Al-Baqara 2:196
البقرةوَأَتِمُّوا۟ ٱلْحَجَّ وَٱلْعُمْرَةَ لِلَّهِ ۚ فَإِنْ أُحْصِرْتُمْ فَمَا ٱسْتَيْسَرَ مِنَ ٱلْهَدْىِ ۖ وَلَا تَحْلِقُوا۟ رُءُوسَكُمْ حَتَّىٰ يَبْلُغَ ٱلْهَدْىُ مَحِلَّهُۥ ۚ فَمَن كَانَ مِنكُم مَّرِيضًا أَوْ بِهِۦٓ أَذًى مِّن رَّأْسِهِۦ فَفِدْيَةٌ مِّن صِيَامٍ أَوْ صَدَقَةٍ أَوْ نُسُكٍ ۚ فَإِذَآ أَمِنتُمْ فَمَن تَمَتَّعَ بِٱلْعُمْرَةِ إِلَى ٱلْحَجِّ فَمَا ٱسْتَيْسَرَ مِنَ ٱلْهَدْىِ ۚ فَمَن لَّمْ يَجِدْ فَصِيَامُ ثَلَـٰثَةِ أَيَّامٍ فِى ٱلْحَجِّ وَسَبْعَةٍ إِذَا رَجَعْتُمْ ۗ تِلْكَ عَشَرَةٌ كَامِلَةٌ ۗ ذَٰلِكَ لِمَن لَّمْ يَكُنْ أَهْلُهُۥ حَاضِرِى ٱلْمَسْجِدِ ٱلْحَرَامِ ۚ وَٱتَّقُوا۟ ٱللَّهَ وَٱعْلَمُوٓا۟ أَنَّ ٱللَّهَ شَدِيدُ ٱلْعِقَابِ
Na timizeni Hija na Umra kwa ajili ya Mwenyezi Mungu. Na ikiwa mtazuiwa, basi (chinjeni) wanyama walio wepesi kupatikana. Wala msinyoe vichwa vyenu mpaka wanyama hao wafike mahali pao pa kuchinjiwa. Na atakayekuwa mgonjwa miongoni mwenu au ana vya kumuudhi kichwani kwake, basi atoe fidia kwa kufunga saumu au kwa kutoa sadaka au kuchinja wanyama. Na mtakapokuwa na amani, basi mwenye kujistarehesha kwa kufanya Umra kisha akahiji, basi achinje mnyama aliye mwepesi kumpata. Na asiyepata, afunge siku tatu katika Hija na siku saba mtakaporudi. Hizo ni kumi kamili. Hayo ni kwa yule ambaye jamaa zake hawako karibu na Msikiti Mtakatifu. Na mcheni Mwenyezi Mungu, na jueni kwamba Mwenyezi Mungu ni Mkali wa kuadhibu.
Maana: Swahili Translation - Rowad Translation Center. Issued by the Islamic Content Service Association in Languages Toleo 1.0.5, 2025-12-17. QuranEnc.com
Na timizeni Hija na Umra kwa ajili ya Mwenyezi Mungu. Na ikiwa mkizuiwa,basi (chinjeni) wanyama walio wepesi kupatikana. Wala msinyoe vichwa vyenu mpaka wanyama hao wafike machinjoni mwao. Na atakaye kuwa mgonjwa au ana vya kumuudhi kichwani mwake basi atoe fidiya kwa kufunga au kwa kutoa sadaka au kuchinja wanyama. Na mtakapo kuwa salama, basi mwenye kujistarehesha kwa kufanya Umra kisha ndio akahiji, basi achinje mnyama aliye mwepesi kumpata. Na asiye pata, afunge siku tatu katika Hija na siku saba mtakapo rudi; hizi ni kumi kaamili. Hayo ni kwa ajili ya yule ambaye watu wake hawako karibu na Msikiti Mtakatifu. Na mcheni Mwenyezi Mungu, na jueni Mwenyezi Mungu ni Mkali wa kuadhibu. [196]
[196] Timizeni Hija na Umra kwa ajili ya Mwenyezi Mungu kwa ukamilifu, wala yasiwe makusudio yenu ya kidunia kama kutaka umaarufu na kadhaalika. Mkiharimia Hija na Umra akakuzuieni adui njiani basi mtatoka katika Ihram yenu kwa kunyoa nywele. Lakini kabla ya hayo mchinje mnyama aliye mwepesi kumpata, kama mbuzi au ngamia au ng'ombe, na kumtoa sadaka kwa masikini. Wala msinyoe mpaka mtimize haya. Mwenye kuharimia akapata maudhi katika nywele zake kwa maradhi au wadudu hapana ubaya kunyoa. Juu yake hapo atoe fidiya kwa kufunga siku tatu, au kutoa sadaka kuwalisha masikini sita chakula cha kutwa, au kuchinja mbuzi na kumtoa sadaka kwa masikini. Na ikiwa mpo katika amani na salama na hakukutokeleeni adui njiani, na mkakusudia Hija na Umra, na mkajistarehesha kwa kufanya Umra kwanza mpaka ufike wakati wa Hija ndio mharimie, basi inakupaseni kuchinja mbuzi kwa ajili ya masikini na mafakiri wa Makka. Asiye pata mbuzi au hamiliki bei yake afunge siku tatu hapo Makka, na siku saba akisha rejea kwao. Haya ni kwa aliye kuwa hana watu wake Makka. Kwa mwenye watu wake Makka hapana kitu akijistarehesha.
