Al-Baqara 2:266
البقرةأَيَوَدُّ أَحَدُكُمْ أَن تَكُونَ لَهُۥ جَنَّةٌ مِّن نَّخِيلٍ وَأَعْنَابٍ تَجْرِى مِن تَحْتِهَا ٱلْأَنْهَـٰرُ لَهُۥ فِيهَا مِن كُلِّ ٱلثَّمَرَٰتِ وَأَصَابَهُ ٱلْكِبَرُ وَلَهُۥ ذُرِّيَّةٌ ضُعَفَآءُ فَأَصَابَهَآ إِعْصَارٌ فِيهِ نَارٌ فَٱحْتَرَقَتْ ۗ كَذَٰلِكَ يُبَيِّنُ ٱللَّهُ لَكُمُ ٱلْـَٔايَـٰتِ لَعَلَّكُمْ تَتَفَكَّرُونَ
Je, angependa mmoja wenu kwamba awe na bustani ya mitende na mizabibu ipitayo mito chini yake. Naye humo hupata katika mazao ya kila namna, na uzee ukamfikia ilhali ana watoto wanyonge. Kisha ikapigwa na kimbunga chenye moto, kwa hivyo ikaungua? Hivi ndivyo Mwenyezi Mungu anavyowabainishia ishara ili mtafakari.
Maana: Swahili Translation - Rowad Translation Center. Issued by the Islamic Content Service Association in Languages Toleo 1.0.5, 2025-12-17. QuranEnc.com
Je! Yupo mmoja wenu anaye penda kuwa na kitalu cha mitende na mizabibu ipitayo mito kati yake, naye humo hupata mazao ya kila namna, na uzee ukamfikia naye hali ana watoto wanyonge, kikapigwa na kimbunga chenye moto, kikaungua? Hivi ndivyo Mwenyezi Mungu anavyo kubainishieni Ishara ili mpate kufikiri. [266]
[266] Hapana yeyote katika nyinyi anaye penda kuwa na kitalu cha mitende na mizabibu na mito inapita kati yake na kimezaa kila namna ya matunda ayatakayo, naye hali amekwisha kuwa mkongwe na akawa na watoto wadogo wanyonge hawawezi kazi wala yeye hajiwezi kwa ukongwe wake, kikaja kitalu chake kikakauka kwa upepo mkali wenye moto, na miti ikaungua, wakati ambao yeye mwenyewe na watoto ndio wamo katika shida ya kuhitaji. Basi hali kadhaalika shani ya mwenye kutoa sadaka na akafuatishia masimbulizi na maudhi na riya, kujionyesha kwa watu, ambayo hayo yakapoteza thawabu zote za sadaka zake, na wala hawezi tena kutoa sadaka kwa kujitengezea nafsi yake. Kwa bayana kama hizi ndio Mwenyezi Mungu anakuonyesheni Ishara ili mpate kutafakari na kujifunza. Ilimu ya kisasa inaeleza kuwa katika anga pepo kali hugongana zikatoka radi na umeme na mvua. Huenda ukatokea moto kwa umeme kwa kugongana mawingu, au pengine huweza kutokea vimondo kutokana na volkano (burkani) iliyo karibu ikateketeza miti na chochote kilicho katika sehemu hizo. Qur'ani inaashiria maana zote hizo.
Maana: Swahili Translation - Ali Mohsin Al-Barwani. Translated by Ali Mohsen Al-Barwani Toleo 1.0.1, 2025-06-25. QuranEnc.com
Je anapendelea mmoja wenu awe na bustani yenye mitende na mizabibu, ambayo inapita chini ya miti yake maji tamu, na ndani yake ana kila aina ya matunda, na amefikia hali ya ukongwe ya kutoweza kupanda mimea kama hii, na ana watoto wadogo wanaohitaji bustani hii, na katika hali hii ukavuma upepo mkali uchomao, ukaja ukaiteketeza? Hivi ndivyo hali ya wasio na ikhlasi katika utoaji wao; watakuja Siku ya Kiyama hawana jema lolote lao. Kwa ufafanuzi huu, Allah Mtukufu Anawabainishia mambo yanayowafaa nyinyi, ili mtaamali na kumtakasia Allah Mtukufu utoaji wenu.
Maana: Swahili Translation - Abdullah Muhammad and Nasser Khamis. Translated by Dr. Abdullah Muhammad Abu Bakr & Shaykh Nasser Khamis Toleo 1.0.1, 2026-03-12. QuranEnc.com
Kiarabu ni maandishi ya Tanzil, bila kubadilishwa. Maana ni matoleo ya wachapishaji wake, bila kubadilishwa; wahakiki wa Sabīl wenyewe bado hawajazikagua. Kiarabu: maandishi ya Uthmani ya Tanzil, toleo la 1.1. Chanzo: tanzil.net