Ruka hadi kwenye maudhui
Sura ya 2 · Aya ya 104

Al-Baqara 2:104

البقرة

يَـٰٓأَيُّهَا ٱلَّذِينَ ءَامَنُوا۟ لَا تَقُولُوا۟ رَٰعِنَا وَقُولُوا۟ ٱنظُرْنَا وَٱسْمَعُوا۟ ۗ وَلِلْكَـٰفِرِينَ عَذَابٌ أَلِيمٌ

Maana

Enyi mlioamini! Msiseme: "Raa'ina", na semeni: "Ndhurna". Na sikieni! Na makafiri watapata adhabu chungu.[1]

[1] Neno “ra’ina" linalomaanisha "tutunze hali zetu". Lakini kwa lugha ya mayahudi linamaanisha ugumu. Basi Mwenyezi Mungu akakataza neno hili ili kuufunga mlango huu, na akawaamrisha waja wake waseme badala yake: “Undhurna" yaani "Tutazame, tutunze.” kwa Waarabu na Mayahudi.

Maana: Swahili Translation - Rowad Translation Center. Issued by the Islamic Content Service Association in Languages Toleo 1.0.5, 2025-12-17. QuranEnc.com

Maana

Enyi mlio amini! Msiseme: "Raa'ina", na semeni: "Ndhurna". Na sikieni! Na makafiri watapata adhabu chungu. [104]

[104] Enyi mlio amini! Tahadharini na hawa Mayahudi. Msimwambie Mtume pale anapo kusomeeni ufunuo: "Raa'ina" kwa kukusudia akuwekeni pahala pa uangalizi wake, yaani (Tuchunge, Turai), na akupeni muda katika kusoma kwake mpaka mzingatie na mhifadhi. Kwani watu makhabithi miongoni mwa Mayahudi husaidiana kutaka kukuigeni na kupindua ndimi zao kwa neno hilo mpaka likawa neno la matusi wanalo lijua wao. Na wao humkabili Mtume kwa neno hilo kwa kumfanyia maskhara. Lakini nyinyi tumieni neno jingine wasilo weza Mayahudi kulipatia njia ya kufanya ukhabithi wao na maskhara yao. Tumieni neno: "Ndhurna" yaani "Tuangalie". Na sikilizeni vyema anayo kusomeeni Mtume. Na Mwenyezi Mungu anawadundulizia adhabu kali kwa Siku ya Kiyama hawa wanao mfanyia maskhara Mtume. Katika lugha ya Kiyahudi ya Kiebrania lipo neno "Rai'nu" ambalo limejengwa na neno "Ra'" kwa maana ya "Shari" na neno "nu" linaonesha jamii, wingi. Na maana ya neno lote ni kuwa "Wewe ni shari yetu", wakikusudia kumwambia Mtume hayo.

Maana: Swahili Translation - Ali Mohsin Al-Barwani. Translated by Ali Mohsen Al-Barwani Toleo 1.0.1, 2025-06-25. QuranEnc.com

Maana

Enyi ambao mliamini, msiseme kumwambia Mtume Muhammad, rehema na amani zimshukie, “Rã’inã.” Yaani: tupatie masikizi yako, utufahamu na utufahamishe. Sababu Mayahudi walikuwa wakisema maneno haya kumwambia Nabii, rehema na amani zimshukie, wakipotoa ndimi zao kwa neno hilo, wakikusudia kumtukana na kumnasibisha na kutoelewa. Na semeni badala yake, enyi Waumini, “Undhurnã.” Yaani: tuangalie na utuchunge. Lina maana yale-yale yanayokusudiwa. «Na msikie Kitabu cha Mola wenu mnachosomewa na mkifahamu.» Na wenye kukanusha wana adhabu yenye kuumiza.

Maana: Swahili Translation - Abdullah Muhammad and Nasser Khamis. Translated by Dr. Abdullah Muhammad Abu Bakr & Shaykh Nasser Khamis Toleo 1.0.1, 2026-03-12. QuranEnc.com

Al-Baqara

Kiarabu ni maandishi ya Tanzil, bila kubadilishwa. Maana ni matoleo ya wachapishaji wake, bila kubadilishwa; wahakiki wa Sabīl wenyewe bado hawajazikagua. Kiarabu: maandishi ya Uthmani ya Tanzil, toleo la 1.1. Chanzo: tanzil.net