Ruka hadi kwenye maudhui
Tafsir As-Saadi - Swahili · An-Nisaa
Sura ya 4

An-Nisaa

Hii ni tarjama ya tafsiri ya as-Saʿdī kama IslamHouse.com inavyoichapisha katika saadi.islamenc.com, iliyosomwa kutoka kurasa za tovuti hiyo. Tovuti haisemi ni nani aliyeitafsiri kwa lugha nyingine wala inafuata toleo gani lililochapishwa, na haitaji masharti ya kuchukua matini yake, kwa hiyo haki ya kuionyesha haijathibitishwa. Hakuna aliyeilinganisha na kitabu kilichochapishwa, na hakuna mwanazuoni aliyeihakiki. Kila kifungu kipo kando ya aya inazozifafanua, ambazo ni matini ya Qur’ani ya Tanzil, inavyoonekana huko; aya ambayo tovuti haitoi ufafanuzi wake yenyewe inakaa pamoja na kifungu kilichotangulia, na faharasa inataja kila aya ya aina hiyo. Sabīl haikuandika wala kutafsiri kwa lugha nyingine chochote kati yake.

Maandishi kutokasaadi.islamenc.comIslamHouse.comnone stated (the site names no licence and no terms for taking its text)ilichukuliwa 2026-10-22

Aya ya 8

وَإِذَا حَضَرَ ٱلْقِسْمَةَ أُو۟لُوا۟ ٱلْقُرْبَىٰ وَٱلْيَتَـٰمَىٰ وَٱلْمَسَـٰكِينُ فَٱرْزُقُوهُم مِّنْهُ وَقُولُوا۟ لَهُمْ قَوْلًا مَّعْرُوفًا 8

{8} Na hii ni katika hukumu nzuri, tukufu, za Mwenyezi Mungu zenye kutuliza nyoyo. Akasema, "Na wakihudhuria ugawi" wa urithi "jamaa wa karibu" yani jamaa wa karibu wasiorithi kwa sababu fulani. Na kauli yake, "ugawi" ni kwa sababu warithi ni miongoni mwa wale wanaogawiwa urithi. "na mayatima na masikini;" yani, wale wanaostahiki miongoni mwa mafakiri. "Basi wapeni kwayo," yani, wapeni kilicho rahisi katika mali hii iliyowajia bila ya juhudi, wala taabu, wala shida, wala machovu. Kwa maana nafsi zao zinaingojea, na nyoyo zao zinaitazamia. Basi zitulizeni fikira zao kwa yale ambayo hayawadhuru, na yana manufaa kwao. Na inachukuliwa kutoka katika maana isiyokuwa ya moja kwa moja kwamba kila mtu ambaye anatazamia na anangoja kile kilichokuja mbele ya mtu inampasa kumpa kile kilicho rahisi kwake. Kama Nabii – rehema na amani za Mwenyezi Mungu ziwe juu yake – alivyokuwa akisema, “Mmoja wenu anapojiwa na mtumishi wake na chakula chake; basi na amkalishe pamoja naye. Na ikiwa hatamkalisha pamoja naye, basi na ampe tonge moja au matonge mawili;” au kama alivyosema. Na Maswahaba - Mwenyezi Mungu awe radhi nao – walikuwa yanapoanza matunda ya kwanza ya miti yao, wanamletea Mtume wa Mwenyezi Mungu – rehema na amani za Mwenyezi Mungu ziwe juu yake, – naye anayabariki na anamtazama mtoto mdogo zaidi ambaye yupo karibu naye. Na anampa hayo, kwa sababu ya kujua kungojea kwake kukubwa kwa hilo. Na yote haya ni ikiwa kuna uwezekano wa kupeana. Na ikiwa hilo haliwezekani kwa sababu ni haki ya wale wasiokuwa na uwezo wa kufanya uamuzi wa busara, au kuna kile ambacho ni muhimu zaidi kuliko hilo, basi na awaambie “kauli njema.” Yani, awajibu jawabu nzuri kwa kauli nzuri isiyokuwa chafu wala mbaya.