Ruka hadi kwenye maudhui
Sura ya 2 · Aya ya 178

Al-Baqara 2:178

البقرة

يَـٰٓأَيُّهَا ٱلَّذِينَ ءَامَنُوا۟ كُتِبَ عَلَيْكُمُ ٱلْقِصَاصُ فِى ٱلْقَتْلَى ۖ ٱلْحُرُّ بِٱلْحُرِّ وَٱلْعَبْدُ بِٱلْعَبْدِ وَٱلْأُنثَىٰ بِٱلْأُنثَىٰ ۚ فَمَنْ عُفِىَ لَهُۥ مِنْ أَخِيهِ شَىْءٌ فَٱتِّبَاعٌۢ بِٱلْمَعْرُوفِ وَأَدَآءٌ إِلَيْهِ بِإِحْسَـٰنٍ ۗ ذَٰلِكَ تَخْفِيفٌ مِّن رَّبِّكُمْ وَرَحْمَةٌ ۗ فَمَنِ ٱعْتَدَىٰ بَعْدَ ذَٰلِكَ فَلَهُۥ عَذَابٌ أَلِيمٌ

Maana

Enyi mlioamini! Mmepewa ruhusa kulipa kisasi katika waliouawa - muungwana kwa muungwana, na mtumwa kwa mtumwa, na mwanamke kwa mwanamke. Na anayesamehewa na ndugu yake chochote, basi ashikwe kulipa kwa wema, na yeye alipe kwa ihsani. Huko ni kupunguziwa kulikotokana na Mola wenu Mlezi, na ni rehema. Na atakayevuka mipaka baada ya haya, basi yeye atapata adhabu chungu.

Maana: Swahili Translation - Rowad Translation Center. Issued by the Islamic Content Service Association in Languages Toleo 1.0.5, 2025-12-17. QuranEnc.com

Maana

Enyi mlio amini! Mmepewa ruhusa kulipa kisasi katika walio uwawa - muungwana kwa muungwana, na mtumwa kwa mtumwa, na mwanamke kwa mwanamke. Na anaye samehewa na ndugu yake chochote basi ashikwe kulipa kwa wema, na yeye alipe kwa ihsani. Huko ni kupunguziwa kuliko tokana na Mola wenu Mlezi, na ni rehema. Na atakaye vuka mipaka baada ya haya, basi yeye atapata adhabu chungu. [178]

