Ruka hadi kwenye maudhui
Sura ya 2 · Aya ya 187

Al-Baqara 2:187

البقرة

أُحِلَّ لَكُمْ لَيْلَةَ ٱلصِّيَامِ ٱلرَّفَثُ إِلَىٰ نِسَآئِكُمْ ۚ هُنَّ لِبَاسٌ لَّكُمْ وَأَنتُمْ لِبَاسٌ لَّهُنَّ ۗ عَلِمَ ٱللَّهُ أَنَّكُمْ كُنتُمْ تَخْتَانُونَ أَنفُسَكُمْ فَتَابَ عَلَيْكُمْ وَعَفَا عَنكُمْ ۖ فَٱلْـَٔـٰنَ بَـٰشِرُوهُنَّ وَٱبْتَغُوا۟ مَا كَتَبَ ٱللَّهُ لَكُمْ ۚ وَكُلُوا۟ وَٱشْرَبُوا۟ حَتَّىٰ يَتَبَيَّنَ لَكُمُ ٱلْخَيْطُ ٱلْأَبْيَضُ مِنَ ٱلْخَيْطِ ٱلْأَسْوَدِ مِنَ ٱلْفَجْرِ ۖ ثُمَّ أَتِمُّوا۟ ٱلصِّيَامَ إِلَى ٱلَّيْلِ ۚ وَلَا تُبَـٰشِرُوهُنَّ وَأَنتُمْ عَـٰكِفُونَ فِى ٱلْمَسَـٰجِدِ ۗ تِلْكَ حُدُودُ ٱللَّهِ فَلَا تَقْرَبُوهَا ۗ كَذَٰلِكَ يُبَيِّنُ ٱللَّهُ ءَايَـٰتِهِۦ لِلنَّاسِ لَعَلَّهُمْ يَتَّقُونَ

Maana

Mmehalalishiwa usiku wa Saumu kuingiliana na wake zenu. Wao ni vazi kwenu, na nyinyi ni vazi kwao. Mwenyezi Mungu alikwishajua kwamba mlikuwa mkizihini nafsi zenu. Kwa hivyo amewakubalia toba yenu na amewasamehe. Basi sasa changanyikeni nao na tafuteni kile alichowaandikia Mwenyezi Mungu. Na kuleni na kunyweni mpaka uwabainikie weupe wa alfajiri kutokana na weusi wa usiku. Kisha timizeni Saumu mpaka usiku. Wala msichanganyike nao hali ya kuwa mmekaa Itikafu msikitini. Hiyo ni mipaka ya Mwenyezi Mungu, basi msiikaribie. Hivyo ndivyo Mwenyezi Mungu anavyowabainishia Aya (Ishara) zake watu ili wapate kumcha.

Maana: Swahili Translation - Rowad Translation Center. Issued by the Islamic Content Service Association in Languages Toleo 1.0.5, 2025-12-17. QuranEnc.com

Maana

Mmehalalishiwa usiku wa Saumu kuingiliana na wake zenu. Wao ni vazi kwenu, na nyinyi ni vazi kwao. Mwenyezi Mungu anajua kwamba mlikuwa mkizikhini nafsi zenu. Kwa hivyo amekukubalieni toba yenu na amekusameheni. Basi sasa changanyikeni nao na takeni aliyo kuandikieni Mwenyezi Mungu. Na kuleni na kunyweni mpaka ubainike kwenu weupe wa alfajiri katika weusi wa usiku. Kisha timizeni Saumu mpaka usiku. Wala msichanganyike nao, na hali mnakaa Itikafu msikitini. Hiyo ni mipaka ya Mwenyezi Mungu, basi msiikaribie. Namna hivi Mwenyezi Mungu anabainisha Ishara zake kwa watu ili wapate kumcha. [187]

