Al-Muminoon 23:27
المؤمنونفَأَوْحَيْنَآ إِلَيْهِ أَنِ ٱصْنَعِ ٱلْفُلْكَ بِأَعْيُنِنَا وَوَحْيِنَا فَإِذَا جَآءَ أَمْرُنَا وَفَارَ ٱلتَّنُّورُ ۙ فَٱسْلُكْ فِيهَا مِن كُلٍّ زَوْجَيْنِ ٱثْنَيْنِ وَأَهْلَكَ إِلَّا مَن سَبَقَ عَلَيْهِ ٱلْقَوْلُ مِنْهُمْ ۖ وَلَا تُخَـٰطِبْنِى فِى ٱلَّذِينَ ظَلَمُوٓا۟ ۖ إِنَّهُم مُّغْرَقُونَ
Tukamfunulia wahyi kwamba, "Unda jahazi mbele ya macho yetu na ufunuo wetu! Na itakapofika amri yetu na ikafurika tanuri, hapo waingize ndani yake kutoka kwa kila jozi, dume na jike, na ahali zako, isipokuwa yule ambaye katika wao juu yake imekwisha tangulia kauli. Wala usiniongeleshe kuhusu hao waliodhulumu. Kwani hao bila ya shaka watazamishwa.
Maana: Swahili Translation - Rowad Translation Center. Issued by the Islamic Content Service Association in Languages Toleo 1.0.5, 2025-12-17. QuranEnc.com
Tukampa wahyi: Unda jahazi mbele ya macho yetu na uwongozi wetu! Basi itapo fika amri yetu na ikafurika tanuri, hapo waingize ndani yake wa kila namna dume na jike, na ahali zako, isipo kuwa yule ambaye katika wao juu yake imekwisha tangulia kauli. Wala usinitajie hao walio dhulumu. Kwani hao bila ya shaka watazamishwa. [27]
[27] Tukamwambia kwa njia ya ufunuo (wahyi): Unda jahazi, nawe utalindwa na uangalizi wetu. Shari yao haitokupata, nasi tutakuongoza katika kazi yako. Na ikifikilia miadi ya kuwaadhibu, na ukaona tanuri inafoka maji kwa amri yetu, basi waingize katika jahazi katika kila namna ya viumbe vilivyo hai dume na jike. Na waingize ahali zako, isipo kuwa walio kwisha thibitika adhabu yao kwa kukosa kwao Imani. Wala usiniombe kuwaokoa wale walio dhulumu nafsi zao na wakawadhulumu na wengineo kwa ukafiri na uasi. Kwani Mimi nimewahukumia kuwazamisha kwa sababu ya dhulma yao ya ushirikina na uasi. "Tukampa wahyi: Unda jahazi mbele ya macho yetu na uwongozi wetu! Basi itapo fika amri yetu na ikafurika tanuri, hapo waingize ndani yake wa kila namna dume na jike, na ahali zako, isipo kuwa yule ambaye katika wao juu yake imekwisha tangulia kauli. Wala usinitajie hao walio dhulumu. Kwani hao bila ya shaka watazamishwa." Hakika haya maelezo ya Tofani lilio tokea ijapo kuwa ni kwa mukhtasari tu katika hizi Aya tukufu, kwa mwenye akili ya kuzingatia yana maana na mambo ya hakika mengi ya ki-ilimu ambayo yanawapitia watu wengi. Na "tanuri" kwa lugha ni jiko la kuchomea mikate, au pia ni uso wa ardhi na kila chenye kutimbuka maji, na kila penye mkusanyiko wa maji. Na si wepesi kusema kwa yakini taarikhi ya hiyo Tofani, kwani zilitokea tofani nyingi zama za kale, kama katika Babilonia, Bara Hindi na Amerika. Na zipo baadhi ya hadithi za kienyeji mbali mbali zinazo taja khabari ya Tofani. Lakini haielekei kuwa hadithi hizo ndio zimekhusu hii Tofani kubwa au Tofani ya