Ruka hadi kwenye maudhui
Sura ya 2 · Aya ya 26

Al-Baqara 2:26

البقرة

إِنَّ ٱللَّهَ لَا يَسْتَحْىِۦٓ أَن يَضْرِبَ مَثَلًا مَّا بَعُوضَةً فَمَا فَوْقَهَا ۚ فَأَمَّا ٱلَّذِينَ ءَامَنُوا۟ فَيَعْلَمُونَ أَنَّهُ ٱلْحَقُّ مِن رَّبِّهِمْ ۖ وَأَمَّا ٱلَّذِينَ كَفَرُوا۟ فَيَقُولُونَ مَاذَآ أَرَادَ ٱللَّهُ بِهَـٰذَا مَثَلًا ۘ يُضِلُّ بِهِۦ كَثِيرًا وَيَهْدِى بِهِۦ كَثِيرًا ۚ وَمَا يُضِلُّ بِهِۦٓ إِلَّا ٱلْفَـٰسِقِينَ

Maana

Hakika Mwenyezi Mungu haoni haya kutoa mfano hata wa mbu na ulio wa zaidi yake. Ama wale walioamini hujua ya kwamba hiyo ni haki iliyotoka kwa Mola wao Mlezi. Lakini wale waliokufuru, husema: 'Ni nini analokusudia Mwenyezi Mungu kwa mfano huu?' Kwa mfano huu huwapoteza wengi na huwaongoa wengi; lakini hawapotezi kwa huo ila wale wavukao mipaka.

Maana: Swahili Translation - Rowad Translation Center. Issued by the Islamic Content Service Association in Languages Toleo 1.0.5, 2025-12-17. QuranEnc.com

Maana

Hakika Mwenyezi Mungu haoni haya kutoa mfano hata wa mbu na ulio wa zaidi yake. Ama wale walio amini hujua ya kwamba hiyo ni haki iliyo toka kwa Mola wao Mlezi, lakini wale walio kufuru husema: Ni nini analo kusudia Mwenyezi Mungu kwa mfano huu? Kwa mfano huu huwapoteza wengi na huwaongoa wengi; lakini hawapotezi ila wale wapotovu, [26]

[26] Mwenyezi Mungu huwaletea mifano watu kueleza hakika ya mambo yalivyo juu, kwa kufananisha na vidudu vidogo na pia vitu vikubwa. Wasio amini waliikejeli hiyo mifano ya vijidudu vidogo kama nzi na buibui. Basi Mwenyezi Mungu aliye takasika haoni aibu kama wanavyo aibika watu kwa kuona haya. Hana la kumzuia asiwape waja wake mfano wowote autakao hata ukiwa mdogo vipi. Kwa hivyo ni sawa kabisa kupiga mfano wa mbu na kilio zaidi kuliko hivyo. Na walio amini wanajua kuwa hii ni mifano, na kuwa huu ni ukweli utokao kwa Mwenyezi Mungu. Ama walio kufuru hawapendi hayo, na husema: "Mwenyezi Mungu anataka nini kwa mfano huu?" Na mfano kama huu huwa ni sababu ya kupotea wale wasio tafuta haki wala hawaitaki, na huwa ni sababu ya kuwaongoa wenye kuamini na kuitaka haki. Basi hawapotei ila waasi walio kwisha potea.

Maana: Swahili Translation - Ali Mohsin Al-Barwani. Translated by Ali Mohsen Al-Barwani Toleo 1.0.1, 2025-06-25. QuranEnc.com

Maana

Allah Mtukufu Halionei haya jambo la haki lolote kulitaja, liwe ni kubwa au dogo, hata kama ni kukipigia mfano kitu kidogo sana, kama mbu na nzi na mfano wake, katika vitu Alivyovipigia mfano Allah Mtukufu kuonyesha kushindwa kwa kila kitu kinachoabudiwa kisichokuwa Allah Mtukufu. Ama waumini, wao wanajua hekima ya Allah Mtukufu katika kupigia mfano kitu kikubwa au kidogo miongoni mwa viumbe Vyake. Ama makafiri, wanafanya maskhara na kusema, “Ni nini lengo la Allah Mtukufu kupigia mfano vidudu hivi vitwevu?” Allah Mtukufu anawajibu kwamba makusudio ni kuwafanyia mtihani na kupambanua Mwenye Imani na kafiri. Kwa hivyo, Allah Mtukufu, kwa mifano hii, anawaepusha na haki watu wengi, kwa kuifanyia kwao maskhara, na Anawapa taufiki kwayo wengineo kupata nyongeza ya Imani na uongofu. Na Allah Mtukufu Hamdhulumu yeyote, kwani Hawaepushi na haki isipokuwa wenye kutoka nje ya utiifu Kwake.

Maana: Swahili Translation - Abdullah Muhammad and Nasser Khamis. Translated by Dr. Abdullah Muhammad Abu Bakr & Shaykh Nasser Khamis Toleo 1.0.1, 2026-03-12. QuranEnc.com

Al-Baqara

Kiarabu ni maandishi ya Tanzil, bila kubadilishwa. Maana ni matoleo ya wachapishaji wake, bila kubadilishwa; wahakiki wa Sabīl wenyewe bado hawajazikagua. Kiarabu: maandishi ya Uthmani ya Tanzil, toleo la 1.1. Chanzo: tanzil.net