[187] Mwenyezi Mungu amekuhalalishieni usiku wa kufunga kuingiana na wake zenu, na wao kuchanganyika nanyi katika maisha na katika malazi. Ilikuwa ni mazito kwenu kujitenga nao, na sasa mmepunguziwa hizo taabu. Mwenyezi Mungu anajua kuwa mlikuwa mkijipunguzia starehe ya nafsi zenu na mkijidhulumu kwa kujizuia msiingiane na wake zenu hata usiku wa Ramadhani. Sasa amekusameheni na kukupunguzieni mikazo. Sasa basi msione vibaya kuchanganyika nao, na stareheni kwa aliyo kuhalalishieni Mwenyezi Mungu, na kuleni na mnywe usiku wa Ramadhani mpaka mwone mwangaza wa alfajiri unapo tokeza kutokana na kiza cha usiku. Hapo tena fungeni na mtimize Saumu mpaka linapo kuchwa jua. Na ilivyo kuwa Saumu ni katika ibada zinazo taka mtu kujiepusha na matamanio ya roho na kuingiana na wanawake wakati wa mchana, basi kadhaalika katika ibada ya kukaa Itikafu msikitini inahitaji kujitenga na kuacha kustarehe na wake zenu wakati huo mnapo kuwapo katika Itikafu. Na haya ya sharia za Saumu na Itikafu alizo kuwekeeni Mwenyezi Mungu yashikeni baraabara msikaribie kuyavunja. Na Mwenyezi Mungu ameyaweka wazi haya kwa watu kwa namna hii ili wapate kuyaogopa na waepukane na matokeo yake.

Maana: Swahili Translation - Ali Mohsin Al-Barwani. Translated by Ali Mohsen Al-Barwani Toleo 1.0.1, 2025-06-25. QuranEnc.com

Maana

Amewahalalishia Allah Mtukufu masiku ya mwezi wa Ramadhani kuwaingilia wake zenu. Wao ni sitara na hifadhi kwenu, na nyinyi ni sitara na hifadhi kwao. Anajua Allah Mtukufu kwamba nyinyi mulikuwa mkizidhiki nafsi zenu kwa kuenda kinyume na yale ambayo Allah Mtukufu Aliyaharimisha kwenu ya kuwaingilia wanawake baada ya Isha katika masiku ya kufunga- hilo lilikuwa mwanzo wa Uislamu-, Allah Mtukufu Alikubali toba yenu na Akawatolea nafasi kwa hili jambo. Basi sasa waingilieni na mtafute kile Alichowakadiria Allah Mtukufu, miongoni mwa watoto, na kuleni na kunyweni mpaka ujitokeze kwenu mwangaza wa asubuhi utengane na weusi wa usiku kwa kujitokeza alfajiri ya kweli. Kisha kamilisheni kufunga kwa kujizuia na venye kutangua mpaka kuingia usiku kwa kuchwa jua. Wala musiwaingilie wake zenu, au kufanya kitu cha kusababisha kuwaingilia, iwapo muko kwenye itikafu misikitini, sababu hilo laharibu itikafu- nako ni kukaa msikitini kwa muda maalumu kwa nia ya kujikurubisha kwa Allah Mtukufu-. Hukumu hizo, ambazo Allah Mtukufu Amezifanya ni Sheria kwenu, ndiyo mipaka Yake itenganishayo kati ya halali na haramu. Basi msiikaribie, ili msije mkaingia katika haramu. Kwa mfano wa ubainifu huu ulio wazi, Allah Mtukufu Anazifafanua aya Zake na hukumu Zake kwa watu, ili wamche na kumuogopa.

Maana: Swahili Translation - Abdullah Muhammad and Nasser Khamis. Translated by Dr. Abdullah Muhammad Abu Bakr & Shaykh Nasser Khamis Toleo 1.0.1, 2026-03-12. QuranEnc.com

Al-Baqara

Kiarabu ni maandishi ya Tanzil, bila kubadilishwa. Maana ni matoleo ya wachapishaji wake, bila kubadilishwa; wahakiki wa Sabīl wenyewe bado hawajazikagua. Kiarabu: maandishi ya Uthmani ya Tanzil, toleo la 1.1. Chanzo: tanzil.net