Nuhu. Uchunguzi umethibitisha na pia zimeonekana tofani nyingi ulimwenguni. Na tofani ya mwisho ya ulimwengu mzima ilikuwa sababu yake ni kumalizika kipindi cha barafu cha mwisho, na kuyayuka barafu nyingi ya kaskazini kabisa na kusini kabisa kwa dunia. Na sisi hatujui kwa yakini lini mizani iligeuka na tanuri ikafurika - yaani uso wa ardhi - kwa kupanda kwa ghafla kwa hivyo kuyayuka barafu, hata yakapanda juu maji ya bahari na ya kamwagika maji. Yafaa kutaja kuwa kuyayuka barafu ya zama za barafu za mwisho kulileta hali ya hewa yenye mvua nyingi sana katika sehemu za dunia zilio mbali na huko kaskazini na kusini kabisa kwa ulimwengu, kama vile katika Bahari ya Kati (Mediterenian). Vyo vyote vile ilivyo inakubalika kuwa hatuna ushahidi wa kuweza kusema lini khasa zilikuwa hizo zama za Nuhu na kaumu yake. Yaliyo dhaahiri kuwa yote hayo ni muujiza wa Mwenyezi Mungu. Na katika miujiza ni kuwa Nuhu aliwanasihi watu wake na akawaonya na ghadhabu ya Mwenyezi Mungu. Na Mwenyezi Mungu akafunua kuwa atawazamisha ikiwa hawakutengenea. Na tena akamfunulia aunde marikebu. Kisha ikaja amri ya Mwenyezi Mungu, na mizani ikapinduka, na tanuri ikafurika, ikamiminika mvua kuthibitisha aliyo yasema Mwenyezi Mungu kumwambia Nuhu ya kwamba Mwenyezi Mungu anajua kuwa hatoamini mtu katika kaumu yake baada ya wale walio kwisha amini.
Maana: Swahili Translation - Ali Mohsin Al-Barwani. Translated by Ali Mohsen Al-Barwani Toleo 1.0.1, 2025-06-25. QuranEnc.com
Hapo tukamletea wahyi na kumwambia, Tengeneza jahazi chini ya uangalizi wetu na amri yetu kwako na usaidizi wetu, na wewe uko kwenye utunzi wetu na hifadhi yetu. Basi amri yetu itakapokuja ya kuwaadhibu watu wako kwa kuwazamisha, na mafuriko yakaanza, na maji yakatoka kwa nguvu kutoka kwenye tanuri, napo ni mahali pa kuchomea mikate, ikiwa ni alama ya kuja kwa adhabu, hapo basi watie ndani ya jahazi, kati ya kila kilicho hai, kiume na kike, ili kizazi kisalie. Na uwatie watu wako pia, isipokuwa yule aliyestahili kuadhibiwa kwa ukafiri wake, kama mke wako na mwanao wa kiume, na usiniombe kuokolewa watu wako waliodhulumu, kwani wao hapana budi ni wenye kuzamishwa. Na katika aya hii pana kuthibitisha sifa ya jicho kwa Allah Mtukufu, kutakasika na sifa za upungufu ni Kwake, kama inavyonasibiana na Yeye, Aliyetukuka, bila kufananisha wala kufikiria kuwa liko namna gani.
Maana: Swahili Translation - Abdullah Muhammad and Nasser Khamis. Translated by Dr. Abdullah Muhammad Abu Bakr & Shaykh Nasser Khamis Toleo 1.0.1, 2026-03-12. QuranEnc.com
Kiarabu ni maandishi ya Tanzil, bila kubadilishwa. Maana ni matoleo ya wachapishaji wake, bila kubadilishwa; wahakiki wa Sabīl wenyewe bado hawajazikagua. Kiarabu: maandishi ya Uthmani ya Tanzil, toleo la 1.1. Chanzo: tanzil.net