Ruka hadi kwenye maudhui
Sura ya 2 · Aya ya 177

Al-Baqara 2:177

البقرة

لَّيْسَ ٱلْبِرَّ أَن تُوَلُّوا۟ وُجُوهَكُمْ قِبَلَ ٱلْمَشْرِقِ وَٱلْمَغْرِبِ وَلَـٰكِنَّ ٱلْبِرَّ مَنْ ءَامَنَ بِٱللَّهِ وَٱلْيَوْمِ ٱلْـَٔاخِرِ وَٱلْمَلَـٰٓئِكَةِ وَٱلْكِتَـٰبِ وَٱلنَّبِيِّـۧنَ وَءَاتَى ٱلْمَالَ عَلَىٰ حُبِّهِۦ ذَوِى ٱلْقُرْبَىٰ وَٱلْيَتَـٰمَىٰ وَٱلْمَسَـٰكِينَ وَٱبْنَ ٱلسَّبِيلِ وَٱلسَّآئِلِينَ وَفِى ٱلرِّقَابِ وَأَقَامَ ٱلصَّلَوٰةَ وَءَاتَى ٱلزَّكَوٰةَ وَٱلْمُوفُونَ بِعَهْدِهِمْ إِذَا عَـٰهَدُوا۟ ۖ وَٱلصَّـٰبِرِينَ فِى ٱلْبَأْسَآءِ وَٱلضَّرَّآءِ وَحِينَ ٱلْبَأْسِ ۗ أُو۟لَـٰٓئِكَ ٱلَّذِينَ صَدَقُوا۟ ۖ وَأُو۟لَـٰٓئِكَ هُمُ ٱلْمُتَّقُونَ

Maana

Siyo wema kuwa mnaelekeza nyuso zenu upande wa mashariki na magharibi. Bali wema ni wa anayemuamini Mwenyezi Mungu na Siku ya Mwisho na Malaika na Kitabu na Manabii. Na anawapa mali - licha ya kuipenda - jamaa na mayatima na masikini na wasafiri, na waombao, na katika ukombozi. Na akawa anashika Swala, na akatoa Zaka, na wanaotimiza agano lao wanapoahidi, na wanaovumilia katika shida na dhara na wakati wa vita. Hao ndio walio sadikisha, na hao ndio wacha Mungu.

Maana: Swahili Translation - Rowad Translation Center. Issued by the Islamic Content Service Association in Languages Toleo 1.0.5, 2025-12-17. QuranEnc.com

Maana

Sio wema kuwa mnaelekeza nyuso zenu upande wa mashariki na magharibi. Bali wema ni wa anaye muamini Mwenyezi Mungu na Siku ya Mwisho na Malaika na Kitabu na Manabii, na anawapa mali, kwa kupenda kwake, jamaa na mayatima na masikini na wasafiri, na waombao, na katika ugombozi, na akawa anashika Swala, na akatoa Zaka, na wanao timiza ahadi yao wanapo ahidi, na wanao vumilia katika shida na dhara na wakati wa vita; hao ndio walio sadikisha, na hao ndio wajilindao. [177]

[177] Watu wamekithirisha maneno juu ya Kibla kama kwamba wema wote ni hayo tu. Hivi sivyo. Kuelekea upande fulani, mashariki au magharibi, sio msingi wa Dini na kupata kheri, lakini kupata wema ni mambo kadhaa wa kadhaa, baadhi yake ni nguzo za itikadi sahihi, na baadhi yake ni katika misingi ya tabia njema na ibada. La kwanza: kumuamini Mwenyezi Mungu, na Siku ya kufufuliwa na kukusanywa na kuhisabiwa na yatakayo tokea Siku ya Kiyama; na kuamini Malaika, na Vitabu vilivyo teremka kwa Manabii, na kuwaamini wenyewe Manabii. Na pili: kutoa mali kwa kupenda na kuridhia nafsi kuwapa mafakiri katika jamaa, na mayatima, na wenye shida ya haja, na wasafiri walio katikiwa safari yao wasipate cha kuwafikishia wendako, na walio lazimika kuomba kwa haja walio nayo, na kukomboa watumwa. ( Walio fungwa na kutawaliwa na dhaalimu ni watumwa pia. )Tatu: kushika Swala. Lane: kutoa Zaka iliyo lazimishwa. La tano: kutimiza ahadi bilhali wal maal. La sita: kustahamili maudhi yanayo teremkia roho na mali, mnapo pambana na adui zama za vita. Basi wenye kukusanya imani hizi na vitendo hivi vya kheri ndio walio sadikisha Imani yao, na wao ndio wanao jilinda na ukafiri na mambo machafu na wakayaepuka.

Maana: Swahili Translation - Ali Mohsin Al-Barwani. Translated by Ali Mohsen Al-Barwani Toleo 1.0.1, 2025-06-25. QuranEnc.com

Maana

Hapana kheri, mbele ya Allah Mtukufu, kuelekea kwenye Swala upande wa mashariki na magharibi, iwapo hilo halitokamani na amri ya Allah Mtukufu na sheria Yake. Hakika kheri yote iko katika imani ya aliyemuamini Allah Mtukufu na akamkubali kuwa Ndiye muabudiwa, Peke Yake, Hana mshirika, na akaiamini Siku ya kufufuliwa na Malipo, na akawaamini Malaika wote na vitabu vyote vilivyoteremshwa, na Mitume wote bila kubagua, na akatoa mali yake kwa hiyari yake, pamoja na kuwa anayapenda sana, kuwapa jamaa zake na mayatima wenye uhitaji waliofiliwa na wazazi wao hali wao wako chini ya umri wa kubaleghe, na akawapa masikini ambao ufukara umewaelemea, na wasafiri wanaohitaji walio mbali na watu wao na mali yao, na waombaji ambao imekuwa ni dharura kwao kuomba kwa uhitaji wao mkubwa, na akatoa mali yake katika kuwakomboa watumwa na mateka, na akasimamisha Swala na akatoa zaka za faradhi, na wale wenye kutekeleza ahadi, na mwenye kusubiri katika hali ya ufukara wake na ugonjwa wake na katika vita vikali. Hao wenye kusifika kwa sifa hizo, ndio waliokuwa wakweli katika imani zao, na wao ndio waliojikinga mateso ya Allah Mtukufu wakajiepusha na vitendo vya kumuasi.

Maana: Swahili Translation - Abdullah Muhammad and Nasser Khamis. Translated by Dr. Abdullah Muhammad Abu Bakr & Shaykh Nasser Khamis Toleo 1.0.1, 2026-03-12. QuranEnc.com

Al-Baqara

Kiarabu ni maandishi ya Tanzil, bila kubadilishwa. Maana ni matoleo ya wachapishaji wake, bila kubadilishwa; wahakiki wa Sabīl wenyewe bado hawajazikagua. Kiarabu: maandishi ya Uthmani ya Tanzil, toleo la 1.1. Chanzo: tanzil.net