Al-Ahzaab 33:37
الأحزابوَإِذْ تَقُولُ لِلَّذِىٓ أَنْعَمَ ٱللَّهُ عَلَيْهِ وَأَنْعَمْتَ عَلَيْهِ أَمْسِكْ عَلَيْكَ زَوْجَكَ وَٱتَّقِ ٱللَّهَ وَتُخْفِى فِى نَفْسِكَ مَا ٱللَّهُ مُبْدِيهِ وَتَخْشَى ٱلنَّاسَ وَٱللَّهُ أَحَقُّ أَن تَخْشَىٰهُ ۖ فَلَمَّا قَضَىٰ زَيْدٌ مِّنْهَا وَطَرًا زَوَّجْنَـٰكَهَا لِكَىْ لَا يَكُونَ عَلَى ٱلْمُؤْمِنِينَ حَرَجٌ فِىٓ أَزْوَٰجِ أَدْعِيَآئِهِمْ إِذَا قَضَوْا۟ مِنْهُنَّ وَطَرًا ۚ وَكَانَ أَمْرُ ٱللَّهِ مَفْعُولًا
Na ulipomwambia yule ambaye Mwenyezi Mungu alimneemesha, nawe ukamneemesha: Shikamana na mkeo, na mche Mwenyezi Mungu. Na ukaficha nafsini mwako aliyotaka Mwenyezi Mungu kuyafichua, nawe ukawachelea watu, hali Mwenyezi Mungu ndiye mwenye haki zaidi kumchelea. Basi Zaid alipokwisha haja naye, tulikuoza wewe, ili isiwe taabu kwa Waumini kuwaoa wake wa watoto wao wa kupanga watapokuwa wamekwisha timiza nao shuruti za talaka. Na amri ya Mwenyezi Mungu ni yenye kutekelezwa.
Maana: Swahili Translation - Rowad Translation Center. Issued by the Islamic Content Service Association in Languages Toleo 1.0.5, 2025-12-17. QuranEnc.com
Na ulipo mwambia yule Mwenyezi Mungu aliye mneemesha, nawe ukamneemesha: Shikamana na mkeo, na mche Mwenyezi Mungu. Na ukaficha nafsini mwako aliyo taka Mwenyezi Mungu kuyafichua, nawe ukawachelea watu, hali Mwenyezi Mungu ndiye mwenye haki zaidi kumchelea. Basi Zaid alipo kwisha haja naye tulikuoza wewe, ili isiwe taabu kwa Waumini kuwaoa wake wa watoto wao wa kupanga watapo kuwa wamekwisha timiza nao shuruti za t'alaka. Na amri ya Mwenyezi Mungu ni yenye kutekelezwa. [37]
[37] Na kumbuka pale ulipo mwambia Zaid bin Haritha, ambaye Mwenyezi Mungu amemneemesha kwa kumwongoa kwenye Uislamu, na wewe ukamneemesha kwa kumlea na kumkomboa utumwani: Shikamana na mkeo, Zainab binti Jahsh, na umche Mwenyezi Mungu, na vumilia kukaa naye. Na wewe ulikuwa unaficha nafsini mwako ambayo Mwenyezi Mungu atakuja yadhihirisha, yaani kuwa yeye atampa t'alaka na wewe utakuja muwoa. Nawe ukakhofu watu wasije kukulaumu. Na Mwenyezi Mungu ndiye anaye stahiki umkhofu, ijapo kuwa hayo ni mashaka juu yako. Basi Zaid alipo kwisha haja naye, na akampa t'alaka kujiondolea dhiki ya kuishi naye, tukakuoza wewe, ili iwe ni chanzo cha kuvunja ada iliyo mbovu. Baada ya hayo hapana ubaya tena kwa Waislamu kuwaoa walio kuwa wake za walio kuwa wamewapanga utoto, baada ya kwisha wat'aliki. Na amri ya Mwenyezi Mungu aitakayo ni lazima iwe bila ya pingamizi.
Maana: Swahili Translation - Ali Mohsin Al-Barwani. Translated by Ali Mohsen Al-Barwani Toleo 1.0.1, 2025-06-25. QuranEnc.com
Na kumbuka pindi uliposema, ewe Nabii, kumwambia yule ambaye Allah Mtukufu Amemneemesha kwa Uislamu, naye ni Zayd bin Ḥārithah ambaye mtume, (rehema na amani zimshukie), alimuacha huru na akamfanya mwanawe na akamneemesha kwa kumuacha huru, «Baki na mke wako, Zaynab binti Jaḥsh, na usimuache! na muogope Allah Mtukufu, ewe Zayd!» na huku unaficha, ewe Nabii, katika nafsi yako kile Alichokuletea wahyi nacho Allah Mtukufu cha Zayd kumuacha Zaynab na kuwa wewe utamuoa. Na Allah Mtukufu, Aliyetukuka, ni Mwenye kudhihirisha ulichokificha, na unaogopa wasije wanafiki wakasema kwamba Muhammad amemuoa mtalaka wa mwanawe wa kupachika, na Allah Mtukufu Anastahiki zaidi umuogope. Basi Zayd alipomaliza haja yake kwa Zaynab na akamuacha kisha eda yake ikamalizika, tulikuoza wewe, ili uwe ni kiigizo katika kubatilisha mila ya uharamishaji wa kuoa mke wa mtoto wa kujipachika baada ya kuachwa, wala haitakuwa kosa na dhambi kwa Wamini kuwaoa wake wa wale watoto wao wa kujipachika baada kuwaacha iwapo wamemaliza haja yao kwao. Na kwa hakika amri ya Allah Mtukufu ni yenye kufanyika, hakuna mwenye kuiwekea pingamizi wala kuizuia. Ada ya kujipachika mtoto ilikuwako zama za ujahiliya (kabla ya Uislamu) kisha ikabatilishwa kwa neno lake Allah Mtukufu, «Waiteni wao kwa kuwanasibisha na baba zao».
Maana: Swahili Translation - Abdullah Muhammad and Nasser Khamis. Translated by Dr. Abdullah Muhammad Abu Bakr & Shaykh Nasser Khamis Toleo 1.0.1, 2026-03-12. QuranEnc.com
Kiarabu ni maandishi ya Tanzil, bila kubadilishwa. Maana ni matoleo ya wachapishaji wake, bila kubadilishwa; wahakiki wa Sabīl wenyewe bado hawajazikagua. Kiarabu: maandishi ya Uthmani ya Tanzil, toleo la 1.1. Chanzo: tanzil.net