Ruka hadi kwenye maudhui
Sura ya 2 · Aya ya 143

Al-Baqara 2:143

البقرة

وَكَذَٰلِكَ جَعَلْنَـٰكُمْ أُمَّةً وَسَطًا لِّتَكُونُوا۟ شُهَدَآءَ عَلَى ٱلنَّاسِ وَيَكُونَ ٱلرَّسُولُ عَلَيْكُمْ شَهِيدًا ۗ وَمَا جَعَلْنَا ٱلْقِبْلَةَ ٱلَّتِى كُنتَ عَلَيْهَآ إِلَّا لِنَعْلَمَ مَن يَتَّبِعُ ٱلرَّسُولَ مِمَّن يَنقَلِبُ عَلَىٰ عَقِبَيْهِ ۚ وَإِن كَانَتْ لَكَبِيرَةً إِلَّا عَلَى ٱلَّذِينَ هَدَى ٱللَّهُ ۗ وَمَا كَانَ ٱللَّهُ لِيُضِيعَ إِيمَـٰنَكُمْ ۚ إِنَّ ٱللَّهَ بِٱلنَّاسِ لَرَءُوفٌ رَّحِيمٌ

Maana

Na vivyo hivyo tumewafanya muwe Umma wa wastani, ili muwe mashahidi juu ya watu, na Mtume awe shahidi juu yenu. Na hatukukifanya kibla ulichokuwa juu yake isipokuwa ili tupate kumjua yule anayemfuata Mtume, na yule anayegeuka akarejea kwa visigino vyake. Na kwa yakini, hilo lilikuwa jambo kubwa isipokuwa kwa wale aliowaongoa Mwenyezi Mungu. Na Mwenyezi Mungu hakuwa mwenye kuipoteza Imani yenu. Kwa hakika, Mwenyezi Mungu kwa watu ni Mpole, Mwenye kuwarehemu mno.

Maana: Swahili Translation - Rowad Translation Center. Issued by the Islamic Content Service Association in Languages Toleo 1.0.5, 2025-12-17. QuranEnc.com

Maana

Na vivyo hivyo tumekufanyeni muwe Umma wa wasitani, ili muwe mashahidi juu ya watu, na Mtume awe ni shahidi juu yenu. Na hatukukifanya kibla ulicho kuwa nacho ila tupate kumjua yule anaye mfuata Mtume na yule anaye geuka akarejea nyuma. Na kwa yakini hilo lilikuwa jambo gumu isipo kuwa kwa wale alio waongoa Mwenyezi Mungu. Na Mwenyezi Mungu hakuwa mwenye kuipoteza Imani yenu. Kwani Mwenyezi Mungu ni Mpole kwa watu na Mwenye kuwarehemu. [143]

[143] Na kwa ajili ya kutaka huku ndio tukakuongoeni kwenye Njia Iliyo Nyooka kabisa, na tukakujaalieni muwe Umma wa katikati ulio bora kwa muujibu tulivyo iwafikisha Dini sahihi na vitendo vyema, ili muwe wenye kuthibitisha Haki kwa mnasaba wa sharia zilizo tangulia, na ili Mtume awe mlinzi juu yenu, akikupeni nguvu kwa uwongozi wake kwa muda wa uhai wake, na kwa kufuata njia yake na mwendo wake baada ya kufa kwake. Ama kibla cha Beitul Muqaddas tulicho amrisha kifuatwe kwa muda fulani tulikifanya kuwa ni mtihani kwa Waislamu ili watambulikane wanao t'ii wakielekee kwa ut'iifu, na wenye kuchukuliwa na mori wao wa Kiarabu kwa kufuata nyao za Ibrahim tu waivunje amri ya Mwenyezi Mungu na kwa hivyo wapotelee njia ya upotovu. Na ilikuwa ile amri ya kuelekea Beitul Muqaddas ni katika mambo magumu ila kwa wale ambao wamejaaliwa kupata hidaya ya Mwenyezi Mungu. Ikawa kufuata amri hii miongoni mwa nguzo za Imani. Mwenye kuelekea kibla cha Beitul Muqaddas katika zama ilipo amrishwa hayo hakupoteza Imani yake na ibada yake kwa upole na rehema ya Mwenyezi Mungu.

Maana: Swahili Translation - Ali Mohsin Al-Barwani. Translated by Ali Mohsen Al-Barwani Toleo 1.0.1, 2025-06-25. QuranEnc.com

Maana

Na kama tulivyowaongoza, enyi Waislamu, kwenye njia sahihi katika Dini, tumewafanya kuwa ni ummah bora ulio muadilifu, ili mue mashahidi juu ya ummah waliopita, kesho Akhera, kwamba Mitume wao waliwafikishia jumbe za Mola wao, na ili Mtume, kesho Akhera, awe vilevile ni shahidi juu yenu, kwamba yeye aliwafikishia ujumbe wa Mola wake. Wala hatukukifanya, ewe Mtume, kile kibla cha Baitul Maqdis ulichokuwa ukikielekea, kisha tukakugeuza tukakuelekeza Alkaba (iliyopo Makkah) isipokuwa ni yapate kuonekana yale tuliyoyajua hapo kale, ujuzi unaofungamana na thawabu na adhabu, ili tumtenganishe yule ambaye atakufuata na kukutii na kuelekea pamoja nawe pale utakapoelekea na yule aliye dhaifu wa imani, awe ni mwenye kubadilika na kuritadi kwa kuacha Dini yake kwa shaka yake na unafiki wake. Hali hii ya kugeuka Muislamu katika Swala yake, kuacha kuelekea Baitul Maqdis na kuelekea Alkaba ni ngumu na nzito, isipokuwa kwa wale walioongozwa na Allah Mtukufu na kupewa neema ya Imani na uchajimungu. Na wala hakuwa Allah Mtukufu ni Mwenye kupoteza imani yenu Kwake na kumfuata kwenu Mtume Wake kwa kuzibatilisha Swala zenu mlipokuwa mnaelekea kibla cha zamani. Hakika Yeye Allah Mtukufu, Aliyetakasika na upungufu wowote na Aliyetukuka, kwa watu ni Mpole na Mwenye huruma.

Maana: Swahili Translation - Abdullah Muhammad and Nasser Khamis. Translated by Dr. Abdullah Muhammad Abu Bakr & Shaykh Nasser Khamis Toleo 1.0.1, 2026-03-12. QuranEnc.com

Al-Baqara

Kiarabu ni maandishi ya Tanzil, bila kubadilishwa. Maana ni matoleo ya wachapishaji wake, bila kubadilishwa; wahakiki wa Sabīl wenyewe bado hawajazikagua. Kiarabu: maandishi ya Uthmani ya Tanzil, toleo la 1.1. Chanzo: tanzil.net