Al-Baqara 2:61
البقرةوَإِذْ قُلْتُمْ يَـٰمُوسَىٰ لَن نَّصْبِرَ عَلَىٰ طَعَامٍ وَٰحِدٍ فَٱدْعُ لَنَا رَبَّكَ يُخْرِجْ لَنَا مِمَّا تُنۢبِتُ ٱلْأَرْضُ مِنۢ بَقْلِهَا وَقِثَّآئِهَا وَفُومِهَا وَعَدَسِهَا وَبَصَلِهَا ۖ قَالَ أَتَسْتَبْدِلُونَ ٱلَّذِى هُوَ أَدْنَىٰ بِٱلَّذِى هُوَ خَيْرٌ ۚ ٱهْبِطُوا۟ مِصْرًا فَإِنَّ لَكُم مَّا سَأَلْتُمْ ۗ وَضُرِبَتْ عَلَيْهِمُ ٱلذِّلَّةُ وَٱلْمَسْكَنَةُ وَبَآءُو بِغَضَبٍ مِّنَ ٱللَّهِ ۗ ذَٰلِكَ بِأَنَّهُمْ كَانُوا۟ يَكْفُرُونَ بِـَٔايَـٰتِ ٱللَّهِ وَيَقْتُلُونَ ٱلنَّبِيِّـۧنَ بِغَيْرِ ٱلْحَقِّ ۗ ذَٰلِكَ بِمَا عَصَوا۟ وَّكَانُوا۟ يَعْتَدُونَ
Na mliposema: 'Ewe Musa! Hatuwezi kuvumilia chakula cha namna moja tu. Basi tuombee kwa Mola wako Mlezi atutolee vile vinavyomea katika Ardhi, kama mboga zake, na matango yake, na vitunguu saumu vyake, na adesi zake, na vitunguu maji vyake.' Akasema: "Mnabadili kilicho duni kwa kilicho bora? Shukeni mjini, huko mtapata mlivyoviomba." Na wakapigwa na unyonge, na umasikini, na wakastahili ghadhabu ya Mwenyezi Mungu. Na haya ni kwa sababu walikuwa wakiyakufuru maneno ya Mwenyezi Mungu, na wakiwauwa Manabii pasipo haki. Hayo ni kwa walivyoasi na wakapindukia mipaka.
Maana: Swahili Translation - Rowad Translation Center. Issued by the Islamic Content Service Association in Languages Toleo 1.0.5, 2025-12-17. QuranEnc.com
Na mlipo sema: Ewe Musa! Hatuwezi kuvumilia chakula cha namna moja tu, basi tuombee kwa Mola wako Mlezi atutolee vile vinavyo mea katika Ardhi, kama mboga zake, na matango yake, na thom zake, na adesi zake, na vitunguu vyake. Akasema: Mnabadili kilicho duni kwa kilicho bora? Shukeni mjini, huko mtapata mlivyo viomba. Na wakapigwa na unyonge,na umasikini, na wakastahili ghadhabu ya Mwenyezi Mungu. Na haya ni kwa sababu walikuwa wakiyakataa maneno ya Mwenyezi Mungu, na wakiwauwa Manabii pasipo haki. Hayo ni kwa walivyo asi na wakapindukia mipaka. [61]
[61] Na kumbukeni pia, enyi Mayahudi, pale wale wazee wenu walio tangulia walipo zidi jeuri zao, wasiipe neema ya Mwenyezi Mungu haki yake, wakamwambia Musa: Sisi hatutovumilia chakula hicho kwa hicho (nacho ni Manna na Salwa). Basi muombe Mola wako atutolee katika ardhi mboga, na matango, na adasi, na thom na vitunguu. Musa aliyastaajabia haya na wala hakupendezewa nayo. Akawaambia: Hivyo nyinyi mnafadhilisha vyakula namna hii kuliko vilivyo kuwa bora zaidi na vizuri zaidi, navyo ni Manna na Salwa? Basi shukeni kutoka Sinai, na ingieni katika mji mmojawapo na huko mtapata hivyo mnavyo vitaka. Na kwa sababu ya kutoridhika kwao huko na inda yao hao Mayahudi walipigwa na madhila, na ufakiri na unyonge, wakastahiki kupata ghadhabu ya Mwenyezi kwa ule mtindo wao wa inda na uasi, kukanusha ishara za Mwenyezi Mungu, na kuwauwa Manabii. Kwa haya ikawa wanaacha Haki iliyo kwisha thibiti na kukubalika. Yaliyo wapelekea hata wakaingia katika ukafiri ule na mauwaji yale ni kule kuziachia nafsi zao kupanda maasi na kufanya uadui na kupindukia mipaka katika maasia.
Maana: Swahili Translation - Ali Mohsin Al-Barwani. Translated by Ali Mohsen Al-Barwani Toleo 1.0.1, 2025-06-25. QuranEnc.com
Na kumbukeni, tulipowateremshia chakula tamu na ndege wa kuvutia, mkawa hamjali, kama ilivyo desturi yenu, ikawapata dhiki na machovu na mkasema, “Ewe Mûsã! Sisi hatutavumilia chakula hicho kwa hicho kisichobadilika siku zote. Basi tuombee Mola wako Atutolee chakula katika mimea ya ardhini kama mboga, matango, mbegu zinazoliwa, adasi na vitunguu.” Mûsã akawaambia, kwa kuwapinga vikali, “Vipi mnataka hivyi ambavyo ni duni zaidi na mnaacha riziki yenye manufaa ambayo Allah Mtukufu amewachagulia? Ondokeni jangwani na mshuke mjini. Huko mtavipata mnavyovitamani sana kwenye mashamba na masoko.” Waliposhuka, iliwabainikia kuwa wao wanatanguliza chaguo lao,kila mahali, juu ya chaguo la Allah Mtukufu na wanayafadhilisha matamanio yao juu ya vitu ambavyo Allah Mtukufu Aliwachagulia. Kwa hivyo, sifa ya unyonge na umasikini wa moyo iliwaambata, na wakaondoka na kurudi wakiwa wamo kwenye ghadhabu kutoka kwa Allah Mtukufu, kwa kuipa mgongo dini ya Allah Mtukufu, na kwa kuwa wao walikuwa wakikanusha aya za Allah Mtukufu na kuua Manabii kwa udhalimu na uadui. Yote hayo ni kwa sababu ya kuasi kwao na kuivuka mipaka ya Mola wao.
Maana: Swahili Translation - Abdullah Muhammad and Nasser Khamis. Translated by Dr. Abdullah Muhammad Abu Bakr & Shaykh Nasser Khamis Toleo 1.0.1, 2026-03-12. QuranEnc.com
Kiarabu ni maandishi ya Tanzil, bila kubadilishwa. Maana ni matoleo ya wachapishaji wake, bila kubadilishwa; wahakiki wa Sabīl wenyewe bado hawajazikagua. Kiarabu: maandishi ya Uthmani ya Tanzil, toleo la 1.1. Chanzo: tanzil.net