Ruka hadi kwenye maudhui
Sura ya 2 · Aya ya 217

Al-Baqara 2:217

البقرة

يَسْـَٔلُونَكَ عَنِ ٱلشَّهْرِ ٱلْحَرَامِ قِتَالٍ فِيهِ ۖ قُلْ قِتَالٌ فِيهِ كَبِيرٌ ۖ وَصَدٌّ عَن سَبِيلِ ٱللَّهِ وَكُفْرٌۢ بِهِۦ وَٱلْمَسْجِدِ ٱلْحَرَامِ وَإِخْرَاجُ أَهْلِهِۦ مِنْهُ أَكْبَرُ عِندَ ٱللَّهِ ۚ وَٱلْفِتْنَةُ أَكْبَرُ مِنَ ٱلْقَتْلِ ۗ وَلَا يَزَالُونَ يُقَـٰتِلُونَكُمْ حَتَّىٰ يَرُدُّوكُمْ عَن دِينِكُمْ إِنِ ٱسْتَطَـٰعُوا۟ ۚ وَمَن يَرْتَدِدْ مِنكُمْ عَن دِينِهِۦ فَيَمُتْ وَهُوَ كَافِرٌ فَأُو۟لَـٰٓئِكَ حَبِطَتْ أَعْمَـٰلُهُمْ فِى ٱلدُّنْيَا وَٱلْـَٔاخِرَةِ ۖ وَأُو۟لَـٰٓئِكَ أَصْحَـٰبُ ٱلنَّارِ ۖ هُمْ فِيهَا خَـٰلِدُونَ

Maana

Wanakuuliza juu ya kupigana vita katika mwezi mtakatifu. Sema: Kupigana vita ndani yake ni dhambi kubwa. Lakini kuzuia watu wasiende katika Njia ya Mwenyezi Mungu na kumkufuru Yeye, na kuzuilia watu wasiende kwenye Msikiti Mtakatifu na kuwatoa watu wake humo, ni makubwa zaidi mbele ya Mwenyezi Mungu. Na fitina ni jambo kubwa zaidi kuliko kuua. Wala hawataacha kupigana nanyi mpaka wawatoe katika Dini yenu kama wakiweza. Na yeyote katika nyinyi atakayeacha Dini yake, na akafa hali ya kuwa ni kafiri, basi hao ndio ambao matendo yao yameharibika katika dunia na Akhera. Na hao ndio watu wa Motoni. Wao humo watadumu.

Maana: Swahili Translation - Rowad Translation Center. Issued by the Islamic Content Service Association in Languages Toleo 1.0.5, 2025-12-17. QuranEnc.com

Maana

Wanakuuliza juu ya kupigana vita katika mwezi mtakatifu. Sema: Kupigana vita wakati huo ni dhambi kubwa. Lakini kuzuilia watu wasende katika Njia ya Mwenyezi Mungu na kumkanusha Yeye, na kuzuilia watu wasende kwenye Msikiti Mtakatifu na kuwatoa watu wake humo, ni makubwa zaidi mbele ya Mwenyezi Mungu. Na fitina ni mbaya zaidi kuliko kuuwa. Wala hawatoacha kupigana nanyi mpaka wakutoeni katika Dini yenu kama wakiweza. Na yeyote katika nyinyi akiacha Dini yake akafa naye ni kafiri, basi hao ndio ambao a'mali zao zimeharibika duniani na Akhera. Na hao ndio watu wa Motoni; humo watadumu. [217]

[217] Waislamu walichukia kupigana katika mwezi mtakatifu, ndio wakakuuliza juu yake. Waambie: Naam, kupigana katika mwezi mtakatifu ni dhambi kubwa. Lakini kubwa zaidi ni haya wayatendayo maadui zenu nayo: kuwazuia watu wasifuate Njia ya Mwenyezi Mungu, wasende kwenye Msikiti Mtakatifu, na kuwafukuza Waislamu kutoka Makka. Na hayo maudhi na mateso yao kuwafanyia Waislamu ili waache Dini yao ni makubwa zaidi kuliko mauwaji yoyote. Kwa hivyo imehalalishwa kupigana vita katika mwezi mtakatifu kwa ajili ya kupambana na maovu haya. Hichi ni kitendo kikubwa cha kujikinga na lilio kubwa zaidi. Enyi Waislamu! Jueni kuwa mwendo wa watu hawa ni mwendo wa ukhalifu na udhaalimu. Na wao hawakubali kwenu uadilifu wala mambo ya kiakili. Na wala hawatasita kukupigeni vita mpaka wakuachisheni Dini yenu pindi wakiweza. Na atakaye dhoofika kwa mashambulio yao akaacha Dini yake na akafa katika ukafiri, basi watu kama hao watapoteza vitendo vyao vyema vyote vya duniani na Akhera. Na hao ni watu wa Motoni ambako watadumu.

Maana: Swahili Translation - Ali Mohsin Al-Barwani. Translated by Ali Mohsen Al-Barwani Toleo 1.0.1, 2025-06-25. QuranEnc.com

Maana

Wanakuuliza washirikina, ewe Mtume, kuhusu mwezi mtukufu wa Ḥaram, «Inafaa kupigana ndani yake?» Waambie, Kupigana katika mwezi mtukufu wa Ḥaram ni jambo kubwa kwa Allah Mtukufu kuuhalalisha na kumwaga damu ndani yake. Na kuwazuia kwenu watu kuingia katika Uislamu, kwa kuwaadhibu na kuwatisha na kumkanusha kwenu Allah Mtukufu na Mtume Wake na dini Yake, na kuwazuia Waislamu wasiingie kwenye Msikiti wa Ḥaram, na kumtoa Nabii na waliohama naye kutoka huko, ambao wao ndio wakazi na wasimamizi wake, hilo ni dhambi kubwa mno na nikosa kubwa mno kwa Allah Mtukufu kuliko kupigana katika mwezi mtukufu wa Ḥaram. Na ushirikina mlionao ni jambo kubwa zaidi na baya zaidi kuliko kuua katika mwezi mtukufu wa Haram. Na Makafiri hawa hawatatishika na kukomeka na makosa yao, bali wao ni wenye kuendelea nayo. Wala hawataacha kuwapiga vita mpaka wawatoe kwenye Uislamu kuwatia kwenye ukafiri, iwapo wataweza kulihakikisha hilo. Na mwenye kuwatii wao, kati yenu, enyi Waislamu, akaacha dini yake na akafa katika ukafiri, basi amali zake zitapotea duniani na Akhera na atakuwa ni miongoni mwa watakaodumu kwenye moto wa Jahanamu, hatatoka humo milele.

Maana: Swahili Translation - Abdullah Muhammad and Nasser Khamis. Translated by Dr. Abdullah Muhammad Abu Bakr & Shaykh Nasser Khamis Toleo 1.0.1, 2026-03-12. QuranEnc.com

Al-Baqara

Kiarabu ni maandishi ya Tanzil, bila kubadilishwa. Maana ni matoleo ya wachapishaji wake, bila kubadilishwa; wahakiki wa Sabīl wenyewe bado hawajazikagua. Kiarabu: maandishi ya Uthmani ya Tanzil, toleo la 1.1. Chanzo: tanzil.net