[178] Katika Sharia tulizo walazimisha Waumini ni hukumu za mauwaji ya makusudi. Tumewaandikia kisasi kwa mauwaji. Na wala msichukulie dhulma za kijahiliya , walipo kuwa wakimuuwa muungwana asiye uwa kwa ajili ya mtumwa, na wakimuuwa mwanamume asiye uwa kwa ajili ya mwanamke, na mkuu asiye uwa badala ya mwenginewe aliye uwa, akaachiliwa aliye uwa khasa. (Kwa kila ukoo kujiona bora). Yatakikana yule aliye uwa auwawe yeye, akiwa ni muungwana, au mtumwa, au mwanamke. Msingi wa sharia ya kisasi ni kuondoa kufanyiana uadui kwa kumuuwa yule yule aliye uwa ili kuuzima moto wa kulipizana na kuondoa uadui. Walio uliwa mtu wao wakiacha kisasi, wakapendelea kuwasamehe wenzao, watakuwa na haki ya kupewa fidia kwa maiti wao. Na wao inatakikana wawe wasemehevu bila ya kumkahirisha aliye uwa. Na juu ya mwenye kuuwa alipe fidia bila ya kujikurupusha. Katika hukumu ya mauwaji kama tulivyo ilazimisha pana wepesi kwa Waumini ukilinganisha na hukumu ya Taurati inayo lazimisha kisasi tu, na kama ilivyo kuwa ni rehema ukilinganisha na watakavyo wenginewe kuwa muuwaji aachiliwe bure bila ya kumtaaradhi. Basi mwenye kuivuka hukumu hii baada ya hayo atapata adhabu chungu duniani na Akhera. Waarabu zama za jahiliya walikuwa hawafanyi usawa baina ya watukufu na wanyonge. Akiuliwa mwongozi hawatosheki na kumuuwa muuwaji bali huyo huachwa akenda kulipizwa kisasi kwa mwongozi wa kabila ya muuwaji. Kwao roho si sawa, na damu si sawa. Uislamu haukukubali haya, lakini ukapasisha Kisasi, roho kwa roho, mwenye kuuwa huuwawa. Muuwaji yeyote awaye atauliwa akiwa muungwana, mtumwa au mwanamke. Haya ni kwa ajili ya usawa katika damu; hapana mwenye damu tukufu na damu isiyo tukufu. Na inafahamika kwa ishara kuwa nafsi kwa nafsi. Na hii ni sharia ya milele, ilikuwako katika Taurat, na Injil na Qur'ani. Na Mwenyezi Mungu Mtukufu amesema: "Na tuliwaandikia kuwa nafsi kwa nafsi..." (taz. sura Almaida ). Na Mtume s.a.w. amesema: "Damu za Waislamu ni sawa." Na amesema: "Nafsi kwa nafsi". Zingatia: Uislamu kwa sharia ya kisasi ina nadhari nyengine, sio kama kanuni za kutungwa. Imewapa wenye kuuliwa mtu wao haki ya kutaka muuwaji auwawe, kuondoa fitna na umwagaji wa damu mkubwa. Imewapa haki ya kusamehe au kulipwa kisasi, wala haizuilii serikali kumfedhehi aliye uwa ikiona hivyo ni maslaha. Uislamu hauzingatii sababu ya kuuwa, kwani mwenye kuuwa amedhulumu hata ikiwa sababu gani. Na huenda ukitafuta sababu akaonewa huruma mkosa, na kumpuuza mkoswa. Na hayo hupelekea mchafuko wa watu kuchukua kisasi mkononi mwao, na kuzalikana makosa juu ya makosa ya kuuwa, kwa kutoridhika wale walio uliwa mtu wao. Nadharia hii ya Kiislamu sasa inadurusiwa katika vyuo vikuu vya Ulaya.

Maana: Swahili Translation - Ali Mohsin Al-Barwani. Translated by Ali Mohsen Al-Barwani Toleo 1.0.1, 2025-06-25. QuranEnc.com

Maana

Enyi mliomuamini Allah Mtukufu na Mtume Wake na mkafanya vitendo vinavyoambatana na Sheria ya Allah Mtukufu Alioifanya faradhi kwenu kwamba mlipize kisasi kwa muuaji aliyeua kwa kukusudia, kwa sharti ya kufanya usawa na kufananisha malipo: auawe muungwana kwa kumuua mfano wake, na mtumwa kwa mfano wake, na mwanamke kwa mfano wake. Na yule atakayesamehewa na msimamizi wa aliyeuawa kwa kumuondolea kisasi na kutosheka kwa kuchukua dia, nayo ni kiwango cha mali maalumu akitoacho mhalifu kikiwa ni badali ya kusamehewa, ni juu ya pande mbili zijilazimishe tabia njema: yule msimamizi adai diya yake bila kutumia nguvu, na yule muuaji ampatiye haki yake kwa wema bila kuchelewesha wala kupunguza. Msamaha huo, pamoja na kupokea hiyo dia, ni masahilisho ya Mola wenu na ni huruma kwenu kwa ule usahali na kujinufaisha. Hivyo basi,mwenye kumuua muuaji baada ya msamaha na kupokea dia, atapata adhabu kali ya kuuawa kwa njia ya kisasi duniani au kutiwa Motoni Akhera.

Maana: Swahili Translation - Abdullah Muhammad and Nasser Khamis. Translated by Dr. Abdullah Muhammad Abu Bakr & Shaykh Nasser Khamis Toleo 1.0.1, 2026-03-12. QuranEnc.com

Al-Baqara

Kiarabu ni maandishi ya Tanzil, bila kubadilishwa. Maana ni matoleo ya wachapishaji wake, bila kubadilishwa; wahakiki wa Sabīl wenyewe bado hawajazikagua. Kiarabu: maandishi ya Uthmani ya Tanzil, toleo la 1.1. Chanzo: tanzil.net