Al-Baqara 2:249
البقرةفَلَمَّا فَصَلَ طَالُوتُ بِٱلْجُنُودِ قَالَ إِنَّ ٱللَّهَ مُبْتَلِيكُم بِنَهَرٍ فَمَن شَرِبَ مِنْهُ فَلَيْسَ مِنِّى وَمَن لَّمْ يَطْعَمْهُ فَإِنَّهُۥ مِنِّىٓ إِلَّا مَنِ ٱغْتَرَفَ غُرْفَةًۢ بِيَدِهِۦ ۚ فَشَرِبُوا۟ مِنْهُ إِلَّا قَلِيلًا مِّنْهُمْ ۚ فَلَمَّا جَاوَزَهُۥ هُوَ وَٱلَّذِينَ ءَامَنُوا۟ مَعَهُۥ قَالُوا۟ لَا طَاقَةَ لَنَا ٱلْيَوْمَ بِجَالُوتَ وَجُنُودِهِۦ ۚ قَالَ ٱلَّذِينَ يَظُنُّونَ أَنَّهُم مُّلَـٰقُوا۟ ٱللَّهِ كَم مِّن فِئَةٍ قَلِيلَةٍ غَلَبَتْ فِئَةً كَثِيرَةًۢ بِإِذْنِ ٱللَّهِ ۗ وَٱللَّهُ مَعَ ٱلصَّـٰبِرِينَ
Basi Taluti alipoondoka na majeshi, alisema: Hakika, Mwenyezi Mungu atawajaribu kwa mto. Hivyo basi, atakayekunywa humo, si pamoja nami. Na yule asiyeyaonja, basi huyo atakuwa pamoja nami; ila atakayeteka humo kiasi cha kitanga cha mkono wake. Lakini walikunywa humo isipokuwa wachache tu miongoni mwao. Na alipovuka mto yeye na wale walioamini pamoja naye, walisema: Leo hatumwezi Jaluti (Goliati) na majeshi yake. Wakasema wale wenye yakini ya kukutana na Mwenyezi Mungu: Ni makundi mangapi madogo yalishinda makundi makubwa kwa idhini ya Mwenyezi Mungu? Na Mwenyezi Mungu yu pamoja na wenye kusubiri.
Maana: Swahili Translation - Rowad Translation Center. Issued by the Islamic Content Service Association in Languages Toleo 1.0.5, 2025-12-17. QuranEnc.com
Basi Twaluti alipo ondoka na majeshi alisema: Mwenyezi Mungu atakujaribuni kwa mto. Atakaye kunywa humo si pamoja nami, na asiye kunywa atakuwa pamoja nami: ila atakaye teka kiasi ya kitanga cha mkono wake. Lakini walikunywa humo isipo kuwa wachache tu miongoni mwao. Alipo vuka mto yeye na wale walio amini pamoja naye, walisema: Leo hatumwezi Jaluti (Goliati) na majeshi yake. Wakasema wale wenye yakini ya kukutana na Mwenyezi Mungu: Makundi mangapi madogo yameshinda makundi makubwa kwa idhini ya Mwenyezi Mungu. Na Mwenyezi Mungu yu pamoja na wenye kusubiri. [249]
[249] Taluti alipo toka nao aliwaambia: "Mwenyezi Mungu anakujaribuni kwa mto ambao mtaukuta njiani mwenu. Msinywe katika mto huo ila tama moja tu. Mwenye kunywa zaidi ya hivyo basi hayumo katika jeshi letu, wala jamii yetu. Kwani amekuwa ameacha kumt'ii Mwenyezi Mungu. Wala asinifuate ila yule ambaye hakunywa ila tama moja tu." Hawakuweza kuvumilia jaribio hili, wakanywa maji mengi, ila wachache tu kati yao. Basi akafuatana na hichi kikundi kidogo akavuka nao mto. Walipoona wingi wa maadui wao walisema: "Hatutoweza hii leo kupigana na Jaluti na askari wake kwa wingi wao na uchache wetu." Baadhi yao wenye nyoyo madhbuti kwa kutaraji kwao malipo ya Mwenyezi Mungu watapo kutana naye, walisema: "Msiogope kitu! Mara nyingi wachache wenye kuamini huwashinda wengi walio makafiri. Subirini, kwani ushindi watapata wenye kusubiri."
Maana: Swahili Translation - Ali Mohsin Al-Barwani. Translated by Ali Mohsen Al-Barwani Toleo 1.0.1, 2025-06-25. QuranEnc.com
Alipotoka Twalut na askari wake kwenda kupigana na watu majabari, aliwaambia, Allah Mtukufu Atawapa mtihani wa subira kwa mto uliyo mbele yenu mtakaouvuka, ili abainike mwenye Imani na aliye mnafiki. Yoyote kati yenu atakaye kunywa maji ya mto huo, si katika mimi, wala hafai kuwa na mimi kwenye jihadi. Na yule ambaye hatayaonja maji hayo, yeye ni katika mimi, kwa kutii amri yangu, na anafaa kwa jihadi. Isipokuwa aliyeruhusiwa na akateka mteko mmoja kwa mkono wake, huyo hana lawama. Basi walipofika mtoni, waliyaangukia maji na waliyanywa sana isipokuwa idadi ya watu wachache kati yao, walisubiri juu ya kiu na joto na wakatosheka na mteko wa mkono. Wakati huo wale walioasi amri, walirudi nyuma. Ṭālūt pamoja na wale Waumini wachache walipouvuka mto – walikuwa watu zaidi ya mia tatu na kumi- kwa ajili ya kupambana na maadui zao na wakaona wingi wa maadui zao na wingi wa silaha walionazo, walisema, Hatuna uwezo leo wa kupigana na Jālūt na askari wake wenye nguvu. Hapo, wale waliokuwa na yakini ya kukutana na Mola Wao walijibu wakiwakumbusha ndugu zao juu ya Allah Mtukufu na uwezo Wake, Ni vikundi vingapi vichache, venye imani na subira, viliyashinda, kwa idhini ya Allah Mtukufu, makundi yaliyokuwa na watu wengi makafiri wenye kuasi, kwa idhini ya Allah Mtukufu. Allah Mtukufu Yupo pamoja na wenye subira kwa taufiki Yake na nusura Yake na malipo Yake mema.
Maana: Swahili Translation - Abdullah Muhammad and Nasser Khamis. Translated by Dr. Abdullah Muhammad Abu Bakr & Shaykh Nasser Khamis Toleo 1.0.1, 2026-03-12. QuranEnc.com
Kiarabu ni maandishi ya Tanzil, bila kubadilishwa. Maana ni matoleo ya wachapishaji wake, bila kubadilishwa; wahakiki wa Sabīl wenyewe bado hawajazikagua. Kiarabu: maandishi ya Uthmani ya Tanzil, toleo la 1.1. Chanzo: tanzil.net