Al-Baqara 2:197
البقرةٱلْحَجُّ أَشْهُرٌ مَّعْلُومَـٰتٌ ۚ فَمَن فَرَضَ فِيهِنَّ ٱلْحَجَّ فَلَا رَفَثَ وَلَا فُسُوقَ وَلَا جِدَالَ فِى ٱلْحَجِّ ۗ وَمَا تَفْعَلُوا۟ مِنْ خَيْرٍ يَعْلَمْهُ ٱللَّهُ ۗ وَتَزَوَّدُوا۟ فَإِنَّ خَيْرَ ٱلزَّادِ ٱلتَّقْوَىٰ ۚ وَٱتَّقُونِ يَـٰٓأُو۟لِى ٱلْأَلْبَـٰبِ
Hija ni miezi maalumu. Basi anayehirimia Hija ndani yake (miezi hiyo), basi asijamiiane wala asipindukie mipaka wala asibishane katika Hija. Na chochote mnachokifanya katika heri, Mwenyezi Mungu anaijua. Na chukueni masurufu. Na hakika, masurufu (yaliyo) bora zaidi ni ucha Mungu. Na nicheni Mimi, enyi wenye akili ya hali ya juu!
Maana: Swahili Translation - Rowad Translation Center. Issued by the Islamic Content Service Association in Languages Toleo 1.0.5, 2025-12-17. QuranEnc.com
Hija ni miezi maalumu. Na anaye kusudia kufanya Hija katika miezi hiyo, basi asiseme maneno machafu wala asifanye vitendo vichafu wala asibishane katika Hija. Na kheri yoyote mnayo ifanya Mwenyezi Mungu anaijua. Na jitengezeeni zawadi. Na hakika bora ya zawadi ni uchamngu. Na nicheni Mimi, enyi wenye akili! [197]
[197] Na Hija inakuwa katika miezi mnayo ijua, kwani jambo hili ni maarufu kwenu tangu zama za Ibrahim a.s. nayo ni miezi ya Mfungo Mosi, Mfungo Pili na Mfungo Tatu. Mwenye kuazimia faridha ya Hija katika miezi hii na akaingia basi afuate vilivyo adabu zake. Katika adabu za Hija ni kuwa mwenye kuharimia ajiepushe na kuingiana na wakeze, na kufanya maasi ya kutukanana na mengineyo, kujadiliana na kubishana na Mahujaji wenziwe, na ajiepushe na kila linalo pelekea chuki na khasama ili atoke katika Ihramu yake naye hali ana hishima yake. Ajitahidi kufanya kheri na kutafuta malipwa kwa Mwenyezi Mungu kwa kutenda mema, kwani Mwenyezi Mungu ni Mwenye kuyajua hayo na ni Mwenye kulipa vitendo vyema. Na mchukue zawadi za Akhera yenu kwa kuchamngu na kufuata amri za Mwenyezi Mungu na kuyaepuka ayakatazayo. Hiyo, basi ndio zawadi bora. Na kuweni wenye kuhisi khofu ya Mwenyezi Mungu katika yote mnayo yafanya na mnayo yawacha kwa mujibu wa akili na hikima njema. Katika vitendo vyenu vyote msichanganyishe hata chembe na mambo ya pumbao au makusudio ya kidunia.
Maana: Swahili Translation - Ali Mohsin Al-Barwani. Translated by Ali Mohsen Al-Barwani Toleo 1.0.1, 2025-06-25. QuranEnc.com
Wakati wa Hija ni miezi ijulikanayo, nayo ni Mfungomosi, Mfungopili na siku kumi za Mfungotatu.Basi mwenye kujilazimisha nafsi yake kuhiji ndani ya miezi hiyo, kwa kutia nia ya kuhirimia Hija, ni haramu kwake kufanya vitenguzi vyake vya kimaneno na kivitendo. Pia ni haramu kwake kutoka kwenye twaa ya Allah Mtukufu kwa kutenda maasia, kubishana, katika Hija, kuletako hasira na chuki. Na wema wowote mnaoufanya, Allah Mtukufu Anaujua, na Atamlipa kila mtu kwa amali yake. Na jichukulieni akiba ya chakula na kinywaji kwa safari ya Hija, na akiba ya amali njema kwa nyumba ya Akhera. Hakika akiba iliyo bora zaidi ni kumuogopa Allah Mtukufu. Basi niogopeni, enyi wenye akili timamu.
Maana: Swahili Translation - Abdullah Muhammad and Nasser Khamis. Translated by Dr. Abdullah Muhammad Abu Bakr & Shaykh Nasser Khamis Toleo 1.0.1, 2026-03-12. QuranEnc.com
Kiarabu ni maandishi ya Tanzil, bila kubadilishwa. Maana ni matoleo ya wachapishaji wake, bila kubadilishwa; wahakiki wa Sabīl wenyewe bado hawajazikagua. Kiarabu: maandishi ya Uthmani ya Tanzil, toleo la 1.1. Chanzo: tanzil.net