Ruka hadi kwenye maudhui
Sura ya 3 · Aya ya 154

Aal-i-Imraan 3:154

آل عمران

ثُمَّ أَنزَلَ عَلَيْكُم مِّنۢ بَعْدِ ٱلْغَمِّ أَمَنَةً نُّعَاسًا يَغْشَىٰ طَآئِفَةً مِّنكُمْ ۖ وَطَآئِفَةٌ قَدْ أَهَمَّتْهُمْ أَنفُسُهُمْ يَظُنُّونَ بِٱللَّهِ غَيْرَ ٱلْحَقِّ ظَنَّ ٱلْجَـٰهِلِيَّةِ ۖ يَقُولُونَ هَل لَّنَا مِنَ ٱلْأَمْرِ مِن شَىْءٍ ۗ قُلْ إِنَّ ٱلْأَمْرَ كُلَّهُۥ لِلَّهِ ۗ يُخْفُونَ فِىٓ أَنفُسِهِم مَّا لَا يُبْدُونَ لَكَ ۖ يَقُولُونَ لَوْ كَانَ لَنَا مِنَ ٱلْأَمْرِ شَىْءٌ مَّا قُتِلْنَا هَـٰهُنَا ۗ قُل لَّوْ كُنتُمْ فِى بُيُوتِكُمْ لَبَرَزَ ٱلَّذِينَ كُتِبَ عَلَيْهِمُ ٱلْقَتْلُ إِلَىٰ مَضَاجِعِهِمْ ۖ وَلِيَبْتَلِىَ ٱللَّهُ مَا فِى صُدُورِكُمْ وَلِيُمَحِّصَ مَا فِى قُلُوبِكُمْ ۗ وَٱللَّهُ عَلِيمٌۢ بِذَاتِ ٱلصُّدُورِ

Maana

Kisha baada ya dhiki aliwateremshia utulivu - usingizi ambao ulifunika kundi moja kati yenu. Na kundi jingine nafsi zao ziliwashughulisha hata wakamdhania Mwenyezi Mungu dhana isiyokuwa ya haki, dhana ya kijinga. Wakisema: Je, sisi tuna lolote katika jambo hili? Sema: Jambo hili lote ni la Mwenyezi Mungu. Wanaficha katika nafsi zao wasiyokudhihirishia. Wanasema: Lau ingelikuwa tuna lolote katika jambo hili, tusingeuliwa papa hapa. Sema: Hata mngelikuwa majumbani mwenu, basi wangelitoka wale walioandikiwa kufa, wakaenda mahali pao pa kuangukia wafe. (Haya ni hivyo) ili Mwenyezi Mungu ayajaribu yaliyo katika vifua vyenu, na asafishe yaliyo katika nyoyo zenu. Na Mwenyezi Mungu anayajua vyema yaliyomo vifuani.

Maana: Swahili Translation - Rowad Translation Center. Issued by the Islamic Content Service Association in Languages Toleo 1.0.5, 2025-12-17. QuranEnc.com

Maana

Kisha baada ya dhiki alikuteremshieni utulivu - usingizi ambao ulifunika kundi moja kati yenu. Na kundi jengine nafsi zao ziliwashughulisha hata wakamdhania Mwenyezi Mungu dhana isiyo kuwa ya haki, dhana ya kijinga. Wakisema: Hivyo tuna lolote sisi katika jambo hili? Sema: Mambo yote ni ya Mwenyezi Mungu. Wanaficha katika nafsi zao wasiyo kubainishia. Wanasema: Lau ingelikuwa tuna lolote katika jambo hili tusinge uliwa hapa. Sema: Hata mngeli kuwa majumbani mwenu, basi wangeli toka walio andikiwa kufa, wakenda mahali pao pa kuangukia wafe. (Haya ni hivyo) ili Mwenyezi Mungu ayajaribu yaliyomo vifuani mwenu, na asafishe yaliyomo nyoyoni mwenu. Na Mwenyezi Mungu anayajua yaliyomo vifuani. [154]

