Ruka hadi kwenye maudhui
Sura ya 1 · Aya ya 7

Al-Faatiha 1:7

الفاتحة

صِرَٰطَ ٱلَّذِينَ أَنْعَمْتَ عَلَيْهِمْ غَيْرِ ٱلْمَغْضُوبِ عَلَيْهِمْ وَلَا ٱلضَّآلِّينَ

Maana

Njia ya wale uliowaneemesha. Siyo ya wale waliokasirikiwa, wala waliopotea.

Maana: Swahili Translation - Rowad Translation Center. Issued by the Islamic Content Service Association in Languages Toleo 1.0.5, 2025-12-17. QuranEnc.com

Maana

Njia ya ulio waneemesha, siyo ya walio kasirikiwa, wala walio potea. [7]

[7] Na njia hiyo ndiyo ya waja wako ulio wawezesha kukuamini Wewe, na ukawajaalia neema ya uwongofu na radhi, sio njia ya walio stahiki kupata ghadhabu zako na wakaiwacha njia ya haki na kheri, kwa sababu hao wameitupa imani kukuamini Wewe na kuelekea kwenye uwongofu wako. (Hapana katika Vitabu vyote vitakatifu, vya dini zote, dua inayo lingana na hii kwa uzuri wake, na utimilivu wake. Baada ya kumsifu Mwenyezi Mungu kwa Rehema yake isio na ukomo wala kipimo, na kumshukuru Mola Mwenye kuviumba na kuviangalia na kuvilea kwa huruma viumbe vyote, na kuhakikisha kuwa tunajua kuwa hapana Mungu ila Yeye tu wa kuabudiwa na kuombwa msaada, na kuwa hapana wa kumuingilia katika Ufalme wake na Uwezo wake wa kulipa hisabu kwa kila alitendalo mtu, hapo tena ndio tunaomba. Na tunaomba nini? Si mkate wa kula, wala riziki yoyote, wala jambo lolote la manufaa ya kimwili duniani, bali tunaomba Uwongofu kwenye Njia Iliyo Nyooka, Njia ya kumwendea Yeye Mwenyezi Mungu Mwingi wa Rehema. Tunaomba tusiendee njia waliyo ifuata wale walio kasirikiwa na Mwenyezi Mungu, kwa kuwa walifunzwa wakajua, lakini kwa chuki na jeuri wakakataa kuongoka, wala sio njia ya wale ambao labda kwa ujinga wamepotea. Hiyo kwa mukhtasari ndiyo Dua ambayo Waislamu, wanafunzwa waiombe, na wanaiomba mara kadhaa wa kadhaa katika Sala zao, na katika kila fursa inapo tokea.)

Maana: Swahili Translation - Ali Mohsin Al-Barwani. Translated by Ali Mohsen Al-Barwani Toleo 1.0.1, 2025-06-25. QuranEnc.com

Maana

Njia ya wale uliowaneemesha miongoni mwa Manabii, wakweli wa imani, mashahidi na wema. Wao ndio watu wa uongofu na kusimama imara. Na usitufanye kuwa miongoni mwa wale waliofuata njia ya waliokasirikiwa, wale walioijua haki na wasiifuate kivitendo, nao ni Mayahudi na wale waliofanana na wao; wala usitufanye ni miongoni mwa wapotevu, nao ni wale ambao hawakuongoka kwa ujinga waliokuwa nao, wakapotea njia, nao ni Wanaswara na waliofuata mwenendo wao. Katika dua hii kuna ponya ya moyo wa Muislamu ya ugonjwa wa ukanushaji, ujinga na upotevu, na ni dalili kwamba neema kubwa zaidi kuliko zote ni neema ya Uislamu. Basi mwenye kuwa mjuzi zaidi wa haki na akawa mfuataji zaidi wa hiyo haki, basi huwa ni aula zaidi wa njia iliyonyoka. Na hapana shaka kwamba Maswahaba wa Mtume wa Allah Mtukufu, rehema za Allah Mtukufu na amani zimshukie, ndio watu aula zaidi wa hilo baada ya Manabii, amani iwashukie. Basi aya hii yaonyesha utukufu wao na ukubwa wa daraja yao, Allah Mtukufu Awe radhi nao. Ni sunna kwa msomaji aseme katika Swala baada ya kusoma Fatiha «Āmīn», na maana yake ni: Ewe Mola! Takabali. Nayo si aya katika sura ya Fatiha kwa maafikiano ya wanavyuoni. Na kwa hivyo wamekubaliana kwa umoja wao kutoiandika kwenye Misahafu.

Maana: Swahili Translation - Abdullah Muhammad and Nasser Khamis. Translated by Dr. Abdullah Muhammad Abu Bakr & Shaykh Nasser Khamis Toleo 1.0.1, 2026-03-12. QuranEnc.com

Al-Faatiha

Kiarabu ni maandishi ya Tanzil, bila kubadilishwa. Maana ni matoleo ya wachapishaji wake, bila kubadilishwa; wahakiki wa Sabīl wenyewe bado hawajazikagua. Kiarabu: maandishi ya Uthmani ya Tanzil, toleo la 1.1. Chanzo: tanzil.net