Ruka hadi kwenye maudhui
Sura ya 2 · Aya ya 25

Al-Baqara 2:25

البقرة

وَبَشِّرِ ٱلَّذِينَ ءَامَنُوا۟ وَعَمِلُوا۟ ٱلصَّـٰلِحَـٰتِ أَنَّ لَهُمْ جَنَّـٰتٍ تَجْرِى مِن تَحْتِهَا ٱلْأَنْهَـٰرُ ۖ كُلَّمَا رُزِقُوا۟ مِنْهَا مِن ثَمَرَةٍ رِّزْقًا ۙ قَالُوا۟ هَـٰذَا ٱلَّذِى رُزِقْنَا مِن قَبْلُ ۖ وَأُتُوا۟ بِهِۦ مُتَشَـٰبِهًا ۖ وَلَهُمْ فِيهَآ أَزْوَٰجٌ مُّطَهَّرَةٌ ۖ وَهُمْ فِيهَا خَـٰلِدُونَ

Maana

Na wabashirie walioamini na wakatenda mema kwamba watapata mabustani yapitayo mito chini yake; kila watakapopewa matunda humo, watasema: 'Haya ndiyo kama tuliyopewa mbele.' Na wataletewa matunda yaliyofanana; na humo watakuwa na wake waliotakaswa; na wao humo watadumu.

Maana: Swahili Translation - Rowad Translation Center. Issued by the Islamic Content Service Association in Languages Toleo 1.0.5, 2025-12-17. QuranEnc.com

Maana

Na wabashirie walio amini na wakatenda mema kwamba watapata mabustani yapitayo mito kati yake; kila watapo pewa matunda humo, watasema: Haya ndiyo kama tuliyo pewa mbele. Na wataletewa matunda yaliyo fanana; na humo watakuwa na wake walio takasika; na wao humo watadumu. [25]

[25] Ikiwa hizi ni adhabu za waovu wapinzani, basi Pepo ndio makao ya Waumini. Waambie wenye kumuamini Mwenyezi Mungu na Mtume wake na Kitabu chake, na wakaikubali haki bila ya kutia shaka au wasiwasi, na wakatenda vitendo vyema - waambie khabari ya kuwafurahisha na kukunjua vifua vyao; nayo ni kuwa Mwenyezi Mungu amewaandalia mabustani yenye mazao, yapitayo mito chini ya miti yake na majumba yake. Kila Mwenyezi Mungu akiwaruzuku matunda ya hizo bustani wao husema: "Haya yamefanana na yale tuliyo pewa kabla." Kwani matunda haya yanashabihiana kwa sura, lakini yanakhitalifiana kwa utamu na ladha. Na watakuwa nao humo pia wake walio kamilika walio safi, wasio kuwa na ila yoyote. Na katika Pepo hii wataishi maisha ya milele wala hawatotoka humo.

Maana: Swahili Translation - Ali Mohsin Al-Barwani. Translated by Ali Mohsen Al-Barwani Toleo 1.0.1, 2025-06-25. QuranEnc.com

Maana

Waambie, ewe Mtume, watu wa Imani na amali nzuri, habari yenye kuwajaza furaha, kuwa wao huko Akhera watakuwa na Mabustani ya ajabu, ambayo inapita mito chini ya majumba yake makubwa na miti yake yenye vivuli. Kila Anapowaruzuku Allah Mtukufu humo aina yoyote ya matunda yenye ladha, watasema, “Allah Mtukufu Alituruzuku aina hii ya matunda kipindi cha nyuma.” Watakapoionja wataikuta ni tafauti tamu yake na ladha yake, ingawa inafanana na aina iliyopita kwa rangi, sura na jina. Na katika hayo Mabustani ya Peponi watakuwa na wake waliosafishika na kila aina ya uchafu, wa nje, kama mkojo na damu ya hedhi, na wandani, kama kusema urongo na kuwa na tabia mbaya. Na wao, katika Pepo na starehe zake, watakaa milele, hawafi humo wala hawatoki.

Maana: Swahili Translation - Abdullah Muhammad and Nasser Khamis. Translated by Dr. Abdullah Muhammad Abu Bakr & Shaykh Nasser Khamis Toleo 1.0.1, 2026-03-12. QuranEnc.com

Al-Baqara

Kiarabu ni maandishi ya Tanzil, bila kubadilishwa. Maana ni matoleo ya wachapishaji wake, bila kubadilishwa; wahakiki wa Sabīl wenyewe bado hawajazikagua. Kiarabu: maandishi ya Uthmani ya Tanzil, toleo la 1.1. Chanzo: tanzil.net