Ruka hadi kwenye maudhui
Sura ya 2 · Aya ya 221

Al-Baqara 2:221

البقرة

وَلَا تَنكِحُوا۟ ٱلْمُشْرِكَـٰتِ حَتَّىٰ يُؤْمِنَّ ۚ وَلَأَمَةٌ مُّؤْمِنَةٌ خَيْرٌ مِّن مُّشْرِكَةٍ وَلَوْ أَعْجَبَتْكُمْ ۗ وَلَا تُنكِحُوا۟ ٱلْمُشْرِكِينَ حَتَّىٰ يُؤْمِنُوا۟ ۚ وَلَعَبْدٌ مُّؤْمِنٌ خَيْرٌ مِّن مُّشْرِكٍ وَلَوْ أَعْجَبَكُمْ ۗ أُو۟لَـٰٓئِكَ يَدْعُونَ إِلَى ٱلنَّارِ ۖ وَٱللَّهُ يَدْعُوٓا۟ إِلَى ٱلْجَنَّةِ وَٱلْمَغْفِرَةِ بِإِذْنِهِۦ ۖ وَيُبَيِّنُ ءَايَـٰتِهِۦ لِلنَّاسِ لَعَلَّهُمْ يَتَذَكَّرُونَ

Maana

Wala msiwaoe wanawake washirikina mpaka waamini. Na mjakazi Muumini ni bora kuliko mwanamke mshirikina hata akiwapendeza. Wala msiwaoze (binti zenu) wanaume washirikina mpaka waamini. Na mtumwa mwanamume Muumini ni bora kuliko mwanamume mshirikina hata akiwapendeza. Hao wanaitia kwenye Moto, naye Mwenyezi Mungu anaitia kwenye Bustani na maghfira kwa idhini yake. Naye huwabainishia Aya zake watu ili wapate kukumbuka.

Maana: Swahili Translation - Rowad Translation Center. Issued by the Islamic Content Service Association in Languages Toleo 1.0.5, 2025-12-17. QuranEnc.com

Maana

Wala msiwaoe wanawake washirikina mpaka waamini. Na mjakazi Muumini ni bora kuliko mshirikina hata akikupendezeni. Wala msiwaoze (binti zenu) wanaume washirikina mpaka waamini. Na mtumwa mwanamume Muumini ni bora kuliko mshirikina hata akikupendezeni. Hao wanaitia kwenye Moto, na Mwenyezi Mungu anaitia kwenye Pepo na maghafira kwa idhini yake. Naye huzibainisha Aya zake kwa watu ili wapate kukumbuka. [221]

[221] Hapana ubaya wowote kuchanganyika na mayatima, lakini kuchanganyika na washirikina ni vibaya. Muumini hana ruhusa kumwoa mshirikina asiye fuata dini ya Kitabu cha mbinguni. Basi msipelekewe kutaka kumwoa mwanamke wa kishirikina kwa ajili ya mali yake, au uzuri wake, au jaha yake, au ukoo wake. Muumini aliye mtumwa ni bora kuliko mshirikina aliye huru mwenye mali, na jamali, na utukufu na nasaba. Wala nyinyi msiwaoeze wanawake walio mikononi mwenu wanaume wa kishirikina wasio amini Vitabu vya mbinguni, wala yasikupelekeeni kumkhiari mshirikina utajiri na cheo chake. Mtumwa Muumini ni bora kuliko huyo. Hao washirikina wanawavutia wenzao kwenda katika maasi na ushirikina, na kwa hivyo wanapaswa kuingia Motoni. Na Mwenyezi Mungu anapo kulinganieni mjitenge na ndoa za washirikina anakulinganieni kwa ajili ya maslaha yenu na mwongoke ili mpate Pepo na maghfira, na mwende katika njia ya kheri kwa taisiri. Na Mwenyezi Mungu anabainisha sharia zake na uwongofu wake kwa watu wapate kujua maslaha yao na kheri yao.

Maana: Swahili Translation - Ali Mohsin Al-Barwani. Translated by Ali Mohsen Al-Barwani Toleo 1.0.1, 2025-06-25. QuranEnc.com

Maana

Wala msiwaoe, enyi Waislamu, wanawake washirikina wanaoabudu masanamu mpaka waingie katika Uislamu. Na mjue kwamba mwanamke kijakazi, asiyekuwa na mali wala utukufu wa nasaba, anayemuamini Allah Mtukufu, ni bora kuliko mwanamke mshirikina, hata kama huyo mshirikina muungwana atawavutia. Wala msiwaoze wanawake wenu waumini, wakiwa ni vijakazi au waungwana, wanaume washirikina mpaka wamuamini Allah Mtukufu na Mtume Wake. Na mjue kwamba mtumwa mwenye Imani, pamoja na ufukara wake, ni bora kuliko mshirikina, hata kama huyo mshirikina atawavutia. Hao wasifikao na ushirikina, wanaume na wanawake, wanamwita kila atangamanaye nao kwenye mambo yapelekayo Motoni. Na Allah Mtukufu, Aliyetakasika na kila sifa ya upungufu, Anawaita waja Wake kwenye dini Yake ya haki inayowapeleka Peponi na kusamehawa madhambi yao kwa idhini Yake. Na Yeye Anabainisha aya Zake na hukumu Zake kwa watu, ili wapate kukumbuka na wazingatie.

Maana: Swahili Translation - Abdullah Muhammad and Nasser Khamis. Translated by Dr. Abdullah Muhammad Abu Bakr & Shaykh Nasser Khamis Toleo 1.0.1, 2026-03-12. QuranEnc.com

Al-Baqara

Kiarabu ni maandishi ya Tanzil, bila kubadilishwa. Maana ni matoleo ya wachapishaji wake, bila kubadilishwa; wahakiki wa Sabīl wenyewe bado hawajazikagua. Kiarabu: maandishi ya Uthmani ya Tanzil, toleo la 1.1. Chanzo: tanzil.net