Al-Baqara 2:142
البقرةسَيَقُولُ ٱلسُّفَهَآءُ مِنَ ٱلنَّاسِ مَا وَلَّىٰهُمْ عَن قِبْلَتِهِمُ ٱلَّتِى كَانُوا۟ عَلَيْهَا ۚ قُل لِّلَّهِ ٱلْمَشْرِقُ وَٱلْمَغْرِبُ ۚ يَهْدِى مَن يَشَآءُ إِلَىٰ صِرَٰطٍ مُّسْتَقِيمٍ
Wapumbavu miongoni mwa watu watasema: ‘Ni nini kilichowageuza kutoka kibla chao walichokuwa wakikielekea?’ Sema: ‘Mashariki na Magharibi ni ya Mwenyezi Mungu; Yeye humwongoa amtakaye kwenye njia iliyonyooka.’
Maana: Swahili Translation - Rowad Translation Center. Issued by the Islamic Content Service Association in Languages Toleo 1.0.5, 2025-12-17. QuranEnc.com
WAPUMBAVU miongoni mwa watu watasema: Nini kilicho wageuza kutoka kibla chao walicho kuwa wakikielekea? Sema: Mashariki na Magharibi ni ya Mwenyezi Mungu; Yeye humwongoa amtakaye kwenye njia iliyo nyooka. [142]
[142] Hakika wale wachache wa akili walio potezwa na pumbao lao wasiweza kufikiri sawa na kuzingatia miongoni mwa Mayahudi, na Wakristo, na washirikina na wanaafiki, watachukizwa kuwaona Waumini wameacha kukielekea kibla cha Beitul Muqaddas (Yerusalemu) walicho kuwa wakikielekea kwanza katika Sala. Na wao wakiona kuwa hicho kinastahiki zaidi kuliko kibla kingine, yaani cha Alkaaba. Basi waambie, Ewe Nabii! Jiha zote ni za Mwenyezi Mungu. Hapana upande ulio bora kuliko mwengine kwa dhati yake, lakini Mwenyezi Mungu ndiye mwenyewe anachagua upande autakao uwe ni kibla cha Sala. Na Yeye kwa mapenzi yake huuongoa kila umma katika wanaadamu kufuata njia iliyo sawa anayo ikhiari Yeye na anayo ikhusisha Yeye. Na sasa umekuja Ujumbe wa Muhammad unafuta risala zote zilizo tangulia, na Kibla cha sasa cha Haki ni hichi cha Alkaaba iliyopo Makka.
Maana: Swahili Translation - Ali Mohsin Al-Barwani. Translated by Ali Mohsen Al-Barwani Toleo 1.0.1, 2025-06-25. QuranEnc.com
Watasema wajinga na madhaifu wa akili, miongoni mwa Mayahudi na mfano wao, wakiwa katika hali ya kufanya maskhara na kupinga, «Ni kitu gani kilichowageuza hawa Waislamu kuacha kibla chao ambacho walikuwa wakisali kukielekea mwanzo wa Uislamu?» (Nacho ni Baitul Maqdis). Waambie, ewe Mtume, «Upande wa Mashariki na wa Magharibi na katikati yake ni milki ya Allah Mtukufu. Hapana upande wowote, miongoni mwa pande zote, ulioko nje ya milki Yake. Yeye Anamuongoza Amtakaye, miongoni mwa waja Wake, kumuelekeza njia ya uongofu iliyo sawa.» Katika hayo, pana ujulishaji kwamba mambo yote ni ya Allah Mtukufu, katika kufuata amri Zake, na kwa hivyo, popote tuelekezwapo tutaelekea.
Maana: Swahili Translation - Abdullah Muhammad and Nasser Khamis. Translated by Dr. Abdullah Muhammad Abu Bakr & Shaykh Nasser Khamis Toleo 1.0.1, 2026-03-12. QuranEnc.com
Kiarabu ni maandishi ya Tanzil, bila kubadilishwa. Maana ni matoleo ya wachapishaji wake, bila kubadilishwa; wahakiki wa Sabīl wenyewe bado hawajazikagua. Kiarabu: maandishi ya Uthmani ya Tanzil, toleo la 1.1. Chanzo: tanzil.net