Aller au contenu
Tafsir As-Saadi - Swahili · Az-Zumar
Sourate 39

Az-Zumar

Voici une traduction du tafsîr d’as-Saʿdī, telle qu’IslamHouse.com la publie sur saadi.islamenc.com, lue dans les pages de ce site. Le site ne dit ni qui l’a traduite ni quelle édition imprimée elle suit, et n’indique aucune condition pour en reprendre le texte, si bien que le droit de la montrer n’est pas vérifié. Personne ne l’a comparée à un livre imprimé, et aucun savant ne l’a relue. Chaque passage se tient à côté des versets qu’il commente, qui sont le texte coranique de Tanzil, montré tel qu’il y est ; un verset auquel le site ne donne aucun commentaire propre se tient avec le passage qui le précède, et l’index nomme chacun de ces versets. Sabīl n’en a rien écrit ni traduit.

Texte desaadi.islamenc.comIslamHouse.comnone stated (the site names no licence and no terms for taking its text)pris le 2026-10-22

Verset 62

ٱللَّهُ خَـٰلِقُ كُلِّ شَىْءٍ ۖ وَهُوَ عَلَىٰ كُلِّ شَىْءٍ وَكِيلٌ 62

{62} Mwenyezi Mungu Mtukufu anajulisha juu ya ukuu wake na ukamilifu wake unaosababisha hasara kwa wale waliomkufuru. Akasema: "Mwenyezi Mungu ndiye Muumba wa kila kitu." Maneno haya na mengineyo yanayofanana na hayo ni mengi katika Qur-ani na ni katika mambo yanayoonyesha kwamba vitu vyote - isipokuwa Mwenyezi Mungu - vimeumbwa. Hili ni jawabu kwa kila mtu anayesema kwamba viumbe vingine ni vya azali, kama vile wanafalsafa wanaosema kwamba ardhi na mbingu ni za azali, na wale wanaosema kuwa roho ni za azali, na maneno mengineyo mfano wa hayo ya wana batili ambayo yanajumuisha kupinga kwamba si Mwenyezi Mungu aliyeviumba. Maneno ya Mwenyezi Mungu si katika vitu vilivyoumbwa. Kwa sababu maneno ni sifa ya yule aliyeyazungumza. Na Mwenyezi Mungu Mtukufu pamoja na majina yake na sifa zake, ndiye wa kwanza, na hakuna chochote kabla yake. Kwa hivyo, wana itikadi ya Muutazila walioichukua aya hii kuwa hoja juu ya suala kwamba maneno yake yameumbwa ni katika ujinga wao mkubwa zaidi. Kwani Mwenyezi Mungu Mtukufu hajaacha kusifika kwa majina yake na sifa zake, wala hakuna sifa mpya miongoni mwa sifa zake iliyojitokeza, na wala hajawahi kutosifika kwa majina yake na sifa zake katika wakati wowote ule. Ushahidi uliopo katika hili ni kwamba Mwenyezi Mungu Mtukufu alijulisha kuhusu nafsi yake Tukufu kwamba Yeye ndiye Muumba wa ulimwengu wote, wa juu na wa chini, na kwamba Yeye ndiye "Mlinzi juu ya kila kitu." Na ulinzi kamili ni jambo ambalo linalazimu kwamba mlinzi huyo ana elimu kamili juu ya kile anachokilinda na kukijua kwa kina, na kwamba anao uwezo kamili juu ya kile anachokilinda; ili aweze kukisimamia kwa kukihifadhi, na pia awe na hekima na ujuzi wa kukisimamia ili aweze kukisimamia na kukiendesha inavyofaa. Kwa hivyo, ulinzi hauwezi kukamilika bila ya haya yote. Basi chochote katika hayo kinapokosekana, basi kinakuwa kimekosekana katika hilo suala nzima. Tayari ilishajulikana na kuthibiti kwamba Mwenyezi Mungu ametakasika mbali na kila upungufu katika sifa zake zote. Kwa hivyo kujulisha kwake kwamba Yeye ndiye Mlinzi juu ya kila kitu kunaonyesha kwamba anajua kikamilifu vitu vyote, na kwamba ana uwezo wa kuvisimamia na kuviendesha, na kwamba ana hekima kamili ambayo kwayo anaviweka vitu mahali pake.