Ruka hadi kwenye maudhui
Sura ya 11 · Aya ya 17

Hud 11:17

هود

أَفَمَن كَانَ عَلَىٰ بَيِّنَةٍ مِّن رَّبِّهِۦ وَيَتْلُوهُ شَاهِدٌ مِّنْهُ وَمِن قَبْلِهِۦ كِتَـٰبُ مُوسَىٰٓ إِمَامًا وَرَحْمَةً ۚ أُو۟لَـٰٓئِكَ يُؤْمِنُونَ بِهِۦ ۚ وَمَن يَكْفُرْ بِهِۦ مِنَ ٱلْأَحْزَابِ فَٱلنَّارُ مَوْعِدُهُۥ ۚ فَلَا تَكُ فِى مِرْيَةٍ مِّنْهُ ۚ إِنَّهُ ٱلْحَقُّ مِن رَّبِّكَ وَلَـٰكِنَّ أَكْثَرَ ٱلنَّاسِ لَا يُؤْمِنُونَ

Maana

Basi je, yule ambaye ana ushahidi ulio wazi kutoka kwa Mola wake Mlezi, na unaofuatwa na shahidi anayetoka kwake, na kabla yake kilikuwapo Kitabu cha Musa kilichokuwa mwongozi na rehema. Hao wanaiamini. Naye anayeikufuru katika makundi, basi Moto ndipo pahali pa miadi yake. Kwa hivyo, usiwe katika shaka juu yake. Hakika, hii ni haki itokayo kwa Mola wako Mlezi, lakini wengi wa watu hawaamini.

Maana: Swahili Translation - Rowad Translation Center. Issued by the Islamic Content Service Association in Languages Toleo 1.0.5, 2025-12-17. QuranEnc.com

Maana

Basi je, mtu aliye na dalili wazi itokayo kwa Mola wake Mlezi, inayo fuatwa na shahidi anaye toka kwake, na kabla yake kilikuwa Kitabu cha Musa kilicho kuwa mwongozi na rehema - hao wanamuamini, na anaye mkataa katika makundi, basi Moto ndio pahala pa miadi yao. Basi usiwe na shaka juu ya hayo. Hii ni Haki itokayo kwa Mola wako Mlezi; lakini watu wengi hawaamini. [17]

[17] Je, anaye kuwa anakwenda katika maisha yake kwa uangalifu na uwongofu kutokana na Mola wake Mlezi, na anaitaka Haki kwa kuifanyia ikhlasi, pamoja naye anaye shahidi anaye mshuhudia kuwa kweli katoka kwa Mwenyezi Mungu, naye shahidi huyo ni Qur'ani, na shahidi wa kabla yake ni Kitabu cha Musa alicho kiteremsha Mwenyezi Mungu kiwe ni uwongozi wa kufuatwa kwa aliyo yaleta, na ni rehema kwa wenye kukifuata, je, huyo ni sawa sawa na anaye kwenda katika maisha yake katika giza na upofu, hashughulikii ila starehe za duniani tu na pumbao lake? Hao walio tajwa mwanzo ndio wale ambao Mwenyezi Mungu ameyatia nuru macho yao. Wanamuamini Nabii huyu, na Kitabu alicho teremshiwa. Na wenye kumkataa wakakusanyika na kujiunga dhidi yake, basi Moto ndio pahali pa miadi yao Siku ya Kiyama. Ewe Nabii! Usiwe na shaka na hii Qur'ani. Hii ni kweli itokayo kwa Mola wako Mlezi. Haingii upotovu. Lakini watu wengi wanapotezwa na matamanio, basi hawaamini kama iwapasavyo. Mwenyezi Mungu amemuamrisha Nabii s.a.w. asitie shaka, si kwa kuwa yawezekana kuwa yeye awe na shaka, lakini ni kuashiria kuwa walio kuwa duni yake Nabii wajilinde wasiache shaka ikaingia nyoyoni mwao.

Maana: Swahili Translation - Ali Mohsin Al-Barwani. Translated by Ali Mohsen Al-Barwani Toleo 1.0.1, 2025-06-25. QuranEnc.com

Maana

Je, yule aliyekuwa kwenye hoja na uangalifu kutoka kwa Mola wake katika kile anachokiamini na anachokilingania kwa wahyi ambao ndani yake Allah Mtukufu Ameuteremsha ushahidi huu, na ukafuatiwa na hoja nyingine kutoka Kwake yenye kuutolea ushahidi, nayo ni Jibrili au ni Muhammad, (rehema na amani ziwashukie), na ukatiliwa nguvu na dalili ya tatu kabla ya Qur’ani, nayo ni Taurati – Kitabu alichoteremshiwa Mûsã chenye uongozi na rehema kwa waliokiamini- (je yeye) ni kama yule ambaye hamu yake ilikuwa ni maisha yenye kutoweka na pambo lake? Hao wanaiamini hii Qur’ani wanazifuata hukumu zake kivitendo. Na mwenye kuikanusha hii Qur’ani, miongoni mwa wale waliojikusanya kumpinga Mtume wa Allah Mtukufu, (rehema za Allah Mtukufu na amani zimshukie), basi malipo yake ni Moto, hapana budi atauingia. Basi usiwe na shaka juu ya jambo la Qur’ani na kuwa inatoka kwa Allah Mtukufu Aliyetukuka baada ya dalili na hoja kulitolea ushahidi hilo. Na ujue kwamba Dini hii ndio ukweli unaotoka kwa Mola wako, lakini wengi wa watu hawaamini wala hawayatendi yale wanayoamrishwa. Huu ni muongozo unaowaenea ummah wa Muhammad, (rehema za Allah Mtukufu na amani zimshukie).

Maana: Swahili Translation - Abdullah Muhammad and Nasser Khamis. Translated by Dr. Abdullah Muhammad Abu Bakr & Shaykh Nasser Khamis Toleo 1.0.1, 2026-03-12. QuranEnc.com

Hud

Kiarabu ni maandishi ya Tanzil, bila kubadilishwa. Maana ni matoleo ya wachapishaji wake, bila kubadilishwa; wahakiki wa Sabīl wenyewe bado hawajazikagua. Kiarabu: maandishi ya Uthmani ya Tanzil, toleo la 1.1. Chanzo: tanzil.net