Hud 11:1
هودالٓر ۚ كِتَـٰبٌ أُحْكِمَتْ ءَايَـٰتُهُۥ ثُمَّ فُصِّلَتْ مِن لَّدُنْ حَكِيمٍ خَبِيرٍ
Alif Laam Raa.[1] Hiki ni Kitabu ambacho Aya zake zimefanywa kuwa sawasawa, kisha zikapambanuliwa kwa kina, kilichotoka kwa Mwenye Hekima, Mwenye habari zote.
[1] Herufi hizi "Alif Laam Raa" na herufi nyinginezo za mkato zilizo mwanzoni mwa sura mbalimbali zinaonyesha hali ya ushindi wa Qur-ani. Kwani, washirikina walipewa changamoto kwayo, lakini wakashindwa na hawakuweza kuipinga, ilhali inajumuisha herufi hizi zinazounda lugha ya Kiarabu. Kwa hivyo, kutoweza kwa Waarabu kuleta kitu kama hicho - ingawa walikuwa ndio watu wenye ufasaha zaidi - kunaonyesha kwamba Qur-ani ni ufunuo (wahyi) kutoka kwa Mwenyezi Mungu.
Maana: Swahili Translation - Rowad Translation Center. Issued by the Islamic Content Service Association in Languages Toleo 1.0.5, 2025-12-17. QuranEnc.com
Alif Lam Ra. Hiki ni Kitabu ambacho Aya zake zimewekwa wazi, kisha zikapambanuliwa, kilicho toka kwa Mwenye Hikima na Mwenye Khabari! [1]
[1] Alif Lam Ra (A.L.R.)...Hizi ni harufi zilizo anziwa Sura hii kuwa ni ishara kuwa Qur'ani ni muujiza juu ya kuwa imeundwa kwa hizi hizi harufi zinazo tamkwa, na pia ni kuwazindua watu wanapo isikiliza inapo somwa Qur'ani Tukufu kuwa ni Kitabu chenye shani kuu. Zimeteremshwa Aya zake zimeshikana, madhubuti, hazina ndani yake upotovu, wala ubabaishi, na zimetungwa kwa njia isiyo na dosari, iwazi, na yenye kubainisha. Kisha hukumu zake zikapambanuliwa. Na Kitabu hichi juu ya utukufu wake ulio nao nafsi yake, kina utukufu zaidi kwa kuwa kimetokana na Mwenyezi Mungu ambaye anajua kila kitu, na Yeye Subhanahu anapanga mambo yote kwa pahala pake.
Maana: Swahili Translation - Ali Mohsin Al-Barwani. Translated by Ali Mohsen Al-Barwani Toleo 1.0.1, 2025-06-25. QuranEnc.com
Alif, Lãm, Rã’. Maneno yashatangulia, kuhusu herufi zinazokatwa, katika mwanzo wa Sura ya Al-Baqarah. Hiki ni Kitabu ambacho Allah Mtukufu Amemteremshia Muhammad, (rehema za Allah Mtukufu na amani imshukie), na ambacho aya zake zimepangwa vizuri zisizo na kasoro wala ubatilifu, kisha zimefafanuliwa kwa maamrisho na makatazo na maelezo ya halali na haramu yatokayo kwa Allah Mtukufu Aliye na hekima katika uendeshaji mambo Aliye Mtambuzi wa vile yanavyoishia.
Maana: Swahili Translation - Abdullah Muhammad and Nasser Khamis. Translated by Dr. Abdullah Muhammad Abu Bakr & Shaykh Nasser Khamis Toleo 1.0.1, 2026-03-12. QuranEnc.com
Kiarabu ni maandishi ya Tanzil, bila kubadilishwa. Maana ni matoleo ya wachapishaji wake, bila kubadilishwa; wahakiki wa Sabīl wenyewe bado hawajazikagua. Kiarabu: maandishi ya Uthmani ya Tanzil, toleo la 1.1. Chanzo: tanzil.net