa wajomba zako, na mabinti wa dada za mama yako waliohama pamoja nawe; na mwanamke Muumini akijitoa mwenyewe kwa Nabii, kama mwenyewe Nabii akitaka kumuoa. Ni halali kwako wewe tu, si kwa Waumini wengine. Sisi tunajua tuliyowafaradhishia wao katika wake zao na wanawake iliyowamiliki mikono yao ya kulia, ili isiwe dhiki kwao. Na Mwenyezi Mungu ni Mwenye kusamehe, Mwenye kurehemu.
Maana: Swahili Translation - Rowad Translation Center. Issued by the Islamic Content Service Association in Languages Toleo 1.0.5, 2025-12-17. QuranEnc.com
Ewe Nabii! Tumekuhalalishia wake zako ulio wapa mahari yao, na ulio wamiliki kwa mkono wako wa kulia katika alio kupa Mwenyezi Mungu, na mabinti ami zako, na mabinti wa shangazi zako, na mabinti wa wajomba zako, na mabinti wa dada za mama yako walio hama pamoja nawe; na mwanamke Muumini akijitoa mwenyewe kwa Nabii, kama mwenyewe Nabii akitaka kumwoa. Ni halali kwako wewe tu, si kwa Waumini wengine. Sisi tunajua tuliyo wafaridhia wao katika wake zao na wanawake ilio wamiliki mikono yao ya kulia. Ili isiwe dhiki kwao. Na Mwenyezi Mungu ni Mwenye kusamehe, Mwenye kurehemu. [50]
[50] Ewe Nabii! Hakika Sisi tumekuhalalishia wake zako ulio wapa mahari. Na tumekuhalishia wajakazi ulio wamiliki mkono wako wa kulia, katika alio kuneemeshea Mwenyezi Mungu. Na tumekuhalalishia kuwaoa mabinti ami zako, na mabinti wa shangazi zako, na mabinti wa wajomba zako, na mabinti wa dada, yaani ndugu wa kike, wa mama yako, walio hama nawe. Na tumekuhalalishia mwanamke Muumini akijitolea nafsi yake bila ya mahari, nawe ikawa unataka kumwoa na umempenda. Kujitolea huku ni kwako wewe tu, si kwa Waumini wengine. Kwao haifai hivyo. Tunajua hukumu tulizo wafaridhia Waumini kwa wake zao na wajakazi wao, na tuliyo kuruhusu wewe, si wao, ili isiwe dhiki juu yako kwa tuliyo kuhukumia. Na Mwenyezi Mungu ni Mwenye kusamehe madhambi ya waja wake, Mwenye kuwarehemu kwa ukunjufu.
Maana: Swahili Translation - Ali Mohsin Al-Barwani. Translated by Ali Mohsen Al-Barwani Toleo 1.0.1, 2025-06-25. QuranEnc.com
Ewe Nabii! Tumekuhalalishia wake uliowapa mahari yao, na tumekuhalalishia wajakazi waliomilikiwa na mkono wako miongoni mwa wale ambao Allah Mtukufu Amekuneemesha nao, na tumekuhalalishia kuwaoa watoto wa kike wa ami zako na watoto wa kike wa shangazi zako na watoto wa kike wa khalati zako waliohama (kuja Madina) pamoja na wewe, na tumekuhalalishia mwanamke Muumini aliyekutunukia nafsi yake bila mahari, iwapo unataka kumuoa, hili ni lako wewe peke yako, na haifai kwa asiyekuwa wewe kumuoa mwanamke kwa kutunukiwa. Tushajua kile tulichowaelekeza Waumini kuhusu wake zao na wajakazi wao kuwa wasioe isipokuwa wake wanne, idadi wanayoitaka ya wajakazi na ulazima wa walii, mahari na mashahidi juu yao. Lakini tumekuruhusu wewe na tumekupa nafasi ambayo hatukumpa mtu mwingine asiyekuwa wewe, ili kifua chako kisiingie dhiki juu ya kuwaoa wale uliowaoa kati ya aina hizi. Hii ni miongoni mwa ziada ya utunzaji wa Allah Mtukufu kwa Mtume Wake, (rehema za Allah Mtukufu na amani zimshukie), na takrima Yake kwake. Na Allah Mtukufu ni Mwingi wa kusamehe dhambi za waja Wake Waumini, ni Mwenye huruma kwa kuwapanulia (milango ya riziki) .
Maana: Swahili Translation - Abdullah Muhammad and Nasser Khamis. Translated by Dr. Abdullah Muhammad Abu Bakr & Shaykh Nasser Khamis Toleo 1.0.1, 2026-03-12. QuranEnc.com
Kiarabu ni maandishi ya Tanzil, bila kubadilishwa. Maana ni matoleo ya wachapishaji wake, bila kubadilishwa; wahakiki wa Sabīl wenyewe bado hawajazikagua. Kiarabu: maandishi ya Uthmani ya Tanzil, toleo la 1.1. Chanzo: tanzil.net