Al-Baqara 2:213
البقرةكَانَ ٱلنَّاسُ أُمَّةً وَٰحِدَةً فَبَعَثَ ٱللَّهُ ٱلنَّبِيِّـۧنَ مُبَشِّرِينَ وَمُنذِرِينَ وَأَنزَلَ مَعَهُمُ ٱلْكِتَـٰبَ بِٱلْحَقِّ لِيَحْكُمَ بَيْنَ ٱلنَّاسِ فِيمَا ٱخْتَلَفُوا۟ فِيهِ ۚ وَمَا ٱخْتَلَفَ فِيهِ إِلَّا ٱلَّذِينَ أُوتُوهُ مِنۢ بَعْدِ مَا جَآءَتْهُمُ ٱلْبَيِّنَـٰتُ بَغْيًۢا بَيْنَهُمْ ۖ فَهَدَى ٱللَّهُ ٱلَّذِينَ ءَامَنُوا۟ لِمَا ٱخْتَلَفُوا۟ فِيهِ مِنَ ٱلْحَقِّ بِإِذْنِهِۦ ۗ وَٱللَّهُ يَهْدِى مَن يَشَآءُ إِلَىٰ صِرَٰطٍ مُّسْتَقِيمٍ
Watu wote walikuwa umma mmoja. Kisha Mwenyezi Mungu akawatuma Manabii wenye kupeana habari njema na waonyaji. Na akateremsha pamoja nao Kitabu kwa haki, ili kihukumu baina ya watu katika yale waliyohitilafiana. Na wala hawakuhitilafiana ndani yake isipokuwa wale waliopewa Kitabu hicho baada ya kufikiwa na hoja zilizo wazi, kwa sababu ya husuda ya baina yao. Ndipo Mwenyezi Mungu kwa idhini yake akawaongoa walioamini kuiendea haki katika yale waliyohitilafiana ndani yake. Na Mwenyezi Mungu humwongoa amtakaye kwenye Njia iliyonyooka.
Maana: Swahili Translation - Rowad Translation Center. Issued by the Islamic Content Service Association in Languages Toleo 1.0.5, 2025-12-17. QuranEnc.com
Watu wote walikuwa ni umma mmoja. Mwenyezi Mungu akapeleka Manabii wabashiri na waonyaji. Na pamoja nao akateremsha Kitabu kwa Haki, ili kihukumu baina ya watu katika yale walio khitalifiana. Na wala hawakukhitalifiana ila wale walio pewa Kitabu hicho baada ya kuwafikia hoja zilizo wazi, kwa sababu ya uhasidi baina yao. Ndipo Mwenyezi Mungu kwa idhini yake akawaongoa walio amini kwendea haki katika mambo waliyo khitalifiana. Na Mwenyezi Mungu humwongoa amtakaye kwenye Njia Iliyo Nyooka. [213]
[213] Hakika watu wana tabia moja ya kuwa wapo tayari kupotoka, na wapo ambao sababu za uwongofu zinakuwa na nguvu kwao, na wengine upotovu ndio unawatawala. Kwa hivyo wakakhitalifiana. Mwenyezi Mungu akawapelekea Manabii kuwaongoa na kuwabashiria kheri na kuwaonya. Na akateremsha kwa hao Manabii Vitabu vyenye kukusanya Haki, ili viwe ndivyo vya kuwahukumu iondoke mizozo baina yao. Lakini wale walio nafiika na uwongofu wa Manabii ndio wao tu walio amini, hao ambao Mwenyezi Mungu amewaongoa kutokana na khitilafu wakafuata Haki. Na Mwenyezi Mungu ndiye anaye wapa tawfiqi watu wa Haki pindi wakisafi niya zao.
Maana: Swahili Translation - Ali Mohsin Al-Barwani. Translated by Ali Mohsen Al-Barwani Toleo 1.0.1, 2025-06-25. QuranEnc.com
Watu walikuwa ni kundi moja, wameafikiana katika kumuamini Allah Mtukufu, kisha walitafautiana katika dini yao.Hapo ndipo Allah Mtukufu Aliwatuma Manabii, wakiwa ni walinganizi wa dini ya Allah Mtukufu, ni wabashiri wa Pepo kwa anayemtii Allah Mtukufu na ni waonyi wa Moto kwa anayemkanusha na kumuasi. Na Akateremsha, pamoja nao, vitabu vya mbinguni vilivyokusanya haki, ili wahukumu baina ya watu kwa yaliyomo ndani, katika yale waliyotafautiana juu yake. Na hawakutafautiana juu ya jambo la Mtume na Kitabu alichokuja nacho, kwa uhasidi na udhalimu, isipokuwa ni wale ambao Allah Mtukufu Amewapa Taurati na wakayajua yaliyomo ndani miongoni mwa hoja na hukumu. Hapo Allah Mtukufu, kwa fadhila zake, aliwaafikia Waumini kuipambanua haki na batili na kuyajua yale waliotafautiana juu yake. Allah Mtukufu Anampa taufiki amtakaye, miongoni mwa waja wake, kufuata njia iliyonyooka.
Maana: Swahili Translation - Abdullah Muhammad and Nasser Khamis. Translated by Dr. Abdullah Muhammad Abu Bakr & Shaykh Nasser Khamis Toleo 1.0.1, 2026-03-12. QuranEnc.com
Kiarabu ni maandishi ya Tanzil, bila kubadilishwa. Maana ni matoleo ya wachapishaji wake, bila kubadilishwa; wahakiki wa Sabīl wenyewe bado hawajazikagua. Kiarabu: maandishi ya Uthmani ya Tanzil, toleo la 1.1. Chanzo: tanzil.net