Ruka hadi kwenye maudhui
Sura ya 2 · Aya ya 259

Al-Baqara 2:259

البقرة

أَوْ كَٱلَّذِى مَرَّ عَلَىٰ قَرْيَةٍ وَهِىَ خَاوِيَةٌ عَلَىٰ عُرُوشِهَا قَالَ أَنَّىٰ يُحْىِۦ هَـٰذِهِ ٱللَّهُ بَعْدَ مَوْتِهَا ۖ فَأَمَاتَهُ ٱللَّهُ مِا۟ئَةَ عَامٍ ثُمَّ بَعَثَهُۥ ۖ قَالَ كَمْ لَبِثْتَ ۖ قَالَ لَبِثْتُ يَوْمًا أَوْ بَعْضَ يَوْمٍ ۖ قَالَ بَل لَّبِثْتَ مِا۟ئَةَ عَامٍ فَٱنظُرْ إِلَىٰ طَعَامِكَ وَشَرَابِكَ لَمْ يَتَسَنَّهْ ۖ وَٱنظُرْ إِلَىٰ حِمَارِكَ وَلِنَجْعَلَكَ ءَايَةً لِّلنَّاسِ ۖ وَٱنظُرْ إِلَى ٱلْعِظَامِ كَيْفَ نُنشِزُهَا ثُمَّ نَكْسُوهَا لَحْمًا ۚ فَلَمَّا تَبَيَّنَ لَهُۥ قَالَ أَعْلَمُ أَنَّ ٱللَّهَ عَلَىٰ كُلِّ شَىْءٍ قَدِيرٌ

Maana

Au kama yule aliyepita karibu na mji hali ya kuwa umekwishakuwa magofu tu. Akasema: Vipi Mwenyezi Mungu ataufufua mji huu baada ya kufa kwake? Basi Mwenyezi Mungu akamfisha yeye (muda wa) miaka mia moja, kisha akamfufua. Akasema: Je umekaa muda gani? Akasema: (Labda) nimekaa siku moja au sehemu ya siku. Akasema: Bali umekaa miaka mia moja. Hebu angalia chakula chako na vinywaji vyako, havikuharibika. Na mwangalie punda wako. Na ili tukufanye uwe ni ishara kwa watu. Na iangalie mifupa yake hii jinsi tunavyoinyanyua kisha tuivishe nyama. Basi yalipombainikia, alisema: Ninajua kwamba kwa hakika Mwenyezi Mungu ni Mwenye uwezo mno juu ya kila kitu.

Maana: Swahili Translation - Rowad Translation Center. Issued by the Islamic Content Service Association in Languages Toleo 1.0.5, 2025-12-17. QuranEnc.com

Maana

Au kama yule aliye pita karibu na mji ulio kwisha kuwa magofu tu, akasema: Ataufufuaje Mwenyezi Mungu mji huu baada ya kufa kwake? Basi Mwenyezi Mungu alimfisha yeye muda wa miaka mia. Kisha akamfufua. Akamuuliza: Je umekaa muda gani? Akajibu: Labda nimekaa siku moja au sehemu ya siku. Akamwambia: Bali umekaa miaka mia wewe. Hebu angalia chakula chako na vinywaji vyako, havikuharibika. Na muangalie punda wako. Na ili tukufanye uwe ni Ishara kwa watu iangalie hii mifupa yake jinsi tunavyo inyanyua kisha tunaivisha nyama. Basi yalipo mbainikia alinena: Najua kwamba Mwenyezi Mungu ni Mwenye uweza juu ya kila kitu. [259]

