Ruka hadi kwenye maudhui
Sura ya 13 · Aya ya 33

Ar-Ra'd 13:33

الرعد

أَفَمَنْ هُوَ قَآئِمٌ عَلَىٰ كُلِّ نَفْسٍۭ بِمَا كَسَبَتْ ۗ وَجَعَلُوا۟ لِلَّهِ شُرَكَآءَ قُلْ سَمُّوهُمْ ۚ أَمْ تُنَبِّـُٔونَهُۥ بِمَا لَا يَعْلَمُ فِى ٱلْأَرْضِ أَم بِظَـٰهِرٍ مِّنَ ٱلْقَوْلِ ۗ بَلْ زُيِّنَ لِلَّذِينَ كَفَرُوا۟ مَكْرُهُمْ وَصُدُّوا۟ عَنِ ٱلسَّبِيلِ ۗ وَمَن يُضْلِلِ ٱللَّهُ فَمَا لَهُۥ مِنْ هَادٍ

Maana

Je, anayeisimamia kila nafsi kwa yale iliyoyachuma...? Na wamemfanyia Mwenyezi Mungu washirika! Sema: Watajeni. Au ndiyo mnampa habari ya yale asiyoyajua katika ardhi, au ni maneno matupu tu? Bali wale waliokufuru wamepambiwa njama zao na wamezuiliwa njia ya sawasawa. Na yule ambaye Mwenyezi Mungu amempoteza, basi hana yeyote wa kumwongoa.

Maana: Swahili Translation - Rowad Translation Center. Issued by the Islamic Content Service Association in Languages Toleo 1.0.5, 2025-12-17. QuranEnc.com

Maana

Je! Anaye isimamia kila nafsi kwa yale iliyo yachuma? Na wamemfanyia Mwenyezi Mungu kuwa na washirika! Sema watajeni. Au ndio mnampa khabari ya yale asiyo yajua katika ardhi; au ni maneno matupu? Bali walio kufuru wamepambiwa vitimbi vyao na wamezuiliwa njia. Na ambaye Mwenyezi Mungu amemwacha apotee basi hana wa kumwongoa. [33]

[33] Hakika washirikina wamefanya upumbavu katika kukanya kwao, wakamfanyia Mwenyezi Mungu washirika wa kuwaabudu. Kwani ati huyo ambaye ndiye Mwenye kuhifadhi na kuangalia kila nafsi, na kuipimia kwa kuilipa kheri na shari inayo ichuma, atakuwa wa kufananishwa na haya masanamu? Ewe Nabii! Waambie: Yaelezeni yalivyo kweli! Je, hayo masanamu ya hai? Yanaweza kujikinga na madhara? Yakiwa mawe hayanufaishi wala hayadhuru, basi mbona mnajidanganya nafsi zenu kuwa miungu hiyo ndio imemwambia Mwenyezi Mungu hayo ambayo mnadhani kuwa Yeye hayajui ya ardhi hii? Au mnaiweka kwenye cheo cha kuiabudu kwa maneno yanayo toka katika ndimi zenu? Hakika iliyopo ni kuwa watu hawa wamezugwa na mazingatio yao na mawazo yao ya upotovu. Na kwa sababu hiyo wameiacha Njia ya Haki wakabaki wakitanga tanga! Na wenye kupotea kama hao, basi hawana wa kuwaongoa yeyote, kwani wameziachisha nafsi zao Njia ya Uwongofu.

Maana: Swahili Translation - Ali Mohsin Al-Barwani. Translated by Ali Mohsen Al-Barwani Toleo 1.0.1, 2025-06-25. QuranEnc.com

Maana

Je, Yule Anayesimamia kila nafsi Akiyadhibiti yale inayoyafanya, ni mwenye haki zaidi ya kuabudiwa au ni hivi viumbe visivyojiweza? Na wao, kwa ujinga wao walimfanyia Allah Mtukufu washirika miongoni mwa viumbe Wake wakawa wanawaabudu. Waambie, ewe Mtume, «Tajeni majina yao na sifa zao.» Na hawatapata kwenye sifa zao chochote cha kuwafanya wao wastahiki kuabudiwa. Au nyinyi mnampasha habari Allah Mtukufu kuwa Ana washirika katika ardhi Yake ambao Hawajui? Au mnawaita ni washirika kimaneno tu bila ya kuwa na hakika? Bali Shetani aliwapambia makafiri neno lao la ubatilifu na akawazuia njia ya Allah Mtukufu. Na yule ambaye Allah Mtukufu Hakumwafikia kuongoka basi hakuna yoyote mwenye kumuongoza na kumwafikia kwenye haki na uongofu.

Maana: Swahili Translation - Abdullah Muhammad and Nasser Khamis. Translated by Dr. Abdullah Muhammad Abu Bakr & Shaykh Nasser Khamis Toleo 1.0.1, 2026-03-12. QuranEnc.com

Ar-Ra'd

Kiarabu ni maandishi ya Tanzil, bila kubadilishwa. Maana ni matoleo ya wachapishaji wake, bila kubadilishwa; wahakiki wa Sabīl wenyewe bado hawajazikagua. Kiarabu: maandishi ya Uthmani ya Tanzil, toleo la 1.1. Chanzo: tanzil.net