Ruka hadi kwenye maudhui
Sura ya 2 · Aya ya 255

Al-Baqara 2:255

البقرة

ٱللَّهُ لَآ إِلَـٰهَ إِلَّا هُوَ ٱلْحَىُّ ٱلْقَيُّومُ ۚ لَا تَأْخُذُهُۥ سِنَةٌ وَلَا نَوْمٌ ۚ لَّهُۥ مَا فِى ٱلسَّمَـٰوَٰتِ وَمَا فِى ٱلْأَرْضِ ۗ مَن ذَا ٱلَّذِى يَشْفَعُ عِندَهُۥٓ إِلَّا بِإِذْنِهِۦ ۚ يَعْلَمُ مَا بَيْنَ أَيْدِيهِمْ وَمَا خَلْفَهُمْ ۖ وَلَا يُحِيطُونَ بِشَىْءٍ مِّنْ عِلْمِهِۦٓ إِلَّا بِمَا شَآءَ ۚ وَسِعَ كُرْسِيُّهُ ٱلسَّمَـٰوَٰتِ وَٱلْأَرْضَ ۖ وَلَا يَـُٔودُهُۥ حِفْظُهُمَا ۚ وَهُوَ ٱلْعَلِىُّ ٱلْعَظِيمُ

Maana

Mwenyezi Mungu - hakuna mungu isipokuwa Yeye, Aliye hai, Msimamizi wa mambo yote milele. Hashikwi na kusinzia wala kulala. Ni vyake vilivyomo mbinguni na vilivyomo duniani. Ni nani huyo awezaye kufanya uombezi mbele yake isipokuwa kwa idhini yake? Anayajua yaliyo mbele yao, na yaliyo nyuma yao, wala wao hawajui vyema chochote katika elimu yake isipokuwa kwa kile akitakacho. Kursi (mahali inapokanyaga miguu) yake imeenea mbingu na dunia, na wala halemewi katika kuvilinda vyote viwili. Na Yeye ndiye aliye juu zaidi, Mkuu.

Maana: Swahili Translation - Rowad Translation Center. Issued by the Islamic Content Service Association in Languages Toleo 1.0.5, 2025-12-17. QuranEnc.com

Maana

Mwenyezi Mungu - hapana mungu ila Yeye Aliye hai, Msimamia mambo yote milele. Hashikwi na usingizi wala kulala. Ni vyake pekee vyote viliomo mbinguni na duniani. Ni nani huyo awezaye kuombea mbele yake bila ya idhini yake? Anayajua yaliyo mbele yao na yaliyo nyuma yao; wala wao hawajui chochote katika vilio katika ujuzi wake, ila kwa atakalo mwenyewe. Enzi yake imetanda mbinguni na duniani; na wala haemewi na kuvilinda hivyo. Na Yeye ndiye aliye juu, na ndiye Mkuu. [255]

[255] Mwenyezi Mungu ndiye anaye stahiki kuabudiwa pekee. Yeye ndiye Mwenye kubaki, Mwenye kuyasimamia mambo ya viumbe daima. Haghafiliki kabisa, wala hanyong'onyei, wala halali wala yanayo fanana na hayo, kwani Yeye hasifiki na upungufu wa chochote. Yeye pekee ndiye Mwenye kumiliki mbingu na ardhi, wala hana mshirika yeyote katika hayo. Kwa hivyo hapana kiumbe anaye weza kumwombea mwenginewe ila kwa idhini ya Mwenyezi Mungu. Yeye Subhanahu wa Taa'la anajua kila kitu. Anayajua yaliyo kuwa na yatayo kuwa. Hapana mtu anaye weza kujua kitu katika ilimu ya Mwenyezi Mungu ila atakavyo Yeye ajue na aridhie. Utawala wake umeenea mbinguni na ardhini. Hayamhangaishi Yeye kuyadabiri hayo, kwani Yeye ametukuka, hana upungufu wala kushindwa na jambo, Muadhamu katika utukufu wake na utawala wake. Katika haya upo ushahidi wa kuonyesha ujuzi wa Mwenyezi Mungu wa daima, na Kusimamia kwake kusio koma kwa yote ya mbinguni na duniani. Pia pana ishara ya kuwa Mwenyezi Mungu hapitikiwi na vituko vinavyo zuka.Ilimu ya Sayansi imethibitisha kuwa kulala ni katika sifa ya wanyama na mimea iliyo hai. Ikiwa Mwenyezi Mungu halali basi Yeye ni hai kwa uhai ulio elekeana na dhati yake, lakini sio kama vilivyo hai vinginevyo.

Maana: Swahili Translation - Ali Mohsin Al-Barwani. Translated by Ali Mohsen Al-Barwani Toleo 1.0.1, 2025-06-25. QuranEnc.com

Maana

Allah Mtukufu Ndiye Ambaye hakuna yoyote anayestahiki uungu na kuabudiwa isipokua Yeye. Ndiye Aliye hai Ambaye Amekusanya maana yote ya uhai mkamilifu unaolingana na utukufu Wake. Ndiye Msimamizi wa kila kitu. Kusinzia hakumshiki wala kulala. Kila kilichoko kwenye mbingu na kilichoko kwenye ardhi ni milki Yake. Na hatakua na ujasiri mtu yoyote kuombea mbele Yake isipokuwa kwa ruhusa Yake. Ujuzi Wake umevizunguka vitu vyote vilivyopita, vilivyoko na vitakavyo kuja. Anajua yaliyo mbele ya viumbe katika mambo ambayo yatakuja na yaliyo nyuma yao katika mambo yaliyopita. Na hakuna yoyote, katika viumbe, mwenye kuona chochote katika elimu Yake isipokuwa kadiri ile ambayo Allah Mtukufu Amemjulisha na kumuonesha. Kursîy Yake imeenea kwenye mbingu na ardhi. Kursîy ni mahali pa nyayo za Mola, uliyo mkubwa utukufu Wake, na hakuna ajuwae namna ilivyo isipokuwa ni Allah Mtukufu. Wala hakumlemei Allah Mtukufu aliyetakasika kuzitunza.(hizo mbingu na ardhi).Yeye Ndiye Aliye juu ya viumbe Vyake vyote, kwa dhati Yake na sifa Zake, Aliyekusanya sifa za utukufu na kiburi. Aya hii ni aya tukufu zaidi katika Qur’ani, na inaitwa Ãyah al- Kursîy.

Maana: Swahili Translation - Abdullah Muhammad and Nasser Khamis. Translated by Dr. Abdullah Muhammad Abu Bakr & Shaykh Nasser Khamis Toleo 1.0.1, 2026-03-12. QuranEnc.com

Al-Baqara

Kiarabu ni maandishi ya Tanzil, bila kubadilishwa. Maana ni matoleo ya wachapishaji wake, bila kubadilishwa; wahakiki wa Sabīl wenyewe bado hawajazikagua. Kiarabu: maandishi ya Uthmani ya Tanzil, toleo la 1.1. Chanzo: tanzil.net