Ruka hadi kwenye maudhui
Sura ya 2 · Aya ya 233

Al-Baqara 2:233

البقرة

وَٱلْوَٰلِدَٰتُ يُرْضِعْنَ أَوْلَـٰدَهُنَّ حَوْلَيْنِ كَامِلَيْنِ ۖ لِمَنْ أَرَادَ أَن يُتِمَّ ٱلرَّضَاعَةَ ۚ وَعَلَى ٱلْمَوْلُودِ لَهُۥ رِزْقُهُنَّ وَكِسْوَتُهُنَّ بِٱلْمَعْرُوفِ ۚ لَا تُكَلَّفُ نَفْسٌ إِلَّا وُسْعَهَا ۚ لَا تُضَآرَّ وَٰلِدَةٌۢ بِوَلَدِهَا وَلَا مَوْلُودٌ لَّهُۥ بِوَلَدِهِۦ ۚ وَعَلَى ٱلْوَارِثِ مِثْلُ ذَٰلِكَ ۗ فَإِنْ أَرَادَا فِصَالًا عَن تَرَاضٍ مِّنْهُمَا وَتَشَاوُرٍ فَلَا جُنَاحَ عَلَيْهِمَا ۗ وَإِنْ أَرَدتُّمْ أَن تَسْتَرْضِعُوٓا۟ أَوْلَـٰدَكُمْ فَلَا جُنَاحَ عَلَيْكُمْ إِذَا سَلَّمْتُم مَّآ ءَاتَيْتُم بِٱلْمَعْرُوفِ ۗ وَٱتَّقُوا۟ ٱللَّهَ وَٱعْلَمُوٓا۟ أَنَّ ٱللَّهَ بِمَا تَعْمَلُونَ بَصِيرٌ

Maana

Na wazazi wanawake wawanyonyeshe watoto wao miaka miwili kamili kwa anayetaka kutimiza kunyonyesha. Na ni juu ya aliyezaliwa mwana huyo chakula chao na mavazi yao kwa wema. Wala halazimishwi mtu isipokuwa kwa kiwango cha uwezo wake. Mama asitaabishwe kwa sababu ya mwanawe, wala yule aliyezaliwa mwana kwa sababu ya mwanawe. Na juu ya mrithi ni mfano wa hivyo. Na kama wote wawili watataka kumwachisha kunyonya kwa kuridhiana na kushauriana, basi hakuna ubaya juu yao. Na mkitaka kuwapa watoto wenu mama wa kuwanyonyesha, basi hakuna ubaya juu yenu ikiwa mtapeana mlichoahidi kwa wema. Na mcheni Mwenyezi Mungu. Na jueni kwamba Mwenyezi Mungu anayaona vyema mnayoyatenda.

Maana: Swahili Translation - Rowad Translation Center. Issued by the Islamic Content Service Association in Languages Toleo 1.0.5, 2025-12-17. QuranEnc.com

Maana

Na wazazi wanawake wawanyonyeshe watoto wao miaka miwili kaamili kwa anaye taka kutimiza kunyonyesha. Na juu ya baba yake chakula cha kina mama, na nguo zao kwa mujibu wa ada. Wala halazimishwi mtu ila kwa kadiri ya uwezo wake. Mama asitiwe taabuni kwa ajili ya mwanawe, wala baba kwa ajili ya mwanawe. Na juu ya mrithi mfano wa hivyo. Na kama wote wawili wakitaka kumwachisha ziwa kwa kuridhiana na kushauriana, basi si vibaya kwao. Na mkitaka kuwapatia watoto wenu mama wa kuwanyonyesha basi hapana ubaya kwenu mkitoa mlicho ahidi kwa mujibu wa ada. Na mcheni Mwenyezi Mungu, na jueni kwamba Mwenyezi Mungu anayaona yote mnayo yatenda. [233]

