Al-Baqara 2:145
البقرةوَلَئِنْ أَتَيْتَ ٱلَّذِينَ أُوتُوا۟ ٱلْكِتَـٰبَ بِكُلِّ ءَايَةٍ مَّا تَبِعُوا۟ قِبْلَتَكَ ۚ وَمَآ أَنتَ بِتَابِعٍ قِبْلَتَهُمْ ۚ وَمَا بَعْضُهُم بِتَابِعٍ قِبْلَةَ بَعْضٍ ۚ وَلَئِنِ ٱتَّبَعْتَ أَهْوَآءَهُم مِّنۢ بَعْدِ مَا جَآءَكَ مِنَ ٱلْعِلْمِ ۙ إِنَّكَ إِذًا لَّمِنَ ٱلظَّـٰلِمِينَ
Na hata ukiwaletea hao waliopewa Kitabu hoja za kila namna, hawatafuata Kibla chako. Wala wewe hutafuata kibla chao. Wala baadhi yao hawatafuata kibla cha wengineo. Na kama ukiyafuata matamanio yao baada ya kile kilichokufikia katika elimu, wewe kwa hakika hapo utakuwa miongoni mwa wenye kudhulumu.
Maana: Swahili Translation - Rowad Translation Center. Issued by the Islamic Content Service Association in Languages Toleo 1.0.5, 2025-12-17. QuranEnc.com
Na hao walio pewa Kitabu, hata ukiwaletea hoja za kila namna, hawatafuata Kibla chako; wala wewe hutafuata kibla chao, wala baadhi yao hawatafuata kibla cha wengineo; na kama ukiyafuata matamanio yao baada ya kukufikia ujuzi, hakika hapo utakuwa miongoni mwa wenye kudhullumu. [145]
[145] Na hakukua kutoridhika kwao Watu wa Kitabu nanyi ni kwa kudanganyikiwa ambako kwaweza kuondoka kwa hoja, bali kuudhika huko ni kwa inadi na kiburi. Kwa hivyo Ewe Mtume! Hata ukiwaletea kila hoja ya kukata kuwa Kibla chako ndicho cha kweli, hawakubali kukifuata Kibla chako. Ikiwa Mayahudi wangali wanatumai kuwa bado utarejea kwenye kibla chao, na wanatoa hiyo ni shuruti ya kusilimu kwao, basi watavunjika moyo, wala wewe hutofuata kibla chao. Na hao watu wa Kitabu kila kikundi chao kina kibla chake mbali. Wakristo hawafuati kibla cha Mayahudi, wala Mayahudi hawafuati kibla cha Wakristo, na kila mmoja kati yao anawaona wengine hawamo katika haki. Basi wewe thibiti hapo hapo kwenye Kibla chako, wala usiyaendekeze matamanio yao. Kwani mwenye kuyafuata matamanio yao baada ya kwisha pata ujuzi kuwa wao ni wapotovu, na kujua kuwa yeye yuko katika haki, basi huyo ni katika walio dhulumu na wenye kubobea katika dhulma. Wanasema wafasiri kuwa Mayahudi wanaelekea kwenye Mwamba katika Beitul Muqaddas na Wakristo wanaelekea Mashariki.
Maana: Swahili Translation - Ali Mohsin Al-Barwani. Translated by Ali Mohsen Al-Barwani Toleo 1.0.1, 2025-06-25. QuranEnc.com
Na lau utawaletea wale waliopewa Taurati na Injili aina yoyote ya hoja na dalili kwamba kuelekea kwako Alkaba katika swala ndio haki kutoka kwa Allah Mtukufu, hawangalikifuata kibla chako, kwa inadi na kiburi. Na wala wewe si mwenye kukifuata kibla chao mara nyingine. Wala baadhi yao si wenye kufuata kibla cha baadhi yao. Na lau utafuata matamanio ya nafsi zao kuhusu kibla na mengineyo, baada ya ujuzi uliyoupata kuwa wewe uko kwenye haki na wao wako kwenye batili, wewe wakati huo utakuwa ni miongoni mwa waliozidhulumu nafsi zao. Haya ni maelezo kuambiwa ummah wote, na ni kitisho na kemeo kwa kila afuataye matamanio ya wanaoenda kinyume na Sheria ya Kiislamu.
Maana: Swahili Translation - Abdullah Muhammad and Nasser Khamis. Translated by Dr. Abdullah Muhammad Abu Bakr & Shaykh Nasser Khamis Toleo 1.0.1, 2026-03-12. QuranEnc.com
Kiarabu ni maandishi ya Tanzil, bila kubadilishwa. Maana ni matoleo ya wachapishaji wake, bila kubadilishwa; wahakiki wa Sabīl wenyewe bado hawajazikagua. Kiarabu: maandishi ya Uthmani ya Tanzil, toleo la 1.1. Chanzo: tanzil.net