An-Noor 24:35
النورٱللَّهُ نُورُ ٱلسَّمَـٰوَٰتِ وَٱلْأَرْضِ ۚ مَثَلُ نُورِهِۦ كَمِشْكَوٰةٍ فِيهَا مِصْبَاحٌ ۖ ٱلْمِصْبَاحُ فِى زُجَاجَةٍ ۖ ٱلزُّجَاجَةُ كَأَنَّهَا كَوْكَبٌ دُرِّىٌّ يُوقَدُ مِن شَجَرَةٍ مُّبَـٰرَكَةٍ زَيْتُونَةٍ لَّا شَرْقِيَّةٍ وَلَا غَرْبِيَّةٍ يَكَادُ زَيْتُهَا يُضِىٓءُ وَلَوْ لَمْ تَمْسَسْهُ نَارٌ ۚ نُّورٌ عَلَىٰ نُورٍ ۗ يَهْدِى ٱللَّهُ لِنُورِهِۦ مَن يَشَآءُ ۚ وَيَضْرِبُ ٱللَّهُ ٱلْأَمْثَـٰلَ لِلنَّاسِ ۗ وَٱللَّهُ بِكُلِّ شَىْءٍ عَلِيمٌ
Mwenyezi Mungu ni Nuru ya Mbingu na Ardhi. Mfano wa Nuru yake ni kama shubaka lenye kuwekwa ndani yake taa. Taa ile imo katika tungi. Tungi lile ni kama nyota inayomeremeta, inayowashwa kwa mafuta yanayotoka katika mti uliobarikiwa, mzaituni. Si wa mashariki wala magharibi. Yanakaribia mafuta yake kung'aa wenyewe ingawa moto haujayagusa, - Nuru juu ya Nuru. Mwenyezi Mungu humwongoa kwenye Nuru yake amtakaye. Na Mwenyezi Mungu huwapigia watu mifano. Na Mwenyezi Mungu ni Mwenye kujua kila kitu.
Maana: Swahili Translation - Rowad Translation Center. Issued by the Islamic Content Service Association in Languages Toleo 1.0.5, 2025-12-17. QuranEnc.com
Mwenyezi Mungu ni Nuru ya Mbingu na Ardhi. Mfano wa Nuru yake ni kama shubaka lenye kuwekwa ndani yake taa. Taa ile imo katika tungi. Tungi lile ni kama nyota inayo meremeta, inayo washwa kwa mafuta yanayo toka katika mti ulio barikiwa, mzaituni. Si wa mashariki wala magharibi. Yanakaribia mafuta yake kung'aa wenyewe ingawa moto haujayagusa - Nuru juu ya Nuru. Mwenyezi Mungu humwongoa kwenye Nuru yake amtakaye. Na Mwenyezi Mungu huwapigia watu mifano. Na Mwenyezi Mungu ni Mwenye kujua kila kitu. [35]
[35] Mwenyezi Mungu ndiye chanzo cha Nuru ya katika mbingu na ardhi. Yeye ndiye Mwenye kunawirisha vyote hivyo kwa nuru yote tunayo iona na tukenda ndani yake, na ya maana, kama Nuru ya Haki na uadilifu, na ilimu, na fadhila, na uwongofu, na Imani, na kwa ushahidi na athari kama alivyo waahidi viumbe vyake, na kwa vyote vinavyo onyesha kuwepo kwa Mwenyezi Mungu, na vikalingania Imani kumuamini Yeye Subhanahu. Na mfano wa Nuru yake Tukufu na dalili zake zilizo zagaa kwa uwazi ni kama mfano wa Nuru ya taa yenye kung'aa kwa ukali kabisa, iliyo wekwa kwenye shubaka la ukutani ili kuukusanya mwangaza wake na kuzidi kuupa nguvu. Na taa hiyo imevikwa tungi la kigae safi linameremeta kama inavyo meremeta nyota. Na taa ile inawaka kwa mafuta ya mti wenye baraka nyingi, ulio pandwa kwenye udongo mzuri na pahali pazuri. Mti huu ni mzaituni unao mea pahala pa kati na kati. Basi huo si wa mashariki ukakosa joto la jua wakati wa alasiri, wala si wa magharibi ukakosa joto la jua wakati wa asubuhi. Bali huo uko juu ya kilele cha mlima, au katika uwazi wa ardhi unao patisha jua mchana kutwa. Mafuta ya mti huu yanakaribia kutoa mwanga kwa ubora wa usafi wake hata ikiwa hayajaguswa na moto wa taa. Mambo haya yote yanazidisha mwangaza wa hiyo taa juu ya mwangaza wake, na Nuru juu ya Nuru. Na namna hii ndio zinakuwa dalili zilizo enea katika ulimwengu, za kuonekana na kupimika kwa akili; ni Ishara zilizo wazi hazitaki kutiliwa shaka yoyote kwa kuwepo Mwenyezi Mungu, na kuwajibikia Imani kumuamini Yeye, na Risala za Mitume aliyo waleta. Na Mwenyezi Mungu humwezesha kufikia Imani amtakaye kwa njia ya dalili hizi ikiwa huyo mtu atajaribu kunafiika na nuru ya akili yake. Na Mwenyezi Mungu ameleta mifano ya kuweza kuhisiwa na kuonekana ili iwe wepesi kuelewa mambo ya kiakili. Na Yeye Subhanahu ni Mkunjufu wa ujuzi, anawajua wenye kuangalia Ishara zake na wenye kuzipuuza na wakapanda kiburi. Naye atawalipa kwa hayo.
