Aal-i-Imraan 3:7
آل عمرانهُوَ ٱلَّذِىٓ أَنزَلَ عَلَيْكَ ٱلْكِتَـٰبَ مِنْهُ ءَايَـٰتٌ مُّحْكَمَـٰتٌ هُنَّ أُمُّ ٱلْكِتَـٰبِ وَأُخَرُ مُتَشَـٰبِهَـٰتٌ ۖ فَأَمَّا ٱلَّذِينَ فِى قُلُوبِهِمْ زَيْغٌ فَيَتَّبِعُونَ مَا تَشَـٰبَهَ مِنْهُ ٱبْتِغَآءَ ٱلْفِتْنَةِ وَٱبْتِغَآءَ تَأْوِيلِهِۦ ۗ وَمَا يَعْلَمُ تَأْوِيلَهُۥٓ إِلَّا ٱللَّهُ ۗ وَٱلرَّٰسِخُونَ فِى ٱلْعِلْمِ يَقُولُونَ ءَامَنَّا بِهِۦ كُلٌّ مِّنْ عِندِ رَبِّنَا ۗ وَمَا يَذَّكَّرُ إِلَّآ أُو۟لُوا۟ ٱلْأَلْبَـٰبِ
Yeye ndiye aliyeteremsha juu yako Kitabu hiki. Ndani yake zimo Aya muhkam (zenye maana wazi). Hizo ndizo msingi wa Kitabu hiki. Na zimo nyingine Mutashabihat (zenye maana zisizo wazi). Ama wale ambao katika nyoyo zao umo upotovu, wao wanafuata zile zenye maana zisizo wazi kwa kutafuta fitina, na kutafuta kupotoa maana yake. Na wala hapana ajuaye maana yake isipokuwa Mwenyezi Mungu. Na wale waliokita katika elimu husema: Sisi tumeziamini, zote zimetoka kwa Mola wetu Mlezi. Lakini hawakumbuki (hayo) isipokuwa wenye akili ya hali ya juu.
Maana: Swahili Translation - Rowad Translation Center. Issued by the Islamic Content Service Association in Languages Toleo 1.0.5, 2025-12-17. QuranEnc.com
Yeye ndiye aliye kuteremshia Kitabu hichi. Ndani yake zimo Aya muhkam, zenye maana wazi. Hizo ndizo msingi wa Kitabu hichi. Na ziko nyengine za mifano. Ama wale ambao nyoyoni mwao umo upotovu wanafuata zile za mifano kwa kutafuta fitna, na kutafuta maana yake; na wala hapana ajuaye maana yake ila Mwenyezi Mungu. Na wale wenye msingi madhubuti katika ilimu husema: Sisi tumeziamini, zote zimetoka kwa Mola wetu Mlezi. Lakini hawakumbuki hayo isipo kuwa wenye akili. [7]
[7] Na Yeye Mwenyezi Mungu ndiye aliye kuteremshia wewe, Muhammad, hii Qur'ani. Na ni katika hikima yake kufanya ndani yake mna Aya zilizo wazi, maana yake na makusudio yake yanajuulikana wepesi. Hizi ndio msingi, ndio asli. Marejeo yote yawe juu ya hizi. Na zipo Aya nyengine za mifano, za mshabaha, zenye kutatanisha. Wengi hawawezi kuzielewa. Na wale ambao hawakubobea, hawakuzama katika ilimu, huwababaisha. Na zimeteremka hizi Aya za mifano ili wanazuoni wachungue kutafuta ilimu ndani yake, na wazingatie, na wazidi kufikiri katika jitihadi, na kufanya uchunguzi katika Dini. Lakini mtindo wa walio iacha Haki ni kutaka kuzifuata hizo Aya za mifano ili kutaka kuchochea fitna, na huzifasiri kwa kufuata matamanio yao. Na hapana anaye jua maana ya Aya hizi kwa hakika ila Mwenyezi Mungu, na wale walio thibiti kweli katika ilimu. Na hao walio thibiti husema: "Sisi tuna yakini kuwa hayo yanatokana na Mwenyezi Mungu. Sisi hatufarikishi katika kuiamini Qur'ani baina ya sehemu zilizo wazi (Muhkam) na zile za mifano (Mutashaabih). Na hawazingatii ila watu wenye akili iliyo nzima, ambayo haifuati pumbao na matamanio.
Maana: Swahili Translation - Ali Mohsin Al-Barwani. Translated by Ali Mohsen Al-Barwani Toleo 1.0.1, 2025-06-25. QuranEnc.com
Yeye Peke Yake Ndiye Ambaye Aliyekuteremshia Qur’ani ambayo katika hiyo kuna aya zenye maana yaliyo wazi; hizo ndizo msingi wa Kitabu ambao unategemewa ikitokea tashwishi, na ambao chochote kinachohalifiana nao kinarudishwa na kuoanishwa nao. Na katika hiyo kuna aya zingine mutashãbihãt: zinazoleta tashwishi kwa kuwa zinabeba zaidi ya maana mamoja, kwa namna ambayo haiwezekani kujuwa maana iliyokusudiwa isipokuwa kwa kuziambatanisha na muḥkam: aya zenye maana yaliyo wazi. Basi wenye nyoyo zenye ugonjwa zilizopotoka, kwa ubaya wa nia zao, huzifuata hizi aya zenye tashwishi peke yake, ili kutia tashwishi kwa watu kwa lengo la kuwapoteza kwa kuzifasiri kuambatana na madhehebu yao yaliyo batili. Ilihali hakuna ajuwaye uhakika wa maana ya aya hizi isipokuwa Allah Mtukufu. Na wale waliozama kwenye elimu wanasema, «Tumeiamini hii Qur’ani, kwani yote imetujia kutoka kwa Mola wetu kwa ulimi wa Mtume Wake Muhammad, rehema za Allah Mtukufu na amani zimshukie,.» na wanairudisha yenye tashwishi katika Qur’ani na kuiyoanisha na iliyo wazi yake. Hakika ni kwamba wanaoyafahamu na kuyazingatia maana kama ilivyo sahihi ipasavyo ni wale wenye akili timamu.
Maana: Swahili Translation - Abdullah Muhammad and Nasser Khamis. Translated by Dr. Abdullah Muhammad Abu Bakr & Shaykh Nasser Khamis Toleo 1.0.1, 2026-03-12. QuranEnc.com
Kiarabu ni maandishi ya Tanzil, bila kubadilishwa. Maana ni matoleo ya wachapishaji wake, bila kubadilishwa; wahakiki wa Sabīl wenyewe bado hawajazikagua. Kiarabu: maandishi ya Uthmani ya Tanzil, toleo la 1.1. Chanzo: tanzil.net