[233] Ni juu ya kina mama kuwanyonyesha wana wao muda wa miaka miwili iliyo timia kwa maslaha ya mtoto mchanga, akitaka hayo mmojapo au wote kati ya wazazi. Itamlazimu baba, kwa kuwa mtoto ni wake, amkimu mama kwa chakula na nguo kwa uwezo wake bila ya israfu wala uchoyo. Kwani haimlazimu mtu kufanya ila kiasi ya uwezo wake, na wala haitakikani kumletea madhara mama kwa kumnyima haki yake ya kumkimu yeye na kumlea mwana. Kadhaalika haitakikani mtoto awe sababu ya kumletea madhara baba yake kwa kumkalifu zaidi kuliko uwezo wake, au kumharimisha haki yake kwa mwanawe. Na akifa baba au akawa fakiri hawezi kazi kiamu kitakuwa juu ya mrithi wa mtoto ikiwa mtoto ana mali yake. Wakitaka wazazi kumwachisha ziwa mtoto kabla ya kutimia miaka miwili wakakubaliana kwa hayo na huku wakiangalia maslaha ya mtoto basi hapana ubaya. Na nyinyi wazazi mkitaka kumpa mama mwingine kumnyonyesha mtoto pia hapana ubaya - na hapo mtamtolea ujira kwa ridhaa na ihsani. Katika myatendayo muangalieni Mwenyezi Mungu, na mjue kuwa Yeye anayajua myatendayo na atakulipeni kwayo. Qur'ani inawajibisha mama amnyonyeshe mwanawe na asinyonyeshwe na mwingine ila kwa dharura, kwani kunyonyesha yeye ni faida kwa mama na mtoto katika siha. Na kuachisha ziwa kuwe kwa taratibu, na yajuzu kabla ya kutimiza muda ikiwa siha ya mtoto inaruhusu hayo

Maana: Swahili Translation - Ali Mohsin Al-Barwani. Translated by Ali Mohsen Al-Barwani Toleo 1.0.1, 2025-06-25. QuranEnc.com

Maana

Na ni juu ya wanawake waliozaa kuwanyonyesha watoto wao muda wa miaka miwili kamili, kwa yule atakaye kukamilisha unyonyeshaji. Na ni wajibu kwa mababa kuwadhamini wanyonyeshaji, waliopewa talaka, kwa chakula chao na mavazi yao kwa njia ipendezayo kisheria na kimila. Kwani Allah Mtukufu hamkalifishi mtu ila kiasi cha uwezo wake. Na haifai kwa wazazi wawili kumfanya mtoto aliyezaliwa kuwa ni njia ya kudhuriana kati yao. Na inamlazimu mrithi, mzazi anapokufa, kile kinachomlazimu mzazi, kabla hajafa, cha matumizi na mavazi. Na wazazi wanapotaka kumuachisha mtoto kunyonya, kabla kukamilisha miaka miwili, basi si makosa kwao iwapo wameridhiana na kushawiriana kwa hilo na kufikia kwenye uamuzi wenye maslahi ya mtoto. Na iwapo wazazi wawili wamekubaliana kumpa mtoto mnyonyeshaji mwengine asiyekuwa mamake ili amnyonyeshe, pia si makosa kwao., iwapo baba atampa mama haki yake, na pia atampa mwenye kunyonyesha haki kwa mujibu wa desturi zinazoeleweka kwa watu. Na muogopeni Allah Mtukufu katika hali zenu zote. Na mjue kwamba Allah Mtukufu kwa mnayoyafanya ni muoni na Atawalipa kwayo.

Maana: Swahili Translation - Abdullah Muhammad and Nasser Khamis. Translated by Dr. Abdullah Muhammad Abu Bakr & Shaykh Nasser Khamis Toleo 1.0.1, 2026-03-12. QuranEnc.com

Al-Baqara

Kiarabu ni maandishi ya Tanzil, bila kubadilishwa. Maana ni matoleo ya wachapishaji wake, bila kubadilishwa; wahakiki wa Sabīl wenyewe bado hawajazikagua. Kiarabu: maandishi ya Uthmani ya Tanzil, toleo la 1.1. Chanzo: tanzil.net