Maana: Swahili Translation - Ali Mohsin Al-Barwani. Translated by Ali Mohsen Al-Barwani Toleo 1.0.1, 2025-06-25. QuranEnc.com
Na tekelezeni Hija na Umra ziwe zimekamilika, zimetakasika na kukusudiwa Allah Mtukufu. Na iwapo kitazuia, kwenda kuzikamilisha baada ya kuzihirimia, kizuizi chochote, kama adui na ugonjwa, lililo wajibu kwenu ni kuchinja kitakacho kuwa chepesi kwenu miongoni mwa ngamia, ng’ombe, mbuzi au kondoo, hali ya kujikurubisha kwa Allah Mtukufu, ili mpate kutoka katika ihramu zenu kwa kunyoa nywele za kichwa au kuzipunguza.Wala msinyoe vichwa vyenu, mkiwa mumezuiwa, mpaka mwenye kuzuiwa amchinje mnyama wake pale pahali alipozuiwa kisha ajitoe kwenye ihramu yake kama alivyochinja Mtume(sala na salamu zimshukie) hapo Hudaibiya kisha akanyoa kichwa chake. Na asiyekuwa yule aliyezuiwa, hatachinja mnyama wake mpaka afike ndani ya eneo tukufu la Maka, ambapo ndipo pahali pake, siku ya idi ambayo ni siku ya kumi na siku zifuatazo za Tashrîq. Na ambaye kati yenu atakuwa mngonjwa au ana udhia katika kichwa chake akawa anahitajia kunyoa, naye yuko kwenye ihramu, basi atanyoa na ni juu yake atoe fidia: afunge siku tatu au awape sadaka masikini sita, kila mmoja nusu pishi ya chakula, au achinje mbuzi au kondoo awape mafukara wa eneo tukufu la Maka. Na pindi mtakapo kuwa kwenye hali ya amani na afya, basi atakaye kujistarehesha kwa kufanya Umra ndani ya Hija, nako ni kuihalalishia mambo alioharamhshiwa kwa sababu ya ihramu baada ya kumaliza Umra yake, inampasa kuchinja kiwezekanacho katika wanyama. Na yule aliyekosa mnyama wa kuchinja, itamlazimu afunge siku tatu ndani ya miezi ya Hija na siku saba mtakapo kumaliza amali za Hija na mkarudi kwenu; hizo ni siku kumi kamili, hapana budi kuzifunga.Mnyama huyo wa kuchinjwa, na yale yaliyopasa juu yake ya kufunga, ni kwa yule ambaye watu wake si wakazi wa ardhi tukufu ya Ḥaram. Na muogopeni Allah Mtukufu na mujilazimishe kuzitekeleza amri Zake na kujiepusha na Makatazo Yake, na mjue kwamba Allah Mtukufu ni mkali wa mateso kwa yule aendaye kinyume na amri Zake na kufanya Aliyoyakemea.
Maana: Swahili Translation - Abdullah Muhammad and Nasser Khamis. Translated by Dr. Abdullah Muhammad Abu Bakr & Shaykh Nasser Khamis Toleo 1.0.1, 2026-03-12. QuranEnc.com
Kiarabu ni maandishi ya Tanzil, bila kubadilishwa. Maana ni matoleo ya wachapishaji wake, bila kubadilishwa; wahakiki wa Sabīl wenyewe bado hawajazikagua. Kiarabu: maandishi ya Uthmani ya Tanzil, toleo la 1.1. Chanzo: tanzil.net