Al-Baqara 2:164
البقرةإِنَّ فِى خَلْقِ ٱلسَّمَـٰوَٰتِ وَٱلْأَرْضِ وَٱخْتِلَـٰفِ ٱلَّيْلِ وَٱلنَّهَارِ وَٱلْفُلْكِ ٱلَّتِى تَجْرِى فِى ٱلْبَحْرِ بِمَا يَنفَعُ ٱلنَّاسَ وَمَآ أَنزَلَ ٱللَّهُ مِنَ ٱلسَّمَآءِ مِن مَّآءٍ فَأَحْيَا بِهِ ٱلْأَرْضَ بَعْدَ مَوْتِهَا وَبَثَّ فِيهَا مِن كُلِّ دَآبَّةٍ وَتَصْرِيفِ ٱلرِّيَـٰحِ وَٱلسَّحَابِ ٱلْمُسَخَّرِ بَيْنَ ٱلسَّمَآءِ وَٱلْأَرْضِ لَـَٔايَـٰتٍ لِّقَوْمٍ يَعْقِلُونَ
Hakika, katika kuumbwa kwa mbingu na ardhi, na kukhitalifiana usiku na mchana. Na marikebu ambazo hupita baharini kwa viwafaavyo watu, na maji anayoyateremsha Mwenyezi Mungu kutoka mbinguni, na kwa hayo, akaihuisha ardhi baada ya kufa kwake, na akaeneza humo kila aina ya wanyama; na katika mabadiliko ya pepo na mawingu yanayoamrishwa kupita baina ya mbingu na ardhi, bila shaka zimo Ishara kwa watu watumiao akili.
Maana: Swahili Translation - Rowad Translation Center. Issued by the Islamic Content Service Association in Languages Toleo 1.0.5, 2025-12-17. QuranEnc.com
Hakika katika kuumbwa kwa mbingu na ardhi, na kukhitalifiana usiku na mchana, na marikebu ambazo hupita baharini kwa viwafaavyo watu, na maji anayo yateremsha Mwenyezi Mungu kutoka mbinguni, na kwa hayo akaihuisha ardhi baada ya kufa kwake, na akaeneza humo kila aina ya wanyama; na katika mabadiliko ya pepo, na mawingu yanayo amrishwa kupita baina ya mbingu na ardhi, bila shaka zimo Ishara kwa watu wanao zingatia. [164]
[164] Na zipo dalili nyingi na Ishara kwa kila mwenye akili juu ya kuwapo kwake na Ungu wake. Miongoni mwa hizo ni hizi mbingu mzionazo zinazo pitiwa na sayari kwa nidhamu bila ya kuzahamiana wala kugongana, zikiuletea ulimwengu huu joto na nuru. Na pia hii dunia yenye bara na bahari, na kupishana usiku na mchana, pamoja na manufaa yake. Katika Ishara na dalili hizo ni kuzingatia marikebu zipitazo baharini zikibeba watu na vifao vyao, na hapana aziendeshao hizo ila Mwenyezi Mungu. Ni Yeye ndiye anaye zituma pepo zinazo leta mvua. Na mvua ikateremka ikahuisha wanyama na ikanywesha ardhi na mimea. Na hizo pepo kwa mivumo yake ya kila namna, na mawingu yaliyo tundikwa baina ya mbingu na ardhi: Jee, yote haya yamesimama kwa uangalifu namna hii na kwa hukumu kama hizi wenyewe tu? Au vimeundwa na Mwenye Kujua Mwenye Uwezo?
Maana: Swahili Translation - Ali Mohsin Al-Barwani. Translated by Ali Mohsen Al-Barwani Toleo 1.0.1, 2025-06-25. QuranEnc.com
Hakika, katika kuumba mbingu kwa kuzifanya ziinuke juu na ziwe kunjufu, na ardhi kwa majabali yake, mabonde yake na bahari zake, na katika kutafautiana usiku na mchana kwa urefu na ufupi, giza na muangaza, na kuandamana kwao kwa kila mmoja kukaa pahali pa mwingine, na katika majahazi yanayopita baharini, yanayobeba vitu vinavyowanufaisha watu, na katika maji ya mvua Aliyoyateremsha Allah Mtukufu kutoka mbinguni, Akaipa uhai ardhi kwa maji hayo ikawa rangi ya kijani yenye kupendeza baada ya kuwa kavu isiyokuwa na mimea, na vile Alivyoeneza Allah Mtukufu humo kila kitambaacho juu ya ardhi hiyo, na katika yale Aliyowaneemesha kwayo ya kuugeuza upepo na kuuelekeza, na katika mawingu yanayopelekwa baina ya mbingu na ardhi, hakika, katika dalili zote hizo zilizopita, pana alama za upweke wa Allah Mtukufu na ukubwa wa neema Zake kwa watu wanaoelewa sehemu za hoja na wanaozifahamu dalili za Allah Mtukufu juu ya upweke Wake na kustahiki Kwake Peke Yake kuabudiwa.
Maana: Swahili Translation - Abdullah Muhammad and Nasser Khamis. Translated by Dr. Abdullah Muhammad Abu Bakr & Shaykh Nasser Khamis Toleo 1.0.1, 2026-03-12. QuranEnc.com
Kiarabu ni maandishi ya Tanzil, bila kubadilishwa. Maana ni matoleo ya wachapishaji wake, bila kubadilishwa; wahakiki wa Sabīl wenyewe bado hawajazikagua. Kiarabu: maandishi ya Uthmani ya Tanzil, toleo la 1.1. Chanzo: tanzil.net