Al-Baqara 2:235
البقرةوَلَا جُنَاحَ عَلَيْكُمْ فِيمَا عَرَّضْتُم بِهِۦ مِنْ خِطْبَةِ ٱلنِّسَآءِ أَوْ أَكْنَنتُمْ فِىٓ أَنفُسِكُمْ ۚ عَلِمَ ٱللَّهُ أَنَّكُمْ سَتَذْكُرُونَهُنَّ وَلَـٰكِن لَّا تُوَاعِدُوهُنَّ سِرًّا إِلَّآ أَن تَقُولُوا۟ قَوْلًا مَّعْرُوفًا ۚ وَلَا تَعْزِمُوا۟ عُقْدَةَ ٱلنِّكَاحِ حَتَّىٰ يَبْلُغَ ٱلْكِتَـٰبُ أَجَلَهُۥ ۚ وَٱعْلَمُوٓا۟ أَنَّ ٱللَّهَ يَعْلَمُ مَا فِىٓ أَنفُسِكُمْ فَٱحْذَرُوهُ ۚ وَٱعْلَمُوٓا۟ أَنَّ ٱللَّهَ غَفُورٌ حَلِيمٌ
Wala hakuna ubaya juu yenu katika kupeleka posa kwa ishara tu kwa wanawake walio katika eda au mkalificha ndani ya nyoyo zenu. Mwenyezi Mungu alikwishajua kwamba nyinyi mtawakumbuka. Lakini msiwaahidi kwa siri, isipokuwa mseme maneno mema. Wala msiazimie kufunga mkataba wa ndoa mpaka andiko (la amri ya eda) lifike muda wake. Na jueni kwamba Mwenyezi Mungu kwa hakika anajua yaliyo katika nafsi zenu. Basi jitahadharini naye. Na jueni kwamba Mwenyezi Mungu ni Mwenye kusamehe, Mpole.
Maana: Swahili Translation - Rowad Translation Center. Issued by the Islamic Content Service Association in Languages Toleo 1.0.5, 2025-12-17. QuranEnc.com
Wala si vibaya kwenu katika kupeleka posa kwa ishara tu kwa wanawake waliomo edani au mkadhamiria katika nyoyo zenu. Mwenyezi Mungu anajua kwamba nyinyi mtawakumbuka. Lakini msiwaahidi kwa siri, ila mnene maneno mema. Wala msiazimie kufunga ndoa mpaka eda ifike mwisho wake. Na jueni kwamba Mwenyezi Mungu anajua yaliyomo katika nafsi zenu. Basi tahadharini naye. Na jueni kwamba Mwenyezi Mungu ni Mwenye kusamehe na Mpole. [235]
[235] Katika muda wa eda hapana dhambi kwenu, nyinyi wanaume, mkiwaonyesha dalili kuwa mnadhamiria kutaka kuwaoa waliomo edani kwa kufiwa na waume zao, lakini hayo yawe ni kudhamiria ndani ya moyo tu. Mwenyezi Mungu hakika anajua kuwa hamwezi kuacha kuwazungumza waliomo edani, kwani ni maumbile baina ya wanaume na wanawake. Kwa hivyo mmepewa ruhusa kuashiria bila ya kubainisha kwa maneno. Basi msiwape ahadi ya kuwaoa ila iwe ishara isiyo ovu wala ya uchafu. Basi msifunge ndoa mpaka baada ya kwisha eda. Na kuweni yakini kuwa Mwenyezi Mungu anayajua mnayo yaficha ndani ya nyoyo zenu. Basi iogopeni adhabu yake, wala msitende anayo kukatazeni. Wala msikate tamaa na rehema yake pale mnapo ikhalifu amri yake, kwani Yeye ni Mwenye kughufiria mno, na anakubali toba ya waja wake, na anasamehe makosa, kama alivyo Mpole hafanyi haraka ya kuwaadhibu wale wanao vunja aliyo yakataza.
Maana: Swahili Translation - Ali Mohsin Al-Barwani. Translated by Ali Mohsen Al-Barwani Toleo 1.0.1, 2025-06-25. QuranEnc.com
Na wala nyinyi hamna dhambi, enyi wanaume, katika ishara mnazozitoa za kutaka kuwaoa wanawake waliofiliwa na waume zao au wale waliopewa talaka ya mwisho, wakiwa wako katika eda lao. Pia hamna dhambi katika mawazo yanayowapitia ndani ya nafsi zenu ya kutaka kuwaoa wamalizapo eda lao. Allah Mtukufu Anajua kwamba nyinyi mtawataja wanawake walio kwenye eda na hamtasubiri kuweza kunyamaza kutowataja, kwa udhaifu wenu. Kwa ajili hiyo, Allah Mtukufu amewahalalishia kuwataja kwa ishara au kwa kudhamiria ndani ya nafsi zenu. Na jihadharini kuagana nao kisiri, kwa kuzini, au kukubaliana kuoana wakiwa bado wako kwenye eda, isipokuwa mtakaposema neno lenye maana kwamba mfano wake, mwanamke huyo, waume huwa wanampendelea. Wala msikusudie kufunga ndoa katika kipindi cha eda mpaka muda wake umalizike. Na jueni kwamba Allah Mtukufu Anayajua yaliyomo katika nafsi zenu, kwa hivyo muogopeni Yeye. Na jueni kwamba Allah Mtukufu ni Mwingi wa kusamehe kwa mwenye kutubia dhambi zake, ni Mpole kwa waja Wake, Hana haraka ya kuwatesa.
Maana: Swahili Translation - Abdullah Muhammad and Nasser Khamis. Translated by Dr. Abdullah Muhammad Abu Bakr & Shaykh Nasser Khamis Toleo 1.0.1, 2026-03-12. QuranEnc.com
Kiarabu ni maandishi ya Tanzil, bila kubadilishwa. Maana ni matoleo ya wachapishaji wake, bila kubadilishwa; wahakiki wa Sabīl wenyewe bado hawajazikagua. Kiarabu: maandishi ya Uthmani ya Tanzil, toleo la 1.1. Chanzo: tanzil.net