[154] Kisha Mwenyezi Mungu baada ya dhiki akakupeni neema ya utulivu, ambao ulidhihiri kwa usingizi ulio wafunika wale walio wa kweli katika Imani yao na kumtegemea kwao Mwenyezi Mungu. Ama kile kikundi kingine, hamu yao ni juu ya nafsi zao tu hawana jenginelo; kwa hivyo wakamdhania Mwenyezi Mungu dhana mbovu za kijahiliya, wakisema kwa kuchukiwa: Tumepata ushindi wowote sisi huo tulio ahidiwa? Sema ewe Nabii: Mambo yote ya kushinda na kushindwa yako kwa Mwenyezi Mungu. Yeye ndiye mwenye kuyaendesha mambo kwa waja wake pindi wao wakichukua khatua za ushindi, au wakifanya mambo ya kusabibisha kushindwa. Na wao wanapo sema hayo wana jambo wanalo lificha katika nafsi zao, wala hawalidhihirishi. Kwani wao husema: Ingeli kuwa sisi tuna khiari yetu tusingeli toka, basi tusingeli shindwa. Waambie: Hata mngeli kuwa ndani ya majumba yenu na kama wapo walio andikiwa kuuliwa basi hapana shaka wangeli toka mpaka pahala pao pa kufa wakauliwa. Na Mwenyezi Mungu amefanya aliyo yafanya hapo Uhud kwa maslaha makubwa, ili apate kutoa ndani yenu ikhlasi, na azitahirishe nyoyo zenu. Na Mwenyezi Mungu anayajua vilivyo yaliyo fichika ndani ya nyoyo zenu.

Maana: Swahili Translation - Ali Mohsin Al-Barwani. Translated by Ali Mohsen Al-Barwani Toleo 1.0.1, 2025-06-25. QuranEnc.com

Maana

Kisha ikawa ni katika rehema za Allah Mtukufu kwa waumini waliomtakasia nia kwamba Aliingiza kwenye nyoyo zao, baada ya kero na usumbufu uliowafika, utulivu na Imani thabiti kuhusu ahadi ya Allah Mtukufu kwao. Miongoni mwa alama za utulivu huo ni usingizi uliolifinika kundi katika wao, nalo ni lile la wale waliokuwa na ikhlasi na yakini kwa Mola wao. Na kundi lingine ilikuwa hamu ya watu wake ni kuziokoa nafsi zao; azma yao ilikuwa dhaifu, wakashughulishwa na nafsi zao na wakawa na dhana mbaya kwa Mola wao, kwa Dini Yake na kwa Mtume Wake. Wakadhani kwamba Allah Mtukufu Hatalitimiza jambo la Mtume Wake na kwamba Uislamu hautasimama ukaimarika. Kwa hivyo, utawaona ni wenye majuto juu ya kutoka kwao. Na huwa wakiambiana wao kwa wao, «Je tulikuwa na chaguo lolote katika kutoka kwetu kwenda kupigana?» Waambie, ewe Mtume, «Mambo yote ni ya Allah Mtukufu. Yeye Ndiye Aliyepanga kutoka kwenu na (Ndiye Aliyepanga yale) yaliyowafikia.» Nao wanayaficha katika nafsi zao wasiyoyadhihirisha kwako ya majuto juu ya kutoka kwao kwenda mapiganoni. Huwa wakisema, «Lau kama tungalikuwa na hiyari japo ndogo, hatungeuawa hapa.» Waambie, «Ajali ziko mikononi mwa Allah Mtukufu. Hata kama mngekuwa majumbani mwenu, na Allah Mtukufu Akakadiria mufe, wangalitoka wale ambao Allah Mtukufu Amewakadiria mauti, kwenda pale watakapouawa.» Na Hakuyafanya hayo Allah Mtukufu isipokuwa ni kuwapa nyinyi mtihani juu ya yaliyomo ndani ya vifua vyenu ya shaka na unafiki na ili Ampambanue mwema na muovu na lipate kudhihirika kwa watu jambo la Muumini na lile la mnafiki, la maneno na vitendo. Allah Mtukufu ni Mjuzi zaidi wa yaliyomo kwenye nyoyo za viumbe Wake. Hakuna chochote, katika mambo yao, kinachofichika Kwake.

Maana: Swahili Translation - Abdullah Muhammad and Nasser Khamis. Translated by Dr. Abdullah Muhammad Abu Bakr & Shaykh Nasser Khamis Toleo 1.0.1, 2026-03-12. QuranEnc.com

Aal-i-Imraan

Kiarabu ni maandishi ya Tanzil, bila kubadilishwa. Maana ni matoleo ya wachapishaji wake, bila kubadilishwa; wahakiki wa Sabīl wenyewe bado hawajazikagua. Kiarabu: maandishi ya Uthmani ya Tanzil, toleo la 1.1. Chanzo: tanzil.net