Aal-i-Imraan 3:195
آل عمرانفَٱسْتَجَابَ لَهُمْ رَبُّهُمْ أَنِّى لَآ أُضِيعُ عَمَلَ عَـٰمِلٍ مِّنكُم مِّن ذَكَرٍ أَوْ أُنثَىٰ ۖ بَعْضُكُم مِّنۢ بَعْضٍ ۖ فَٱلَّذِينَ هَاجَرُوا۟ وَأُخْرِجُوا۟ مِن دِيَـٰرِهِمْ وَأُوذُوا۟ فِى سَبِيلِى وَقَـٰتَلُوا۟ وَقُتِلُوا۟ لَأُكَفِّرَنَّ عَنْهُمْ سَيِّـَٔاتِهِمْ وَلَأُدْخِلَنَّهُمْ جَنَّـٰتٍ تَجْرِى مِن تَحْتِهَا ٱلْأَنْهَـٰرُ ثَوَابًا مِّنْ عِندِ ٱللَّهِ ۗ وَٱللَّهُ عِندَهُۥ حُسْنُ ٱلثَّوَابِ
Basi, Mola wao Mlezi akayakubali maombi yao akayajibu: Hakika Mimi, sipotezi matendo ya mfanya matendo yeyote miongoni mwenu, akiwa mwanamume au mwanamke, kwani ni nyinyi kwa nyinyi. Basi waliohama, na waliotolewa katika makazi yao, na wakaudhiwa katika Njia yangu, na wakapigana vita, na wakauliwa, kwa yakini Mimi nitawafunikia makosa yao; na kwa yakini nitawaingiza katika Mabustani yanayopita mito chini yake. Hizo ndizo thawabu zinazotoka kwa Mwenyezi Mungu. Na Mwenyezi Mungu kwake kuna thawabu njema kabisa.
Maana: Swahili Translation - Rowad Translation Center. Issued by the Islamic Content Service Association in Languages Toleo 1.0.5, 2025-12-17. QuranEnc.com
Mola Mlezi wao, akayakubali maombi yao akajibu: Hakika sipotezi kazi ya mfanya kazi miongoni mwenu, akiwa mwanamume au mwanamke, kwani ni nyinyi kwa nyinyi. Basi walio hama, na walio tolewa makwao, na wakateswa katika Njia yangu, na wakapigana, na wakauliwa, kwa yakini Mimi nitawafutia makosa yao, na kwa yakini nitawaingiza katika Mabustani yanayo pita mito kati yake. Hayo ndiyo malipo yanayo toka kwa Mwenyezi Mungu. Na Mwenyezi Mungu kwake yapo malipo mema kabisa. [195]
[195] Mola wao Mlezi aliwaitikia dua yao, akiwabainishia kuwa Yeye hampotezei mtendaji thawabu za vitendo vyake, sawa sawa akiwa mwanamume au mwanamke, kwani mwanamke anatokana na mwanamume, na mwanamume anatokana na mwanamke. Basi wale walio hajiri, wakahama, wakagura, wanatafuta radhi ya Mwenyezi Mungu, na wakatolewa makwao, na wakapata mateso katika Sabili Llahi, Njia ya Mwenyezi Mungu, wakapigana vita, na wakakhatirisha kuuwawa, bali wakauliwa walio uliwa, Mwenyezi Mungu amejilazimisha Mwenyewe kuwasamehe madhambi yao, na kuwatia kwenye Mabustani yenye kupita kati yake mito, kuwa ni malipo matukufu yaliyo bora kutokana na Mwenyezi Mungu. Na kwa Mwenyezi Mungu peke yake, ndio yako malipo mazuri.
Maana: Swahili Translation - Ali Mohsin Al-Barwani. Translated by Ali Mohsen Al-Barwani Toleo 1.0.1, 2025-06-25. QuranEnc.com
Na Allah Mtukufu Akaitikia maombi yao kwamba Yeye Hazipotezi juhudi za yoyote aliyetenda amali njema, awe ni mwanamume au ni mwanamke. Kwani wao, katika undugu wa kidini, kukubaliwa amali zao na kulipwa kwazo, ni sawa. Kwa hivyo, wale waliohama kwa kutaka radhi za Allah Mtukufu, wakatolewa kwenye majumba yao, wakaudhiwa katika kumtii Mola wao na kumuabudu kwao Yeye Peke Yake, wakapigana na wakauawa Katika njia ya Allah Mtukufu kwa kulikuza neno Lake, hao Allah Mtukufu Atawapa sitara kwa maasia waliyoyafanya kama Alivyowasitiri nayo duniani na Hatawahesabu kwayo. Na atawaingiza, tena Atawaingiza, kwenye mabustani ya Peponi ambayo inapita mito chini ya majumba yake ya fahari na miti yake. Hayo yakiwa ni malipo kutoka kwa Allah Mtukufu. Na kwa Allah Mtukufu kuna malipo mazuri.
Maana: Swahili Translation - Abdullah Muhammad and Nasser Khamis. Translated by Dr. Abdullah Muhammad Abu Bakr & Shaykh Nasser Khamis Toleo 1.0.1, 2026-03-12. QuranEnc.com
Kiarabu ni maandishi ya Tanzil, bila kubadilishwa. Maana ni matoleo ya wachapishaji wake, bila kubadilishwa; wahakiki wa Sabīl wenyewe bado hawajazikagua. Kiarabu: maandishi ya Uthmani ya Tanzil, toleo la 1.1. Chanzo: tanzil.net