Maana: Swahili Translation - Ali Mohsin Al-Barwani. Translated by Ali Mohsen Al-Barwani Toleo 1.0.1, 2025-06-25. QuranEnc.com
Allah Mtukufu ni Nuru ya mbinguni na ardhini, Anaendesha mambo humo na Anawaongoza watu wake. Kwa hivyo, Yeye, kutakasika na sifa za upungufu ni Kwake, ni Nuru, na pazia Yake ni Nuru. Kwayo zimeng’ara mbingu na ardhi na vilivyomo ndani. Na kitabu cha Allah Mtukufu na uongofu wake ni nuru kutoka Kwake, kutakasika na sifa za upungufu ni Kwake. Na lau si nuru Yake yeye Aliyetukuka, lingeshikamana giza na kupandana, hili juu ya lingine. Mfano wa nuru Yake ambayo inaongoza kupeleka Kwake, nayo ni Imani na Qura’ni ndani ya moyo wa mwenye kuamini, ni kama kishubaki, nacho ni kidirisha ukutani kisichoonyesha upande wa pili, kwenye kidirisha kuna taa, ambapo hapo kidirisha kinakusanya nuru ya ile taa, zote zikawa mwangaza wake ni mmoja. Na taa hiyo iko kwenye kioo, kana kwamba kioo hicho kwa usafi wake ni nyota ing’arayo kama duri. Taa hiyo inawashwa kwa mafuta ya mti uliobarikiwa, nao ni mzaituni, si wa upande wa mashariki tu usiopatwa na jua mwisho wa mchana, wala si wa magharibi tu usiopatwa na jua mwanzo wa mchana, isipokuwa uko katikati kwenye sehemu ya ardhi, haukuelekea Mashariki wala Magharibi. Yanakaribia mafuta yake kwa usafi wake kuwaka yenyewe bila ya kuguswa na moto, na pindi yakiguswa na moto hung’ara mn’garo mkali mno, nuru juu ya nuru. Hiyo ni nuru kutokana na mwangaza utokao kwenye mafuta, ulioko juu ya nuru itokanayo na kuwasha moto. Basi huo ndio mfano wa uongofu, huwa unang’ara ndani ya moyo wa mwenye Imani. Na Allah Mtukufu Anamuongoza na kumuelekeza kuifuata Qur’ani Amtakaye, na Anawapigia watu mifano ili wapate kuifahamu mifano yake na hekima zake. Na Allah Mtukufu kwa kila kitu ni Mjuzi mno na hakuna chochote kinachofichamana Kwake.
Maana: Swahili Translation - Abdullah Muhammad and Nasser Khamis. Translated by Dr. Abdullah Muhammad Abu Bakr & Shaykh Nasser Khamis Toleo 1.0.1, 2026-03-12. QuranEnc.com
Kiarabu ni maandishi ya Tanzil, bila kubadilishwa. Maana ni matoleo ya wachapishaji wake, bila kubadilishwa; wahakiki wa Sabīl wenyewe bado hawajazikagua. Kiarabu: maandishi ya Uthmani ya Tanzil, toleo la 1.1. Chanzo: tanzil.net