[259] Kisha zingatia kisa hichi cha ajabu, cha mtu aliye pita kwenye mji uliyo kwisha teketea, sakafu za majumba yake zimeporomoka na zimebomoa viwambaza vyake, na watu wake wameangamia. Akasema huyo mtu: Vipi Mwenyezi Mungu atawahuisha tena watu wa mji huu baada ya kuwa wamekwisha kufa? Mwenyezi Mungu akamfisha yeye na akamweka, naye ni maiti, muda wa miaka mia. Kisha akamfufua, ili amwonyeshe wepesi wa ufufuaji na imtoke shaka. Kisha akamwuliza: Umekaa muda gani nawe maiti? Akajibu, naye hajui urefu wa muda wake: Siku moja, au sehemu ya siku. Akaambiwa: Bali umekaa, nawe ni mfu, muda wa miaka mia. Kisha akaonyeshwa jambo jengine kuwa ni dalili ya uweza wa Mwenyezi Mungu. Akamwambia: Angalia chakula chako hakikuchacha, na vinywaji vyako havikutaghayari. Aidha muangalie punda wako. Na hayo tumeyafanya ikudhihirikie uliyo dhani hayawi, ya kufufuliwa vilio kufa, na tukufanye wewe uwe ni Ishara ya kuwaonyesha watu ukweli wa kufufuliwa. Kisha Mwenyezi Mungu akaamrisha atazame maajabu ya kuumba kwake vilivyo na uhai, na vipi anairekibisha mifupa, na kuivisha nyama, kisha akaitia roho vikawa vinataharaki. Basi ulipo mfungukia yule mtu uweza wa Mwenyezi Mungu, na wepesi wa kufufua, alisema: Najua kuwa hakika Mwenyezi Mungu ni Muweza wa kila kitu.

Maana: Swahili Translation - Ali Mohsin Al-Barwani. Translated by Ali Mohsen Al-Barwani Toleo 1.0.1, 2025-06-25. QuranEnc.com

Maana

Au je uliona, ewe Mtume, mfano wa yule aliyepita kwenye kijiji ambacho nyumba zake zilikuwa zimevunjika na kuangukia misingi yake na akasema, «Vipi Allah Mtukufu Atakihuisha kijiji hiki baada ya kuwa kimekufa?» Allah Mtukufu Akamfisha miaka mia moja kisha Akamrudishia roho yake na Akamwambia, «Ni kwa muda gani ulikuwa umekufa?» Akasema, «Nilikuwa nimekufa kwa muda wa siku moja au sehemu ya siku.» Akampa habari kuwa alikuwa amekufa kwa muda wa miaka mia. Na Akamuamrisha akiangalie chakula chake na kinywaji chake vipi Allah Mtukufu Amevihifadhi visiharibike muda huu mrefu. Na Akamuamrisha amtazame punda wake aone vipi Allah Mtukufu Alimuhuisha baada ya kuwa mifupa iliyotapakaa. Na Akamwambia, «Na ili tukufanye wewe ni dalili kwa watu.» Yaani: dalili iliyo wazi ya uwezo wa Allah Mtukufu kufufua baada ya kufa. Na akamuamrisha aitazame mifupa aone vipi Allah Mtukufu Anavyoiinua baadhi yake juu ya mingine na kuiunganisha baadhi yake na mingine na kuivisha nyama baada ya kushikana na kisha kuirudishia uhai.Yalipomfunukia hayo waziwazi alikubali ukubwa wa Allah Mtukufu na kuwa Yeye ni Muweza wa kila kitu. Na akawa ni dalili kwa watu.

Maana: Swahili Translation - Abdullah Muhammad and Nasser Khamis. Translated by Dr. Abdullah Muhammad Abu Bakr & Shaykh Nasser Khamis Toleo 1.0.1, 2026-03-12. QuranEnc.com

Al-Baqara

Kiarabu ni maandishi ya Tanzil, bila kubadilishwa. Maana ni matoleo ya wachapishaji wake, bila kubadilishwa; wahakiki wa Sabīl wenyewe bado hawajazikagua. Kiarabu: maandishi ya Uthmani ya Tanzil, toleo la 1.1. Chanzo: tanzil.net