Aal-i-Imraan 3:152
آل عمرانوَلَقَدْ صَدَقَكُمُ ٱللَّهُ وَعْدَهُۥٓ إِذْ تَحُسُّونَهُم بِإِذْنِهِۦ ۖ حَتَّىٰٓ إِذَا فَشِلْتُمْ وَتَنَـٰزَعْتُمْ فِى ٱلْأَمْرِ وَعَصَيْتُم مِّنۢ بَعْدِ مَآ أَرَىٰكُم مَّا تُحِبُّونَ ۚ مِنكُم مَّن يُرِيدُ ٱلدُّنْيَا وَمِنكُم مَّن يُرِيدُ ٱلْـَٔاخِرَةَ ۚ ثُمَّ صَرَفَكُمْ عَنْهُمْ لِيَبْتَلِيَكُمْ ۖ وَلَقَدْ عَفَا عَنكُمْ ۗ وَٱللَّهُ ذُو فَضْلٍ عَلَى ٱلْمُؤْمِنِينَ
Na Mwenyezi Mungu aliwatimilizia ahadi yake, vile mlivyokuwa mnawaua kwa idhini yake, mpaka mlipolegea na mkazozana katika amri hii, na mkaasi baada ya Yeye kuwaonyesha yale mnayoyapenda. Wapo miongoni mwenu wanaotaka dunia, na wapo miongoni mwenu wanaotaka Akhera. Kisha akawatenga nao (maadui) ili akujaribuni. Naye sasa amekwishawasamehe. Na Mwenyezi Mungu ni Mwenye fadhila juu ya Waumini.
Maana: Swahili Translation - Rowad Translation Center. Issued by the Islamic Content Service Association in Languages Toleo 1.0.5, 2025-12-17. QuranEnc.com
Na Mwenyezi Mungu alikutimilizieni miadi yake, vile mlivyo kuwa mnawauwa kwa idhini yake, mpaka mlipo legea na mkazozana juu ya amri, na mkaasi baada ya Yeye kukuonyesheni mliyo yapenda. Wapo miongoni mwenu wanao taka dunia, na wapo miongoni mwenu wanao taka Akhera. Kisha akakutengeni nao (maadui) ili akujaribuni. Naye sasa amekwisha kusameheni. Na Mwenyezi Mungu ni Mwenye fadhila juu ya Waumini. [152]
[152] Nusura ya Mwenyezi Mungu ni jambo la hakika ya kweli. Mwenyezi Mungu ametimiza miadi yake kuwa alikupeni ushindi pale mara ya kwanza mlipo wauwa maadui wengi kwa radhi yake; mpaka yalipo dhoofika maoni yenu katika vita na mkakhitalifiana kuifahamu amri ya Nabii aliyo kupeni msiondoke kwenye vituo vyenu. Baadhi yenu mkaacha vituo vyenu mlipo ona mnashinda, na wengine wakabaki mpaka mwisho. Kikundi kimoja kikaasi amri ya Mtume kikenda kuwania ngawira baada ya kwisha kuonyeshwa mkipendacho, nao ni ushindi. Mkawa makundi mawili, wanao taka raha ya dunia, na wanao taka malipo ya Akhera. Ilivyo kuwa hivyo Mwenyezi Mungu akaondoa kwenu nusura yake, mkashindwa, ili akujaribuni, atambulikane mwenye ikhlasi na asiye kuwa nayo. Lakini sasa amekusameheni kwa kuwa mmejuta. Na Mwenyezi Mungu ana fadhila kwenu kwa kukusameheni na kukubali toba yenu.
Maana: Swahili Translation - Ali Mohsin Al-Barwani. Translated by Ali Mohsen Al-Barwani Toleo 1.0.1, 2025-06-25. QuranEnc.com
Na kwa hakika Aliwahakikishia nyinyi Allah Mtukufu yale Aliyowaahidi ya kuwanusuru pindi mlipokuwa mnawaua makafiri katika vita vya Uhud kwa idhini Yake Allah Mtukufu. Mpaka mlipokuwa waoga, mkawa madhaifu wa kupigana na mkatafautiana: je, mtasalia kwenye sehemu zenu za kivita au mtaziacha, ili mkusanye ngawira pamoja na wanaokusanya? Na mkaiasi amri ya Mtume wenu alipowaamrisha msiondoke kwenye sehemu zenu kwa vyovyote vile. Hapo ndipo pigo la kushindwa likawapata baada ya kuwaonesha mnayoyapenda ya ushindi, na ikadhihirika kuwa kati yenu kuna wanaotaka ngawira na kati yenu kuna wanaotaka Akhera na malipo yake. Kisha Allah Mtukufu Aliziepusha nyuso zenu na maadui wenu ili awape mtihani. Kwa hakika Aliyajua Allah Mtukufu majuto yenu na toba yenu, ndipo Akawasamehe. Na Allah Mtukufu ni Mwenye fadhila kubwa kwa Waumini.
Maana: Swahili Translation - Abdullah Muhammad and Nasser Khamis. Translated by Dr. Abdullah Muhammad Abu Bakr & Shaykh Nasser Khamis Toleo 1.0.1, 2026-03-12. QuranEnc.com
Kiarabu ni maandishi ya Tanzil, bila kubadilishwa. Maana ni matoleo ya wachapishaji wake, bila kubadilishwa; wahakiki wa Sabīl wenyewe bado hawajazikagua. Kiarabu: maandishi ya Uthmani ya Tanzil, toleo la 1.1. Chanzo: tanzil.net