Ruka hadi kwenye maudhui
Sura ya 2 · Aya ya 195

Al-Baqara 2:195

البقرة

وَأَنفِقُوا۟ فِى سَبِيلِ ٱللَّهِ وَلَا تُلْقُوا۟ بِأَيْدِيكُمْ إِلَى ٱلتَّهْلُكَةِ ۛ وَأَحْسِنُوٓا۟ ۛ إِنَّ ٱللَّهَ يُحِبُّ ٱلْمُحْسِنِينَ

Maana

Na toeni katika njia ya Mwenyezi Mungu, wala msijitupe katika maangamivu kwa mikono yenu. Na fanyeni wema. Hakika, Mwenyezi Mungu huwapenda wanaofanya wema.

Maana: Swahili Translation - Rowad Translation Center. Issued by the Islamic Content Service Association in Languages Toleo 1.0.5, 2025-12-17. QuranEnc.com

Maana

Na toeni katika njia ya Mwenyezi Mungu, wala msijitie kwa mikono yenu katika maangamizo. Na fanyeni wema. Hakika Mwenyezi Mungu huwapenda wafanyao wema. [195]

[195] Kupambana na makafiri kunahitaji kutoa roho kama ilivyo kutoa mali. Basi toeni kwa kuandaa vita, na jueni kuwa kupigana na hawa ni kupigana katika Njia ya Mwenyezi Mungu. Basi msikae tu. Toeni mali kwa ajili yake, kwani mkitofanya na mkafanya ubakhili adui atakupandeni na atakudhilini. Hapo itakuwa kama mlio jitokomeza wenyewe kwenye maangamio. Tendeni lilio kuwajibikieni kwa uzuri na vilivyo, kwani Mwenyezi Mungu hupenda anapo fanya jambo mtu alifanye vizuri. Aya 190 mpaka 195 zinaeleza sharia ya vita katika Uislamu. Nazo zinaeleza kwa matamshi yalio wazi haya yafuatayo: 1. Ruhusa ya kupigana imetolewa kwa ajili ya kujilinda na uvamizi wa vita wa vitendo khasa, au zikidhihiri dalili kuwa maadui wanataka vita. Vita havikulazimishwa kwa ajili ya vita wala kwa sababu ya kutaka kuwasilimisha watu kwa kuwauwa na kuwapiga vita. 2. Kunakatazwa kuvamia au kuanza uadui kwa njia yoyote ile. Basi hapana ruhusa kufanyiwa uadui asiye pigana, wala hapana ruhusa kuvuka mipaka ya uadui wakati wa vita: basi hauliwi asiye chukua silaha, wala hakhusiani na vita bali ni mwenye kukumbwa tu na vita. Wala hauliwi mwenye kusalimu amri na akatupa silaha. Wala hapana ruhusa kuwavunjia watu nyumba zao, huko ni kupita mpaka. 3. Mzingatie fadhila iliyo onyeshwa kwa kuamrishwa kuchamngu. Basi msivunje heshima ya wanawake kuwanajisi, hata washirikina wakifanya hayo. Wala msiwakatekate walio uwawa hata ikiwa makafiri wakiwafanyia hayo Waumini. Washirikina walimfanyia hayo Bwana wa Mashahidi, Hamza, wala Mtume s.a.w. hakutoa ruhusa kumfanyia hayo maiti yeyote, bali alikataza akasema:"Tahadharini msiwakatekate maiti". 4. Vita vinakwisha wakiacha washirikina kuwafitini Waumini katika Dini yao, na Dini inakuwa inataka akili na nyoyo zimwelekee Mwenyezi Mungu kwa uhuru. 5. Hapana vita katika mwezi mtukufu, nayo ni miezi ya Hija na Umra. Ikiwa washirikina watapigana katika miezi hiyo, basi Waumini nao yawapasa wapigane. 6. Kuacha kutoka kwenda pigana na maadui wanauwa pasina nasi kupigana nao ni kuipoteza kheri na wema. Kwa haya inadhihiri kuwa vita vya Islamu vina fadhila katika sababu zinazo pelekea kuanza kwake, na vina uadilifu katika kuviendesha. Viwapi hivi na vita vya mataifa mengine ya zamani na ya sasa! Vita vyao hao ni vya uchafu, na vita vya Islamu ni vya Haki na vyenye fadhila.

Maana: Swahili Translation - Ali Mohsin Al-Barwani. Translated by Ali Mohsen Al-Barwani Toleo 1.0.1, 2025-06-25. QuranEnc.com

Maana

Na endeleeni, enyi Waumini, kutoa mali kwa kuinusuru dini ya Allah Mtukufu na kupigana jihadi katika njia yake. Wala msiziingize nafsi zenu kwenye maangamivu kwa kuacha jihadi katika njia ya Allah Mtukufu na kuacha kutoa katika njia Yake. Na fanyeni wema katika kutoa na kutii, na mzifanye amali zenu zote ni zenye kutakasika kwa kukusudiwa Allah Mtukufu. Kwa hakika Allah Mtukufu Anawapenda watu wenye kutakasa nia na kufanya wema.

Maana: Swahili Translation - Abdullah Muhammad and Nasser Khamis. Translated by Dr. Abdullah Muhammad Abu Bakr & Shaykh Nasser Khamis Toleo 1.0.1, 2026-03-12. QuranEnc.com

Al-Baqara

Kiarabu ni maandishi ya Tanzil, bila kubadilishwa. Maana ni matoleo ya wachapishaji wake, bila kubadilishwa; wahakiki wa Sabīl wenyewe bado hawajazikagua. Kiarabu: maandishi ya Uthmani ya Tanzil, toleo la 1.1. Chanzo: tanzil.net