Ruka hadi kwenye maudhui
Sura ya 2 · Aya ya 144

Al-Baqara 2:144

البقرة

قَدْ نَرَىٰ تَقَلُّبَ وَجْهِكَ فِى ٱلسَّمَآءِ ۖ فَلَنُوَلِّيَنَّكَ قِبْلَةً تَرْضَىٰهَا ۚ فَوَلِّ وَجْهَكَ شَطْرَ ٱلْمَسْجِدِ ٱلْحَرَامِ ۚ وَحَيْثُ مَا كُنتُمْ فَوَلُّوا۟ وُجُوهَكُمْ شَطْرَهُۥ ۗ وَإِنَّ ٱلَّذِينَ أُوتُوا۟ ٱلْكِتَـٰبَ لَيَعْلَمُونَ أَنَّهُ ٱلْحَقُّ مِن رَّبِّهِمْ ۗ وَمَا ٱللَّهُ بِغَـٰفِلٍ عَمَّا يَعْمَلُونَ

Maana

Kwa yakini, tuliona unavyougeuzageuza uso wako mbinguni. Basi, tutakuelekeza kwenye Kibla unachokiridhia. Basi, elekeza uso wako upande wa Msikiti Mtakatifu. Na popote mnapokuwa, zielekezeni nyuso zenu upande wake. Na hakika, wale waliopewa Kitabu wanajua sana kwamba hiyo ndiyo haki itokayo kwa Mola wao Mlezi. Na Mwenyezi Mungu si mwenye kughafilika mbali na yale wanayoyatenda.

Maana: Swahili Translation - Rowad Translation Center. Issued by the Islamic Content Service Association in Languages Toleo 1.0.5, 2025-12-17. QuranEnc.com

Maana

Kwa yakini tukiona unavyo geuza geuza uso wako mbinguni. Basi tutakuelekeza kwenye Kibla ukipendacho. Basi elekeza uso wako upande wa Msikiti Mtakatifu; na popote mnapokuwa zielekezeni nyuso zenu upande huo; na hakika wale walio pewa Kitabu wanajua kwamba hiyo ni haki itokayo kwa Mola wao Mlezi. Na Mwenyezi Mungu si mwenye kughafilika na yale wanayo yatenda. [144]

[144] Na Sisi tulikuona vipi unazichungua mbingu asaa uteremke Wahyi (ufunuo) wa kugeuza Kibla cha Beitul Muqaddas ufuate cha Alkaaba ambacho unakipenda, kwa kuwa ndicho Kibla cha Ibrahim, baba wa Manabii, na baba wa Mayahudi na Waarabu. Na hapo pana Maqaamu Ibrahim, alipokuwa akisimama Ibrahim. Kwa hivyo hichi ni Kibla kilicho kusanya wote, ijapokuwa kinaacha kibla cha Mayahudi. Basi hivi sasa Sisi tunakupa lile ombi lako. Kwa hivyo katika Sala zako elekea Masjidil Haraam (Msikiti Mtakatifu). Na nyinyi Waumini, kadhaalika, elekeeni huko popote pale mlipo. Watu wa Kitabu wanao udhika kwa kukiacha kwenu Kibla cha Beitul Muqaddas wanajua katika vitabu vyao kuwa nyinyi ni watu wa Alkaaba. Na wanajua kuwa amri ya Mwenyezi Mungu inawakhusisha watu wa kila sharia na kibla chao. Na hii ni haki inayo tokana na Mola wao Mlezi. Lakini wao wanataka kukufitinisheni na kukutilieni shaka katika Dini yenu. Na Mwenyezi Mungu si mwenye kughafilika nao, na Yeye atawalipa kwa wayatendayo.

Maana: Swahili Translation - Ali Mohsin Al-Barwani. Translated by Ali Mohsen Al-Barwani Toleo 1.0.1, 2025-06-25. QuranEnc.com

Maana

Hakika Tunauona mzunguko wa uso wako upande wa mbinguni mara baada ya mara, huku ukingojea kuteremka Wahyi juu yako kuhusiana na Kibla. Basi hakika tutakuelekeza kwenye kibla unachokipenda na unachokiridhia, nacho ni upande wa Msikiti wa Ḥaram ulioko Makkah. Basi, elekeza uso wako huko. Na popote mtakapokuwa, enyi Waislamu, na mkataka kuswali, elekeeni upande wa Msikiti wa Ḥaram. Na hakika wale ambao Allah Mtukufu amewapa elimu ya Kitabu miongoni mwa Mayahudi na Wanaswara wanajua kwamba kugeuzwa kwako kuelekezwa Alkaba ndio haki iliyothibiti katika vitabu vyao. Na wala Allah Mtukufu hakuwa ni Mwenye kughafilika juu ya yale wayafanyayo hawa wapinzani wenye shaka, na Atawalipa kwayo.

Maana: Swahili Translation - Abdullah Muhammad and Nasser Khamis. Translated by Dr. Abdullah Muhammad Abu Bakr & Shaykh Nasser Khamis Toleo 1.0.1, 2026-03-12. QuranEnc.com

Al-Baqara

Kiarabu ni maandishi ya Tanzil, bila kubadilishwa. Maana ni matoleo ya wachapishaji wake, bila kubadilishwa; wahakiki wa Sabīl wenyewe bado hawajazikagua. Kiarabu: maandishi ya Uthmani ya Tanzil, toleo la 1.1. Chanzo: tanzil.net