Yusuf 12:83
يوسفقَالَ بَلْ سَوَّلَتْ لَكُمْ أَنفُسُكُمْ أَمْرًا ۖ فَصَبْرٌ جَمِيلٌ ۖ عَسَى ٱللَّهُ أَن يَأْتِيَنِى بِهِمْ جَمِيعًا ۚ إِنَّهُۥ هُوَ ٱلْعَلِيمُ ٱلْحَكِيمُ
Akasema: Bali nafsi zenu zimewashawishi kwenye jambo fulani. Basi subira ni nzuri! Huenda Mwenyezi Mungu akaniletea wote pamoja. Hakika Yeye ndiye Mwenye kujua vyema, Mwenye hekima.
Maana: Swahili Translation - Rowad Translation Center. Issued by the Islamic Content Service Association in Languages Toleo 1.0.5, 2025-12-17. QuranEnc.com
Akasema: Bali nafsi zenu zimekushawishini kwenye jambo fulani. Subira ni njema! Asaa Mwenyezi Mungu akaniletea wote pamoja. Hakika Yeye ni Mjuzi Mwenye hikima. [83]
[83] Wakarejea wana walio baki kwa Yaa'qub. Wakamueleza kama alivyo wausia kaka yao mkubwa. Khabari ile ikamtibua huzuni zake, zikazidi kwa kumpoteza mwanawe wa pili. Wala hakutua nafsi yake kwa kuwa wao hawana makosa ya kusabibisha kupotea kwake, naye angali na machungu kwa waliyo mfanyia Yusuf. Akapiga ukelele kwa kuwatuhumu akiwaambia: Niya yenu haikusalimika katika kumhifadhi mwanangu, lakini nafsi zenu zimekuchocheeni mumpoteze kama mlivyo mpoteza nduguye. Lau kuwa nyinyi hamkutoa fatwa ya kuwa mwizi ashikwe afanywe mtumwa kuwa ndiyo adabu ya mwizi huyo Mheshimiwa asingeli mshika mwanangu, wala asingeli baki kaka yenu huko Misri. Lakini mimi sina hila ila kustahamili katika msiba wangu kwa maliwaza mema, huku nikitaraji kwa Mwenyezi Mungu anirudishie wanangu wote. Kwani Yeye ndiye Mwenye ujuzi ulio zunguka hali yangu na hali zao. Na Yeye ndiye Mwenye hikima yenye kushinda, na kwa hiyo ndio hunitendea na hunipangia.
Maana: Swahili Translation - Ali Mohsin Al-Barwani. Translated by Ali Mohsen Al-Barwani Toleo 1.0.1, 2025-06-25. QuranEnc.com
Akawaambia, «Bali nafsi zenu zinazoamrisha mabaya ndizo zilizowapambia njama mlizozipanga, kama mlivyomfanyia Yûsuf. Basi uvumilivu wangu ni uvumilivu mzuri usio na babaiko wala ulalamishi. Kwani huenda Allah Mtukufu Akanirudishia wanangu watatu: Yûsuf, nduguye wa kwa baba na mama na ndugu yao mkubwa aliyebaki nyuma kwa sababu ya ndugu yake. Hakika Yeye Ndiye Mjuzi wa hali yangu, Ndiye Mwenye hekima katika uendeshaji mamboWake».
Maana: Swahili Translation - Abdullah Muhammad and Nasser Khamis. Translated by Dr. Abdullah Muhammad Abu Bakr & Shaykh Nasser Khamis Toleo 1.0.1, 2026-03-12. QuranEnc.com
Kiarabu ni maandishi ya Tanzil, bila kubadilishwa. Maana ni matoleo ya wachapishaji wake, bila kubadilishwa; wahakiki wa Sabīl wenyewe bado hawajazikagua. Kiarabu: maandishi ya Uthmani ya Tanzil, toleo la 1.1. Chanzo: tanzil.net