Yunus 10:35
يونسقُلْ هَلْ مِن شُرَكَآئِكُم مَّن يَهْدِىٓ إِلَى ٱلْحَقِّ ۚ قُلِ ٱللَّهُ يَهْدِى لِلْحَقِّ ۗ أَفَمَن يَهْدِىٓ إِلَى ٱلْحَقِّ أَحَقُّ أَن يُتَّبَعَ أَمَّن لَّا يَهِدِّىٓ إِلَّآ أَن يُهْدَىٰ ۖ فَمَا لَكُمْ كَيْفَ تَحْكُمُونَ
Sema, "Je, yupo yeyote katika washirika wenu mwenye kuongoa kwenye haki?" Sema, "Mwenyezi Mungu anaongoa kwenye haki." Basi, je, yule anayeongoa kwenye haki anastahiki zaidi kufuatwa au yule asiyeongoka isipokuwa akiongozwa? Basi nyinyi mna nini, mnahukumu namna gani?
Maana: Swahili Translation - Rowad Translation Center. Issued by the Islamic Content Service Association in Languages Toleo 1.0.5, 2025-12-17. QuranEnc.com
Sema: Je! Yupo katika miungu yenu ya ushirikina anaye ongoa kwendea Haki? Sema: Mwenyezi Mungu anaongoa kwendea Haki. Basi, je, anaye stahiki kufuatwa ni yule Mwenye kuongoa kwendea Haki au asiye ongoa ila aongozwe yeye? Basi nyinyi mna nini? Mnahukumu namna gani? [35]
[35] Ewe Mtume! Waambie hao washirikina: Yupo yeyote katika hao mlio wafanya washirika wa Mwenyezi Mungu mkawaabudu, awezaye kupambanua baina ya uwongofu na upotovu, akawaongoza watu kwenye Njia ya Haki? Wataemewa! Basi, je! Yupi bora kufuatwa - Mwenye kuweza kuongoa kwendea Haki au asiye weza hata kujiongoa nafsi yake? Naye huyo hawezi kumwongoa mtu, ila yeye anahitaji mtu wa kumwongoa. Hao ndio kama wakuu wa makafiri, mapadri na mamonaki ambao ndio mmewafanya ni waola mkamuacha Mwenyezi Mungu!! Nini basi kilicho kupelekeeni kukengeuka hata mkawashirikisha hawa na Mwenyezi Mungu? Na nini hali ya ajabu iliyo kusukumeni kwenye hizo hukumu na sharia za kigeni?
Maana: Swahili Translation - Ali Mohsin Al-Barwani. Translated by Ali Mohsen Al-Barwani Toleo 1.0.1, 2025-06-25. QuranEnc.com
Sema, ewe Mtume, kuwaambia hawa washirikina, «Je, kuna yoyote, miongoni mwa washirika wenu, mwenye kuongoza kwenye njia iliyonyooka?» Hakika wao hawawezi hilo. Waambie, «Allah Mtukufu, Peke Yake, Anamuongoza aliyepotea njia ya uongofu na kumuelekeza kwenye haki. Basi ni yupi anayefaa zaidi kufuatwa: ni yule anayeongoza, peke yake, kwenye njia ya haki au ni yule ambaye haongoki, kwa kutojua kwake na kwa upotevu wake, nao ndio hao washirikina wenu ambao hawaongozi wala hawaongoki mpaka waongozwe? Basi muna nini nyinyi, vipi mnamlinganisha Allah Mtukufu na viumbe vyake?» Huu ni uamuzi uliotenguka.
Maana: Swahili Translation - Abdullah Muhammad and Nasser Khamis. Translated by Dr. Abdullah Muhammad Abu Bakr & Shaykh Nasser Khamis Toleo 1.0.1, 2026-03-12. QuranEnc.com
Kiarabu ni maandishi ya Tanzil, bila kubadilishwa. Maana ni matoleo ya wachapishaji wake, bila kubadilishwa; wahakiki wa Sabīl wenyewe bado hawajazikagua. Kiarabu: maandishi ya Uthmani ya Tanzil, toleo la 1.1. Chanzo: tanzil.net