Aal-i-Imraan 3:153
آل عمرانإِذْ تُصْعِدُونَ وَلَا تَلْوُۥنَ عَلَىٰٓ أَحَدٍ وَٱلرَّسُولُ يَدْعُوكُمْ فِىٓ أُخْرَىٰكُمْ فَأَثَـٰبَكُمْ غَمًّۢا بِغَمٍّ لِّكَيْلَا تَحْزَنُوا۟ عَلَىٰ مَا فَاتَكُمْ وَلَا مَآ أَصَـٰبَكُمْ ۗ وَٱللَّهُ خَبِيرٌۢ بِمَا تَعْمَلُونَ
Pale mlipokuwa mkikimbia mbio, wala hamumsikilizi yeyote, na Mtume anawaita, yuko nyuma yenu. Basi Mwenyezi Mungu akawapa dhiki juu ya dhiki, ili msisikitike kwa yale yaliyowakosa wala kwa yale yaliyowapata. Na Mwenyezi Mungu ana habari za yote mnayoyatenda.
Maana: Swahili Translation - Rowad Translation Center. Issued by the Islamic Content Service Association in Languages Toleo 1.0.5, 2025-12-17. QuranEnc.com
Pale mlipo kuwa mkikimbia mbio wala hamumsikilizi yeyote, na Mtume anakuiteni, yuko nyuma yenu. Mwenyezi Mungu akakupeni dhiki juu ya dhiki, ili msisikitike kwa yaliyo kukoseeni wala kwa yaliyo kusibuni. Na Mwenyezi Mungu anazo khabari za yote mnayo yatenda. [153]
[153] Enyi Waumini! Hebu ikumbukeni hali yenu wakati ule mlipo kuwa mkitoka mbio wala hamumsikii mtu kwa shida ya kukimbia; na Mtume anakuiteni nyuma yenu mrejee. Mwenyezi Mungu akakujazini huzuni ya kufudikiza kama wingu lilio funika nafsi zenu, ili msisikitike kwa ngawira mlizo zikosa wala kushindwa kuliko kusibuni. Na Mwenyezi Mungu anajua vyema makusudio yenu na vitendo vyenu.
Maana: Swahili Translation - Ali Mohsin Al-Barwani. Translated by Ali Mohsen Al-Barwani Toleo 1.0.1, 2025-06-25. QuranEnc.com
Kumbukeni, enyi maswahaba wa Muhammad, rehema za Allah Mtukufu na amani zimshukie, hali zenu zilivyokuwa, mlipokuwa mnalipanda jabali mkiwakimbia maadui zenu, wala hamgeuki kumwangalia yoyote kwa sababu ya yale yaliyowafikia ya babaiko, kuogopa na fazaa. Na huku Mtume wa Allah Mtukufu, rehema za Allah Mtukufu na amani zimshukie, amekita kwenye uwanja wa vita, anawaita nyuma yenu kwa kuwaambia, «Njooni kwangu, enyi waja wa Allah Mtukufu,» hali ya kuwa nyinyi hamsikii wala hamuangalii. Hapo yakawa malipo yenu ni kupatwa na machungu, dhiki na kero. Aliyafanya hayo Allah Mtukufu ili msihuzunike kwa mliyoyakosa ya ushindi na ngawira wala yaliyowafikia ya kuingiwa na woga na kushindwa. Allah Mtukufu ni Mtambuzi wa matendo yenu yote; hakuna chochote katika hayo kinachofichika Kwake.
Maana: Swahili Translation - Abdullah Muhammad and Nasser Khamis. Translated by Dr. Abdullah Muhammad Abu Bakr & Shaykh Nasser Khamis Toleo 1.0.1, 2026-03-12. QuranEnc.com
Kiarabu ni maandishi ya Tanzil, bila kubadilishwa. Maana ni matoleo ya wachapishaji wake, bila kubadilishwa; wahakiki wa Sabīl wenyewe bado hawajazikagua. Kiarabu: maandishi ya Uthmani ya Tanzil, toleo la 1.1. Chanzo: tanzil.net